Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi na nianze na kumshukuru Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Rais alipokuja kutafuta kura moja ya jambo alituahidi pale ilikuwa ni barabara ya Mwandiga - Chankele – Kagunga. Naomba atakapokuja kujibu hoja utuambie status ya barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Rais alipokuwa Simbo alisema atatupa kilometa kumi za lami kutoka Simbo – Ilagala. Naomba Waziri atakapokuja kujibu hoja napo utusaidie status ya suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Mheshimiwa Rais aliongelea suala la kuwalipa fidia wale ambao hawakulipwa kwenye barabara ya Mwandiga - Manyovu. Nalo naomba kujua status yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, nataka nipate status ya gati la Kagunga na watu wanaolipwa fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa ambalo leo nadhani nitatumia muda wangu mrefu ni suala la viwanja vya ndege na ATC pamoja na reli. Reli ndiyo inayoweza kukuza uchumi wetu kwa haraka sana. Mimi naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kama kuna jambo ambalo Rais Magufuli ataenda kwenye historia ya miaka 100 ni kujenga reli kwa kiwango cha standard gauge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la reli ni legacy ya Rais Magufuli. Mimi namuomba Waziri, unless hataki tuandike legacy ya Mheshimiwa Rais Magufuli, naomba tujenge reli ya kiwango cha standard gauge kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Mwanza, kutoka Tabora kwenda mpaka Kigoma, kutoka Isaka kwenda Keza, kutoka Kaliua kwenda Mpanda, Mpanda kwenda Karema na Uvinza kwenda Msongati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tubadili tabia, tukienda kwa hali hii tutaongea tutamaliza miaka mitano hatujaanza kujenga. Nchi zinazotuzunguka za Afrika, Kenya ilikuwa ni jambo la siku mbili, tatu leo wanajenga reli yao, Uganda nao wanajenga, Ethiopia wamejenga, Senegal wamejenga na wote hawa wamekwenda China kuchukua fedha. Naomba sana Mheshimiwa Waziri najua atasema ameweka shilingi trilioni moja, trilioni moja huwezi kujenga reli hii. Ni matarajio yangu shilingi trilioni moja hii ni sehemu ya fedha ya Serikali kama mchango wetu kwenye huo mpango mkubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nawaombeni watu wa Wizara, Rais Magufuli tutamtofautisha na Marais wote tukijenga reli. Akijenga barabara na Kikwete alijenga, Marais wote walijenga barabara. Tunachotaka Rais Magufuli fanyeni kila mnaloweza tuache longolongo tujenge reli kwa standard gauge. Naomba Waziri unapokuja kujibu hapa atuambie jambo ambalo linaeleweka. Kama anakuja anasema anataka watu washindane, naombeni tusiwe wafungwa wa sheria zetu, hili suala ni la uchumi, ni la maendeleo, naomba tujenga reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ndege, mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri ameanza kutengeneza ndege, lakini naomba tuseme tunataka kujenga airline ya namna gani? Kama tunataka kujenga airline kwanza lazima tuje na Shirika la Ndege ambalo ni imara. Wengine wanasema hamna wapanda ndege, ngojeni niwaambieni, tukiweka viwanja vya ndege mikoa yote, bei za ndege zitashuka na watu wote watapanda ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena mimi nachosema mikoa ambayo imeanza juzi ya Geita, Simiyu, Katavi, Songwe tujenge viwanja vya ndege. Viwanja vya Bukoba, Kigoma, Tabora, Singida, Dodoma vyote vijengwe. Tukishakuwa na viwanja tukawa na network, hilo shirika letu la ndege la ATC likawa lina-fly mikoa yote, kitakachotokea bei zitashuka, watu wengi watapanda ndege na shirika hili litapata faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mikoa lazima tujenge viwanja vya ndege, hiyo mikoa mipya ya wenzetu, Shinyanga tujenge, kiwanja cha Mwanza ni muhimu sana, tupanue kiwanja cha Kigoma na tupanue kiwanja cha Tabora. Kwa kufanya hivyo, tunayo hakika hili shirika tunalotaka kutengeneza litakuwa na maana na litatupeleka mbele tutapata faida. Kama unaleta shirika la ndege unataka ukashindane na mashirika yaliyoanza muda mrefu umeanza na kushindwa. Lazima tuanze kwanza ndani ili kama walivyosema wenzangu, leo unakwenda unapanda FastJet kweli inaonekana bei rahisi lakini ukiwa na begi unalipa shilingi 100,000 au shilingi 200,000 inawezekanaje? Siyo ndege rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata tiketi yenyewe wanakuambia labda ni shilingi 90,000, unakuta tiketi za bei hiyo ni nne au tano nyingine zote ni za shilingi 400,000 mpaka shilingi 500,000, ni kwa sababu hatuna ushindani. Anayeweza kuleta ushindani ni shirika letu la ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la minara vijijini. Nimesoma hapa suala la UCSAF naona Wazri sasa hivi halichangamkii sana. Tulianzisha sheria hapa, tukasema tuweke huko ili UCSAF wapeleke minara vijijini. Haiwezekani minara tukaletewa na hawa Halotel, Halotel ni wafanyabiashara kama yalivyo makampuni mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni kama Serikali tuendeleze mipango yetu ya kuhakikisha tunawapa fedha watu wa UCSAF ili kasi ya kuleta minara iwe kubwa. Mheshimiwa Waziri anajua kuna vijiji vyangu vya Kata ya Ziwani, vijiji vyote saba hakuna minara na tumelisema hili, tunaomba sasa lifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la bandari ya Dar es Salaam. Kuna kitu kinaitwa VAT kwenye transit cargo, Waziri najua atajibu atasema VAT haitozwi lakini kwenye sheria ipo, tuliipitisha mwaka jana kwenye Finance Act. Kwa sababu tuliipitisha mwaka jana, yule anayetaka kutumia bandari ya Dar es Salaam anachukua sheria, una muda gani kwenda kumwambia hatutozi. Tuitoe kwenye sheria ili wajue hakuna VAT kwenye transit cargo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ni ushindani, naombeni sana tuiache bandari ya Dar es Salaam ifanye biashara kama biashara zingine zozote duniani. Kama kuna sehemu tunatakiwa tusiweke siasa ni kwenye bandari ya Dar es Salaam. Tumecheza na siasa, tulianza mwaka 2008 tunaongelea habari ya gati 13 na 14 leo ni mwaka 2016 hatujajenga. Tulikwenda China na watu wa Mombasa, Mombasa wameshamaliza kujenga wanaanza kwenda Lamu, sisi bado tunajiuliza tu tutumie modal gani. Nadhani muda umetosha, nakuomba sana Waziri umefika wakati tuache siasa kwenye suala la bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ya Dar es Salaam lazima itafute masoko, lazima waende huko kwenye masoko wakaiuze bandari. Naombeni muondoe urasimu ili watu wa masoko waende huko, ndiyo kazi yao kwa sababu tunashinda, mzigo wenyewe siyo mwingi sana duniani. Ni kweli sasa hivi kuna downturn ya economy duniani, mzigo umeshuka lakini sisi hata kama mzigo umeshuka duniani lazima kuwe na sababu za kwetu, kama sisi hatutekelezi majukumu yetu kwetu utashuka zaidi na Mungu ametupa bandari hii tuitumie kwa maendeleo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri atakapokujibu hoja atuambie kwa uhakika tuweze kumwelewa lini tunaanza ujenzi wa reli ya kati? Lini tunaanza kuandika historia ya Rais Magufuli ya miaka 100 ijayo ya kujenga reli ya standard gauge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja.