Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia asubuhi ya leo. Nianze kwa kuungana na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanampongeza sana Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa kazi kubwa, ubunifu na uzalendo mkubwa aliounesha katika utendaji wake Serikalini tangu alivyoanza kuteuliwa kwenye Wizara mbalimbali na sasa kwenye Wizara hii, Mheshimiwa Mchengerwa ameonyesha ubunifu wa hali ya juu sana na mimi nina mpongeza sana huyu Babu yangu kutoka Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane pia na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Naibu Waziri Mary Masanja, mpambanaji huyu mama, amefika mpaka Madaba na amefanya kazi na Wanamadaba pamoja na Wanawino kwa kweli mchango wake kwa Taifa letu hautasahaulika na hasa kwa Wanamadaba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninayo mambo machache ya kuchangia lakini niliona ni vema nikaanza kuwapongeza na kuwashukuru viongozi hawa wakubwa wa Wizara hii na katika orodha hiyo naomba uniruhusu nimuunganishe na Mkurugenzi Mkuu wa TFS, Dos Santos Silayo ambaye anafanya kazi kwa karibu sana na Mhifadhi Mkuu wa Shamba letu la TFS lililopo Wino, Madaba, kwa uzalendo mkubwa sana waliouonesha kwa wananchi wa Madaba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapompongeza Ndugu Silayo na Dada yetu Glory Kasmiri ambaye ni Mhifadhi Mkuu wa Shamba letu la Wino, ninakumbuka na kutambua mchango mkubwa sana wanaoutoa kwa wananchi wa Madaba. Moja, ieleweke kwamba Mheshimiwa Waziri nadhani unajua kwamba Shamba la Wino la TFS liko katika Halmashauri ya Madaba na shamba lile lina hekta 39,711. Shamba hili linagusa vijiji vitatu muhimu, Kijiji cha Wino, Ifinga na Mkongotema. Kazi inayofanyika kwenye shamba hili ni kubwa na uwekezaji uliofanyika kwenye eneo hili ni mkubwa na shamba hili linaweza likashika nafasi ya tatu hadi ya tano Kitaifa. Kwa hiyo, mnaweza mkaelewa ni ukubwa gani wa uwekezaji umefanyika katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru viongozi wangu hawa kwa kusaidia pia shughuli zingine za maendeleo ambazo wanazifanya kwenye Vijiji vya Wino, Ifinga na Kijiji cha Matetereka. Natambua michango ya cement, natambua mchango wa mabati, natambua mchango wa wajasiriliamali, vifaa vya kuvunia asali lakini mitaji na vifaa vya kufuga nyuki kwenye misitu. Kazi inayofanyika ni kubwa nilitamani niwashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua miche mingi ya miti mnaizalisha na mnagawa kwa wananchi hawa kupitia programu yetu ya panda miti kibiashara, wananchi wa Madaba wamepata miche mingi sana na tunaendelea kupanda, nitumie fursa hii kutoa wito kwa Wanamadaba tuendelee kupanda miti kwa bidii kubwa kwa sababu miaka 10 ijayo Madaba itakuwa moja katika Halmashauri tajiri sana hapa Tanzania, tutakuwa tunafukuzana na Halmashauri ya Mafinga, kwa hiyo niwaalike sana Wanachi wa Madaba kutumia hii fursa ambayo tunaipata TFS kwa ajili ya kuandaa na kukuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba pamoja na kazi nzuri ambayo tumeifanya kupitia TFS Madaba, huduma kwa wananchi, tunazo hifadhi na maeneo ambayo yanafaa kuwa hifadhi ya wanyapori. Tumeleta kwako kupata kibali cha kuanzisha Hifadhi ya Wanyamapori Ifinga. Mheshimiwa Waziri naomba nikufahamishe kwamba Ifinga ni Kijiji ambacho kinapakana na Hifadhi ya Mwalimu Nyerere au Selous katika maeneo hayo lakini tunapakana na Malinyi. Tunayo hifadhi kubwa ambayo tulitamani hifadhi hii ichangie kwenye Pato la Kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kijiji ni maskini sana ukilinganisha na vijiji vingi Tanzania, ndiyo kijiji pekee ambacho ndicho kijiji na Kata yaani tuna Kata na kijiji kimoja ndicho hicho hicho. Hawa wako mbali sana hawafikiki kirahisi. Tunayo changamoto ya barabara, tunayo changamoto ya kipato cha wananchi, tunayo changamoto ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali. Tumeomba Mheshimiwa Waziri utusaidie eneo hili lina heka 37,225 tunaomba eneo hili litumike kuwa hifadhi ya jamii kwa maana ya WMA. Hatua zote tumezimaliza tunachosubiri ni Wizara yako itume wataalamu wakafanye tathmini ya utoshelevu na mahitaji mengine ya eneo hilo lakini tunaomba sana Mheshimiwa Babu yangu Mchengerwa tupe eneo hili tukafanye hifadhi ya wanyamapori ili kuchangia kipato cha wananchi wetu na kuchangia uhifadhi hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba bonde hili linachangia sana maji yanayoenda Rufiji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, ushiriki wa wananchi katika kuhifadhi maeneo haya kama ambavyo tumefanya kwenye misitu ni ushiriki wa wananchi katika kuchangia kuhakikisha kwamba tunahifadhi Bwawa letu la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Halmashauri ya Madaba inapakana na Hifadhi ya Mbarang’andu, hifadhi hii ipo ndani ya Halmashauri ya Namtumbo lakini kuna Kijiji cha Ngadinda, Kijiji cha Mbangamawe, Kijiji cha Lutukila. Vijiji hivi vyote vinapakana na hifadhi hii na vijiji hivi vyote wananchi wake wameshiriki katika kuhifadhi mazingira ya eneo hili. Tunaomba basi kunapokuwa na gawio linalotokana na mapato ya WMA vijiji hivi vitatu vinufaike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Kijiji cha Ngadinda kimepoteza mpaka miundombinu ya umwagiliaji ambayo ilijengwa kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa wananchi wale. Ile miundombinu ya umwagiliaji imeangukia kwenye eneo la WMA na wananchi wanashindwa kulitumia, basi mapato yanayotokana na uhifadhi huo yakasaidie maendeleo ya wananchi wetu wa Ngadinda, Mbangamawe na Lutukila. Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa maslahi ya muda nikuombe sana hiki Kijiji cha Hifinga kama nilivyokwambia huko nyuma miaka ya 1950 kilikuwa kwenye Wilaya ya Ulanga, kwa hiyo hakikuwa Songea. Sasa kimekuwa adopted Songea kwa sababu ya mazingira yake ya kijiografia. Tumepata wawekezaji kama SUA wana hekta 10,000 za kupanda miti. Tuna KKKT, hawa hawajafanya lolote lakini wana eneo kubwa sana wamelichukua kutoka kwa wananchi. Tunayo program ya FDT Concession lakini tuna Mufindi Wood Poles.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wadau ambao ninawashukuru sana mbele yako nimetamka kuhusu TFS, na Mufindi Wood Poles ninawapongeza sana kwa kuchangia sana maendeleo ya kijiji kile sasa tunajenga kituo cha afya kwa kupitia mchango wa wadau hawa. Ninawashukuru na ninawaomba waendelee, SUA tunawashukuru kwa sehemu wameanza kufanya sehemu fulani lakini bado ahadi zao hazijatekelezwa kwa asilimia 100. Ninaomba ushirikiane nasi kuwataka wadau wote waliowekeza kwenye kijiji cha Ifinga waliochukua ardhi ya kijiji cha Ifinga wakatekeleze ahadi zao na wakapande miti. Kama hawatafanya hivyo Mheshimiwa Waziri tutaomba ushauri wako ili maeneo haya muhimu yarudi kwa wananchi ili waweze kunufaika nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mheshimiwa Waziri ninarudia kukupongeza na ninakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Ahsante sana. (Makofi)