Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupewa nafasi. Niungane na wenzangu kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo wamefanya katika kuifufua Sekta hii ya Utalii ambayo ilikuwa imeathirika kwa kiwango kikubwa sana kutokana na Covid-19. Sote tunajua kwamba mwaka 2019/2020 watalii walishuka mpaka chini ya 600,000 lakini jitihada kubwa zimefanyika ambazo zimepelekea idadi ya watalii imeongezeka mpaka kufikia 1,500,000 mwaka 2021 na taarifa ya sasa hivi inaonesha wamefika milioni 3.8. Ni hatua kubwa Serikali wamefanya wakiongozwa na Rais wetu mpendwa mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kweli hongera sana kwa kazi hiyo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtalii ni nani? Mtalii ni mtu yeyote anayeweza kusafiri kutoka sehemu anakoishi akaenda sehemu nyingine kwa lengo la kupata burudani, kwa lengo la kwenda kujifunza, kwa malengo mengine. Unaenda sehemu nyingine kwenda kula Maisha, huo ndio utalii. Kwa hiyo tunahitaji tuwe na mikakati ya kuwawezesha watalii waka-enjoy, wakale maisha. Tunahitaji utalii wa wanyamapori, jitihadi lazima zifanyike idadi ya watalii wa wanyamapori iongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utalii wa milima pia uongezeke, nchi yetu ina milima mingi. Utalii wa miamba kama vile Olduvai Gorge lazima watalii waongezeke, tunayo miamba mingi nchi hii. Utalii wa mikutano mbalimbali inayofanyika katika nchi hii, lazima tuwekeze ili tuwe na mikutano ya aina mbalimbali kuvutia watalii. Tunahitaji utalii wa misitu, utalii wa matibabu, hospitali mbalimbali ambazo sasa hivi tunaboresha huduma tutapata watalii kutoka nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, tunahitaji vilevile watalii wa vyuo kuja kusoma na kuja kujifunza. Tunahitaji utalii wa fukwe na utalii wa mambo mengine mengi. Wote huu ni utalii, lakini maana ya utalii tunaupima kwa kuangalia idadi ya watu waliokuja wa ndani na wale wa kutoka nje, lakini na kiasi cha fedha killichoingia katika uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, ili tuweze kupata fedha za kutosha tunahitaji kuwekeza, lazima tuwekeze vya kutosha. Tuwekeze kwenye kujenga hoteli, kujenga kumbi za kitalii, kumbi zitakazovutia watu mbalimbali kuja kufanya mikutano hapa. Tunahitaji kuwekeza kwenye miundombinu, tunahitaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali kuvutia watalii kutoka nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ili tufanikiwe tunahitaji kuboresha huduma. Sasa hivi huduma zetu katika meneo mengi ya utalii kwenye mahoteli bado hazijawa vizuri. Ni wajibu wa Wizara kuhakikisha inaboresha haya ili tuvutie watalii walio wengi. Tumeona kulikuwa na programu ile ya kuboresha utalii kusini ili kuhakikisha nchi yetu inapata katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na programu ya REGROW ambayo ilikuwa na dola za Marekani 150. Toka wakati ule mpaka leo ile programu bado haijafanikiwa. Kule kusini hatujatangaza ipasavyo vivutio na maliasili tulizonazo. Kule Mbozi tuna kimondo kizuri, hapo Iringa tuna Ruaha, tuna Mikumi, tuna Rungwe tuna milima, tuna wanyama, tuna kila aina ya vivutio. Lazima tuwekeze ili tuhakikishe kwa kweli na huko zinapatikana fedha zitakazotoa mchango mkubwa katika kuijenga nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kuna Ruaha kule, kuna maeneo mengine Rungwe kule kuna mlima na kuna kamto fulani kamuhimu sana, kana historia nzuri sana, kuna utamaduni. Kwa utajiri mkubwa huu tulionao nchi yetu tunahitaji kuwekeza. Tukiwekeza sekta zikajipanga vizuri nchi hii tutapiga hatua kubwa na tutapata maendeleo makubwa sana. Kwa hiyo, kazi ya Wizara ni kuhakikisha ina-coordinate sekta zote hizi tuwekeze. Tufanye kazi kwa pamoja ili nchi iende mbele na sisi tuone manufaa ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, tunahitaji kuwekeza zaidi, angalia royal tour. Tumetangaza kwa royal tour imeleta impact, je, tukitangaza? Sasa Wizara wajiongeze basi, waende sasa wakatangaze na maeneo mengine. Royal tour ni moja, je, maeneo mengine tumeyatangazaje? Mheshimiwa Rais ametuonesha mfano, sasa na wao wachukue pale alipoishia twende mbele tutangaze nchi hii tufanikiwe. Nina imani tutafanikiwa sana na tutafika mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, tunaomba Wakala wa Misitu ibadilishwe iwe sasa ni Mamlaka ya Kusimamia Misitu yote Nchini. Misitu ni uhai, misitu ni maisha, misitu ni maisha yetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)