Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nije kwenye suala la pongezi. Pongezi nyingi sana kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi aliyoionesha na dhamira ya dhati kabisa ya kuutangaza utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara. Lakini kwa niaba ya wananchi wa Buchosa naomba nitoe shukrani sana kwa Wizara kwa kutujengea vizimba viwili kuzuia wananchi wetu wasiliwe na mamba.

Mheshimiwa Spika, hapa ndani leo imekuwa ni suala la ndovu kila kona, lakini napenda niwaongezee suala la mamba. Kule ninapotoka mimi wananchi, hasa akina mama, wanaliwa sana na mamba, na kimekuwa kilio changu sana kwenye Wizara. Ombi langu kwa Wizara ituongezee vizimba vingine vya kuzuia watu wasiliwe na mamba hasa maeneo ya kuchota maji na maeneo ambayo watu wetu wengi wanakwenda kuoga nyakati za jioni. Hayo ndiyo mambo ambayo wananchi wa Buchosa wamenituma.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni maeneo ya hifadhi. Tunacho Kisiwa cha Maisome ambacho wananchi walikuwepo baadaye tukaja kupima eneo tukasema hii ni hifadhi, idadi ya watu imeongezeka, wananchi wanaomba kukatiwa kipande kidogo kwenye eneo la hifadhi ili waweze kupata maeneo ya kufuga mifugo yao na hata maeneo ya kuishi.

Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo kwenye Kisiwa cha Kome, na kwenyewe kuna tatizo hilo. Wananchi wanalalamika eneo la hifadhi lipo, idadi ya watu imeongezeka lakini hawana sehemu ya kujenga na pia kulisha mifugo yao. Kwa hiyo kila siku ng’ombe wanakamatwa wanapigwa faini 100,000 kwa ng’ombe, kwa hiyo naiomba Serikali hii sikivu, Mheshimiwa Waziri tulishazungumza, nikuombe sana suala hili uzingatie na ninakukaribisha Buchosa uje ujionee mwenyewe, umeniahidi kuja wananchi wanasikia, nakukaribisha sana Buchosa uje ujionee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Wizara hii ni suala la biashara kabisa asilimia 100. Uhifadhi, lakini tunawezaje kupata fedha kutoka kwenye uhifadhi, tunawezaje kugeuza Hifadhi zetu za Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, wanyama kama tembo, simba waweze kuwa fedha. Hilo ndilo jambo ninalotamani kuliona. Nataka kuona fedha katika nchi hii ili ziweze kusaidia juhudi za maendeleo kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nimefanya utafiti kidogo na nimegundua kabisa ya kwamba kila unapo-double juhudi za kutangaza biashara ya utalii mapato yanaongezeka. Sasa, nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri nikakutana na maandishi yanasema kama ifuatavyo: -

“Bila kutangaza sana bado tumeweza kufikia kiasi cha pato la Taifa asilimia 21 kutokana na utalii.” Bila kutangaza sana, bila promotion hii ni bahati kubwa sana, haitokei mahali popote duniani, yaani kwenye ulimwengu huu tulio nao wa leo unasema bila kutangaza sana tumefanikiwa. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba kama Waziri angetangaza sana, mapato yangeweza kuongezeka na hicho ndio kimenisimamisha hapa kuongea leo.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba siridhishwi kabisa na investment iliyofanyika kwenye suala zima la kutangaza utalii wetu. Tanzania katika dunia ni Nchi ya pili kwa vivutio vya asili ikiongozwa na Brazil. Tanzania ni Nchi ya kwanza Afrika kwa vivutio vya kiasili, nchi ya kwanza lakini angalia mapato yake. Mapato yake ni kidogo sana. Kama Taifa tunaweza kusema bado GDP ratio inaturuhusu kukopa. Tuna asilimia 40 tu, wenzetu wana asilimia 77, lakini je, tutegemee mikopo kila mara na utajiri huu tulionao? Ningetamani siku moja nchi yangu isikope, iweze kutumia zawadi ambazo Mungu ametupa kuendesha nchi yetu na inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikusomee data moja hapa, data moja rahisi tu. Baraza la Utalii Duniani (WTTC) mwaka 2019 lilisema maneno yafuatayo, Idara ya Utalii Tanzania iliingiza dola bilioni 6.7 mwaka 2019, bila kutangaza tunaingiza fedha hizi tuki-double itakuwa bilioni 13. Fedha hizo ukizijumlisha kwa ujumla wake ni trilioni 16. Shilingi trilioni 16 hiyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, namalizia. Shilingi trilioni 16 hiyo deficit kwenye bajeti yetu sisi ni shilingi trilioni 10 ingeweza kuziba debt…tusikope. Ombi langu juhudi za kutangaza ziongezeke, tusiridhike na mambo ya bila kutangaza tumefanikiwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)