Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mvomero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Maliasili, pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya uzima. Nami nielekeze mchango wangu moja kwa moja bila kupoteza muda kwenye Wizara yetu hii ambayo ni muhimu sana kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze na mimi kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa Royal Tour ambayo imefanya vizuri na imeongeza watalii wengi sana katika nchi yetu. Pia nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wako kwa kazi kubwa na nzuri ambazo mnazifanya katika nchi hii, katika kipindi kifupi nafikiri miezi mitatu na siku kadhaa tumeona mabadiliko makubwa na sisi tunaimani sana na wewe. Nikuambie Mheshimiwa Waziri nilipanga kushika shilingi leo lakini kwa namna ambavyo nakuamini nina imani yote ambayo umetuambia yatakwenda kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu nataka kuboresha tu kwenye hotuba yako ili uweze kuona namna nzuri ya kutusaidia watu wa Mvomero. kwanza ni suala la Tembo.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2021 nilichangia kwenye Wizara hii ya Maliasili kwenye upande wa tembo, mwaka 2022 nilichangia na leo 2023 hakukuwa na utekelezaji wa aina yoyote lakini nina imani kama nilivyosema sasa unakwenda kutusaidia na kutatua changamoto tulizo nazo katika Wilaya yetu ya Mvomero.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri sasa hivi tembo katika nchi hii wana thamani kuliko binadamu, wenzangu wengi waliochangia hapa wameeleza kwenye maeneo yao namna ambavyo tembo wanawasumbua wananchi. Mvomero tumepakana na Hifadhi ya Mikumi, mpaka nazungumza hapa Mheshimiwa Waziri, tembo wameshaua wananchi 37. Wananchi wameshapoteza Maisha 37 kwa kipindi kifupi tu, wiki mbili zilizopita tumetoka kumzika ndugu yetu pale Mkata ameuawa na tembo.
Mheshimiwa Spika, pia wananchi ambao mashamba yao yameharibiwa na hawa wanyama ni zaidi ya 2,500, hakuna chochote walicholipwa. Tunajua hakuna fidia kuna kifuta machozi na kuna kifuta jasho ambacho kwanza ni kidogo sana, leo mwananchi shamba lake likiharibiwa na tembo anatakiwa ekari moja alipwe laki moja, tunafahamu gharama za kutayarisha shamba, gharama za kupanda, kulima, mpaka kuvuna, leo shamba likiharibiwa na tembo anatakiwa kulipwa kiasi kisichozidi laki moja.
Mheshimiwa Spika, pia mwananchi ambaye ameuawa na tembo familia yake inatakiwa kulipwa kifuta machozi kisichozidi milioni moja. Hizi ni kanuni zilizopitwa na wakati Mheshimiwa Waziri, tunawaumiza wananchi na hawa wananchi siyo kwamba wanataka hizi fidia, siyo kwamba wanataka hiki kifuta machozi na kifuta jasho, wanataka kuishi kwa amani hawataki kuishi na tembo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashangaa naomba leo nizungumze kwa kawaida tu, hivi Serikali imeshindwa kweli kuwarudisha tembo na kuwapeleka kule kwenye hifadhi? Ina maana kwamba hawa watalii ambao wanakuja kwenye hizi hifadhi zetu hawariziki na wale tembo ambao wako mle kwenye zile hifadhi? Sasa hawa tembo ambao wako nje ya hifadhi wanafanya nini Mheshimiwa Waziri? Watu wanaisha, watu wanapotea na hawo ni Watanzania wenzetu! Kifuta machozi chenyewe na kifuta jasho ni kidogo na hawalipwi kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mvomero toka mwaka 2019 mpaka leo hakuna mtu aliyelipwa, lakini inaonesha Serikali inathamini sana tembo kuliko binadamu. Niliona kwenye hotuba yako kwamba utakuja sasa na sheria mpya ambayo itaweza kuwasaidia wale wananchi ambao wanakutana na hii adha ya tembo na tuondokane sasa na haya mambo ya kikoloni, haya mambo ya kulipana laki moja na milioni moja yalishapitwa na wakati. Tembo akienda kufanya uhalibifu kwenye maeneo ya wananchi kuwe na sheria ya kumlipa mwananchi fidia siyo kifuta machozi na kifuta jasho kama vile hisani, kuwe na fidia ambayo atakwenda kulipwa huyo mwananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri, mimi nina ushauri na sidhani kama Serikali mnashindwa, hivi ile Hifadhi ya Mikumi, sisi tuna Kata Saba ambazo zimepakana na Hifadhi, wale tembo waliopo kwenye hizi Kata Saba kwenye hii Tarafa ya Mlali, hivi mkiwarudisha kule halafu mkaweka fensi kwenye ile hifadhi hata zile fensi za umeme ambazo mnazipa umeme baadae mnyama akitaka kwenda kugusa fensi anapigwa shot anarudi, hivi Serikali na yenyewe inashindwa kuweka hizi fensi?
Mheshimiwa Spika, mbona wananchi wa kawaida katika maeneo mengine wanaweka hizi fensi? Ama kuchimba mtaro mkubwa ili wanyama wasiweze kuvuka na lenyewe linashindikana hili? Wako wakulima wetu katika Tarafa hii ya Mlali wana mashamba lakini wamezungusha fensi wamechimba mifereji hakuna mnyama anayeingia katika mashamba, sasa nashindwa kuelewa Serikali inashindwaje kuweka fensi hata ya waya wa umeme wa kuzuia wanyama hawa wasiende kwenye maeneo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tembo ni wengi sana, wananchi sasa hivi hawalimi Kata ya Doma pale Kijiji cha Doma kule Mahalaka hali mbaya, hakuna mwananchi anayelima na kule tunajua wananchi wetu wanajishughulisha na shughuli za kilimo, kuna kilimo cha biashara wanalima nyanya na kuna kilimo cha chakula, pale Msongozi, Mkata, Mangaye Kata nzima ile hakuna mwananchi analima, Merela hakuna mwananchi yeyote analima, Rubungo na Mlali yote kwa ujumla hakuna mwananchi anayelima. Sasa Mheshimiwa Waziri ninakuomba na kwa sababu ninakuamini na hata ulivyoteuliwa kwenye Wizara hii mimi nilinyoosha mikono juu na kumshukuru Mungu kwamba matatizo haya sasa yanakwenda kuisha. Nimeona kwenye hotuba yako umesema Tanzania kwa Afrika tumekuwa watu wa tatu kama sikosei kwa kuwa na tembo wengi, Kimataifa huko tuna sifa kubwa ya kuhifadhi tembo lakini hawa tembo ambao huko nje tuna sifa huku ndani wanaua wananchi.
Mheshimiwa Spika, ninaomba sana, naomba shughulikia masuala haya ya tembo. Pia nikupongeze nilikuomba siku moja unisadie tuweze kukutana na watu wa TAWA na ukatoa maelekezo tukakutana na watu wa TAWA tukafanya kikao kama wiki tatu zilizopita. Kikao kile nina imani kama yale tuliokubaliana yatatekelezeka hii changamoto kama siyo kuisha inakwenda kupungua kwa kiasi kikubwa, ninakupongeza sana kwa hilo.
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri sisi Mvomero tuna hifadhi ya Wami Mbiki na kuna Hifadhi ya Msitu. Hifadhi hii ya Wami Mbiki ni hifadhi ambayo ina migogoro na wananchi wanaopakana na hii hifadhi kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesema toka nimekuwa Mbunge na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais ile timu ya Mawaziri Nane, pamoja ya kwamba hii timu imekwenda kukagua yale maeneo na kuanza kupima. Mimi kama Mbunge sijui na wananchi hawajashirikishwa lakini tuna imani itakwenda kututendea haki, nimeona kwenye hotuba yako ulisema utawaagiza Wakuu wa Mikoa haraka iwezekanavyo waende wakamalize haya matatizo ya mipaka katika hizi hifadhi. Mimi nina imani pale katika Hifadhi yetu ya Wami Mbiki tunakwenda sasa kumaliza yale matatizo ili wananchi wetu sasa waweze kulima kwa uhuru. Wamekuwa wakinyanyasika miaka yote, wamekuwa wakinyanyasika kila siku wanashindwa kujua hatma yao lakini kwa maelekezo yako nina imani mambo yanakwenda kukaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tuna Hifadhi ya Msitu wa Magote, hii hifadhi ilianzishwa mwaka 1940. Wananchi wameishi ndani ya hii hifadhi katika kipindi chote, kuanzia mwaka 1940 mpaka leo wananchi wapo kwenye ile hifadhi na watu wamezikana mababu na mababu katika ile hifadhi. Leo Serikali inataka kuwaondoa hawa wananchi ili hifadhi hii sasa waanze kupanda miti watu wa TFS, wakati hifadhi hii eneo lote la hifadhi kuna shughuli za kijamii na watu wamejenga, watu wamezikana, hakuna eneo lililobakia. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri hifadhi hii ni hifadhi ndogo sana, ipo pale Jongoya. Ninaomba busara zako utusaidie hifadhi hii wapewe wananchi ili tuweze kuondokana na adha. (Makofi)
SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)