Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na uhai saa hizi tuko hapa tukiwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti. Naomba nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa ajili ya utalii. Tumeona jitihada kubwa amefanya kupitia Royal Tour, tumeona kazi kubwa sana, tumeona watalii wakija katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Waziri pamoja na watendaji kazi wake wote, Katibu Mkuu na wote wanaowasimamia katika Wizara hii. Kwanza kabisa, naomba niseme ndani ya Jimbo langu la Nsimbo, Mbuga ya Katavi ndiyo ilipo. Hii mbuga haitangazwi kabisa. Sasa Rais katuonesha mfano, kaonesha ubunifu, lakini ninamuamini Waziri wetu Mheshimiwa Mchengerwa, atafanya ubunifu ili Mbuga yetu ya Katavi iweze kutangazwa kwa sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa ndege Katavi upo, ndege zinafika, barabara kutoka kwenye uwanja wa ndege mpaka kwenye eneo letu la mbuga ni ya lami. Sasa sidhani kama kuna kitu ambacho kinaweza kushinidikana kufanya jitihada za kuhamasisha ili mbuga yetu iweze kutangazwa ili watalii waweze kufika Katavi kwa sababu, mazingira tayari yameshakuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji chetu cha Stalike kinapakana kabisa na Mbuga ya Katavi. Kuna mto ambao umetenganisha; naomba nimshukuru sana Kamishna Mwakilema, tumeongenaye amekubali kwenda kuongea na wananchi. Tatizo ni moja tu, wale wananchi toka mwaka 1974 katika ule mto, huko kijijini kabisa wanavua Samaki, lakini leo tumewazuia kabisa kuvua Samaki, nao ndiyo kipato chao cha uchumi. Sasa na Kata ya Stalike ndiyo inayoathirika kwa wanyama wakali. Wakulima wa Kata ya Stalike, wakilima mazao yao yote yanaliwa na tembo, wanaofanya vurugu katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni jambo la busara tu, sasa hivi twende tukakae tukaongee na wananchi wa Kata ya Stalike ili tuelewane. Kama ni kujengewa mabwawa, basi wajengewe mabwawa, kuliko kuacha na kuwazuia kabisa ili wasiweze kufanya shughuli zozote za kibiashara na kiuchumi katika Mto ule wa Stalike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni TAWA. Kuna msitu wa Ugara Game Reserve na Msitu wa Msimu Game Reserve. Wananchi walikuwa wanaenda mle ndani katika hayo maeneo kuvuna asali na wameweka mizinga yao ya asali, lakini leo TAWA wamewazuia kuingia kuvuna asali na vilevile wanawa-charge pesa. Akiingia na baiskeli analipa shilingi 10,000, akiingia na pikipiki analipa shilingi 30,000, wakiingia na gari wanalipa shilingi 50,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii misitu tumeikuta na hizi games tumezikuta, kama wananchi wa Ugalla wao katika Game Reserve ya Ugalla walikuwa wanaishi, ni maisha yao walikuwa wanaishi, ndiyo makazi yao. Wanafanya mila zao za jadi, leo tumewakuta tunawazuia wasifanye mambo yao ya jadi na mila zao. Vilevile kila akiingia atoe shilingi 10,000, akiingia na pikipiki shilingi 30,000. Najua Kamishna wa TAWA, Ndg. Nyanda ni msikivu. Ninavyoongea ananisikia, naomba twende tukakae na wananchi tuweze kukubaliananao ili waweze kupunguziwa ghasia hii ambayo wanaipata sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni TFS, wenzangu wengi wameongea. Nimi jimbo langu limezungukwa na misitu, lakini TFS ndiyo wanaolinda misitu na wananchi wanachotaka ni kitu kidogo tu, wanataka tuwape elimu, tuwashirikishe, tuwaoneshe mipaka kuliko kuwapiga na kuwa-fyekea mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Deus amesema hapa, wananchi wanalima. Sasa hivi TFS wametulia kimya. Saa hizi wametulia. Mvua zikianza kunyesha, wananchi wanalima, wanawatizama, mazao yakishakamilika ndiyo kipindi sasa cha kwenda kufyeka mazao yao na kuwanyanyasa na kuwapiga. Ni dhambi kubwa sana. Kwa nini tusiwaelimishe? Kwa nini tusikaenao kitako tukawaambia hapa ni mipaka yetu, hapa msiingie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tupo, watushirikishe, twenenao wakaongee na hao wananchi kuliko jinsi wanavyofanya. Wananchi wanateseka mpaka wanapata hasira na Serikali yao. Mheshimiwa Waziri tunajua wewe ni msikivu, tumekuona jitihada zako, kwa kipindi kifupi hiki tumeona kazi kubwa, miezi mitatu ulivyokabidhiwa Wizara tumeona jitihada zako. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, pita katika Mikoa yako yote yenye hifadhi ili uweze kuongea na wananchi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lupembe.

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie moja tu, kuna…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, tunakushukuru kwa mchango wako…

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo tu…

MWENYEKITI: …muda wako umekwisha.

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuunga mkono hoja.