Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia jioni hii ya leo. Naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu. Naomba nianze na pongezi kubwa, niungane na wachangiaji wote waliompongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza utalii kwa kupitia Royal Tour. Pia niungane na wote ambao wamekuwa wakikuombea wewe kugombea Urais katika Mabunge na nina imani kabisa kwamba hiyo nafasi utakayoigombea tunakuja kuweka historia katika Bunge letu hili la Jamhuri ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wetu Mheshimiwa Mchengerwa ambaye kwa kweli kwa kipindi tu kifupi ameweza kuonesha kwamba Wizara hii inaanza kubadilika na inaleta maendeleo mazuri. Pia nimpongeze Naibu Waziri, wifi yangu ambaye pia amefanya kazi nzuri sana katika Wizara hii, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichangie kuhusu Mradi wa REGROW; kusema kweli kabisa Mradi REGROW kama walivyosema wenzetu wote waliochangia asubuhi na sasa hivi, ni mradi ambao tulikuwa tunategemea sasa utakuza utalii katika Mikoa yote ya Kusini lakini tunaona bado mradi huu unasuasua. Toka ulipoanza mwaka 2019 sasa hivi tuna miaka mitano, lakini bado tunaona hakuna chochote kinachowekezwa katika Mkoa wa Iringa, maana yake tuliambiwa kungejengwa kituo kikubwa cha maonesho ya utalii wa kimataifa katika Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Spika, pia walisema wangejenga ofisi ya kanda, lakini tunaona mpaka leo hii bado. Je, ni lini sasa vitu hivi vitajengwa, lakini pia nataka kujua je, wananchi wameandaliwa kiasi gani kuupokea huu mradi, kwa sababu tunategemea huu mradi sasa watajiajiri kwa kutumia utalii kama ilivyo kaskazini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuletea pesa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege. Tunategemea huu uwanja wa ndege pia utahamasisha sana utalii katika Mkoa wetu wa Iringa na Nyanda za Juu Kusini, lakini sasa tulikuwa tunaomba pamoja na huu ujenzi bado wanatakiwa wajenge ile barabara inayokwenda katika mbuga za Wanyama, Ruaha National Park kwa sababu kukiwepo tu na huu uwanja bila kujengwa ile barabara bado tutakuwa hatujafanya chochote.
Mheshimiwa Spika, tunategemea hata utalii wa ndani utaongezeka, lakini vilevile tunaomba pia katika lile lango pale Idodi kijengwe kituo kikubwa cha polisi kwa ajili ya usalama wa watalii kwa sababu tumeona kuna kontena tu ambapo sio vizuri. Pia wangesaidia hata ujangili ambao unatokea pale, kituo kile kitasaidia, wapewe na gari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wetu wa Iringa lipo eneo ambalo tunaomba Serikali ibadilishe matumizi ili gereza lile liondolewe eneo hilo litumike kama kivutio cha utalii. Eneo la Kihesa Mgagawa ambalo lipo katika Wilaya ya Kilolo, Mkoani kwetu Iringa. Hili eneo lilitumika na wapigania uhuru wa Kusini mwa Afrika, walilala pale akina Mandela, walikuwepo akina Sam Nujoma, walikuwepo Walter Sisulu, Thabo Mbeki. Hawa watu ni maarufu sana sasa kuweka gereza sidhani kama tunawatendea haki, na hiki ni kivutio ambacho kingeweza kuwavuta watu wote katika nchi zao waje waone wapigania uhuru walikuwa katika maeneo gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakumbuka Balozi aliishawahi kuja kutembelea lile eneo alisikitika sana kukuta kwamba kuna gereza. Nashauri ni bora hata kijengwe chuo cha utalii lakini pia hayo maeneo yatumike kwa utalii ili tuweze kutengeneza pesa. Pia itasaidia hata wananchi ambao wapo Kihesa Mgagao kujiajiri kwa kutumia utalii na barabara nyingi za pale zingetengenezwa. Hao watu ambao marais wao walikuwa wamekaa katika kile kituo wangekuwa wanakuja kutalii na ingesaidia kuongeza pato la utalii katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niungane na wale wote waliozungumzia kuhusiana na tatizo la ndovu. Katika Mkoa wetu wa Iringa ndovu pia wamekuwa wakileta uharibifu mkubwa. Yapo maeneo ambayo yameathirika na tembo na haya maeneo mengi ni yale ambayo yamezungukwa na Ruaha National Park. Katika Jimbo la Isimani kuna Kata ya Idodi, Mlowa, Pawaga, Unyinga na kadhalika. Pia katika Jimbo letu la Kilolo kuna Mahenge, Nyanzwa na Ruaha Mbuyuni na changamoto kubwa kabisa ya hawa watu ni fidia ambayo wanapewa fidia kidogo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana. Malizia sentensi kengele imeshagonga.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba, pengine sasa hawa watu ambao wapo katika haya maeneo waweze kupatiwa hata miradi midogo midogo kama ufugaji wa nyuki ili waweze kusaidia. Tumesikia kwamba nyuki huwa wanasaidia kufukuza tembo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.