Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuchangia katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kuweza kusimama hapa na kuchangia katika Wizara hii. Nashukuru sana Wizara kwa kufanya maboresho makubwa katika bustani ya wanyamapori iliyopo pale Tabora Mjini. Wamefanya maboresho makubwa pale wameongeza wanyama wa aina mbalimbali, sasa hivi kuna simba, kuna chui, kuna pundamilia, kuna fisi kuna nyani na kuna ndege wa aina mbalimbali wakiwepo aina ya tausi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Tabora tunashukuru kwa sababu lile eneo lilikuwa ni pori, pori kabisa na ni eneo la Mjini karibia na Hospitali ya Kitete. Kwa hiyo, walivyoweka ile bustani kwa upande wetu sisi kwanza kabisa tumeshapata maeneo ya utalii. Sasa hivi Tabora imefunguka barabara za lami ni nyingi, hata sasa wanaokwenda Mwanza, wanaokwenda Kigoma, wanaokwenda Shinyanga wanaokwenda Kahama lazima wapitie Tabora ndiyo waweze kufika kwenye maeneo yao kutokana na barabara kuwa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niseme tu tunaendelea kuwakaribisha sana watu wote wa Tanzania wanaopita katika Mkoa wetu wa Tabora. Sasa hivi tuna bustani nzuri ambayo kuna wanyama wa kila aina tunatangaza utalii wetu wa Tanzania. Niwashukuru sana TAWA lakini naomba kuishauri Serikali endeleeni kuboresha eneo lile hasa kwenye masuala ya miundombinu ili kuweza kuongeza vivutio pia kuongeza watu ambao wanaweza wakaja pale kwa sababu watavutika na mambo mengi ambayo yatakuwa pale. Naamini bado lakini mtakuwa kwenye process hivyo naomba sana Serikali iweze kuongeza ili tuweze kuwa na vivutio vizuri katika Mkoa wetu wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo kuhusiana na maslahi ya watumishi. Ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri, Serikali mmeunda Jeshi Usu, Jeshi hili linafanya kazi kwenye taasisi mbalimbali za Wizara hii, lakini wote wanafanya kazi ya aina moja. Changamoto iliyopo na ambayo mimi niliiona na mpaka sasa naomba niiseme ni utofauti wa mishahara kwa watumishi hawa. Haiwezekani hawa mnawapa hiki, hawa mnawapa hiki wakati wote wanafanya kazi ya aina moja. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali ili kuondoa huu mkanganyiko, ili kuondoa kuombwa kuhama hama kwa hawa wafanyakazi, kwa sababu wengi wanatoka kwenye eneo ambalo halina mshahara mzuri wanataka waende kwenye taasisi ambazo zinalipwa vizuri kama TANAPA na NCAA. Kwa hiyo, hawa wengine wanaona kwa nini wakati sisi wote tunafanya kazi moja. Kwa hiyo, ninaomba sana na niiombe Serikali angalieni maslahi ya watumishi hawa, wawe na maslahi ya aina moja ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi hizi kazi ni ngumu, ngumu kwa wote. Wanaolinda mapori kazi ni ngumu na wanalinda hizi hifadhi zetu kazi ni ngumu. Kwa hiyo, wapeni maslahi yao ya aina moja ili wote waweze kufanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusiana na mapori ya akiba kwenye Kanda yetu ya Magharibi. Kanda ya Magharibi tunayo mapori ya Luganzo, Tongwe, Igombe, Ugalla, Inyonga na Wembera, haya mapori yameshapandishwa hadhi. Pamoja na kupandishwa hadhi hifadhi hizi zinasubiri kukamilika kwa zoezi la mapitio ya mipaka, zoezi hili lilianza lakini lilisimamishwa. Kwa hiyo, tunaomba sana zoezi hili liendelee ili mipaka hii waipitie, wakishaipitia pawekwe zile beacon ili wananchi wetu waweze kupata maeneo ya kufanya kazi kwa utaratibu mzuri ili kuondokana na kugombana baina ya wahifadhi pamoja na wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ugomvi katika maeneo yao, hivyo tunashauri sana hii Kamati ambayo imeundwa, tunaomba sana iendelee na zoezi hili ili basi waweze kumaliza hii kazi na wananchi wetu waweze kuwa na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala lingine suala la Msomera. Kwanza kabisa mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuamua kwa dhati kabisa kutaka kuiponya Hifadhi yetu ya Ngorongoro. Wananchi wa Ngorongoro walioamua kuondoka wenyewe kwa hiari wameshafika Msomera, lakini hawa wafugaji wameniomba niwaombee wanachangamoto kubwa ya maji pamoja na maeneo ya malisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali kupitia Wizara hii wawafanyie kila linalowezekana wafugaji hawa, kwa sababu wao wanachotegemea ni mifugo yao. Kazi nzuri iliyofanyika, nyumba nyingi zilizojengwa na wananchi ambao wameshahamia kule wanachoomba wapewe maji pamoja na maeneo ya malisho, mifugo ndiyo kitu wanachokitegemea katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wengine ambao wapo kule Ngorongoro wamekaa wanasubiri, Mheshimiwa Waziri kupitia Wizara yako tunaomba sana wale ambao tayari wanasubiri kwa hiari yao kuondoka kule kurudi huku fanyeni kila linalowezekana, malizeni huu mpango ili kuweza kuunga mkono juhudi za Mama. Kuweza kuhifadhi zaidi Mbuga yetu ya Ngorongoro na kuweza kuwa salama. Tulikuwa tukienda Ngorongoro unaanza kukutana na kondoo, ng’ombe, mbuzi lakini sasa hivi angalau hawajaisha lakini angalau kumepungua hata ukipita unaanza kuona, unajua kwamba kweli sasa hili ni eneo la uhifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba na mazungumzo pia yaendelee hata kwa wale ambao bado hawapo tayari muendelee kuwaomba siyo kuwalazimisha kama ambavyo mmefanya tangu mwanzo ili waendelee kuhama wenyewe kwa hiari, waweze kuondoka pale na waweze kwenda Msomera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msomera sasa hivi shule zipo, tumeona kuna zahanati, tumeona kuna kila huduma za kijamii. Sasa changamoto iliyopo wapewe maji pia wapewe na maeneo ya malisho ili wasipate hamu tena ya kurudi Ngorongoro na kuanza tena kufukuzana kama ambavyo watu wanatarajia. Kwa sababu hili zoezi siyo watu wote walilipenda, hasa hata wenzetu majirani walilichukia na matokeo yake walianza kama kufanya hujuma lakini Mungu amebariki msimamo wa Rais wetu umekwenda vizuri na leo watu wengi wako Msomera kwa hiari yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalizungumza hili kwa sababu nilikwenda na nimejionea mwenyewe na tumpongeze sana Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya aliyeko sasa kwa kazi nzuri anayofanya ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kuwa na utulivu na wanaendelea kupata mahitaji yao katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya muda naomba kushukuru kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)