Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuongea machache kuhusu bajeti iliyokuwa mbele yetu. Naomba niingie moja kwa moja kwenye hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wanategemea reli hususani mkoa wangu wa Katavi na Wilaya ya Mpanda. Alikuwepo Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Arfi, alikuwa anatetea sana reli ya kutoka Tabora - Mpanda. Mimi kila siku najiuliza Wabunge humu ndani wanazungumza kuhusu reli, lakini utekelezaji wake haupo. Mheshimiwa Arfi alivyokuwepo humu ndani alikuwa anazungumza kila siku, reli ya Mpanda - Tabora siyo salama. Mpaka leo reli ya Mpanda - Tabora ina pounds 40 na reli hiyo inabeba mizigo mingi, inailetea pesa nyingi Serikali na wananchi wa Mpanda wanategemea reli lakini mpaka leo reli ile wala haijashughulikiwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unasikia kuna sehemu reli zinang‟olewa zinapachikwa pound nyingine. Sasa najiuliza zile pound zinatoka zinakwenda wapi? Hivi karibuni walizing‟oa pound 60 Tura, sasa zile zilipelekwa wapi? Badala ya kutolewa pale na kupelekwa sehemu ambapo kuna pound ndogo ili reli yake iweze kuimarishawa lakini ndugu zangu hakuna kitu kama hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku wananchi wa Mpanda tunalalamika kuwa hatuna barabara, tunategemea reli na ndiyo maana Wabunge wengi wanasema RAHCO na TRL waunganishwe hili shirika lingine life kwa sababu hawana faida. Kuna pound zingine wameziacha pale makao makuu, pound 80 zimekaa hawajui kama wananchi wengine wanahitaji hizo pound, sasa wana maana gani? Hii RAHCO tunaomba Serikali sheria ilikuja Bungeni na ikaunganisha RAHCO na TRL, sasa sheria hiyo ije tena tutenganisha Shirika la RAHCO pamoja na TRL, sheria hiyo ije tena tupangue tuunganishe hili shirika liwe moja. Kwanza ukiangalia wanapewa hela nyingi halafu vitu vyake havieleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka mnasikia Godegode kuna matatizo, treni inaanzia Dodoma, ina maana Serikali mpaka leo haina ufumbuzi wa tatizo la pale Godegode? Kila siku Godegode treni imeishia Dodoma, Godegode treni imeishia Dar es Salaam, Godegode kuna mafuriko. Mnajua kabisa Godegode tatizo, kwa nini msichukue hatua za kurekebisha kwa sababu treni inayotoka Dar es Salaam – Mwanza – Kigoma - Mpanda inabeba abiria wengi sana na wananchi wengi maskini wanategemea reli, kwa nini hapo Godegode hapashughulikiwi, kila siku Godegode shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze kwanza Kaimu Mkurugenzi mpya, nashangaa kwa nini hawampi ukurugenzi, amethubutu safari hii, wananchi wamekwama njiani na treni amechukua chakula yeye kama yeye kuwapelekea wananchi. Tunaomba hawa Wakurugenzi ambao wanao uthubutu wapewe ukurugenzi. Kitu cha kushangaza, mimi naomba niseme, leo hii mashirika yote makubwa, bandari Mkurugenzi Kaimu, uwanja wa ndege Mkurugenzi Kaimu, TRL Mkurugenzi Kaimu, wapeni ukurugenzi kamili ili waweze kufanya kazi nzuri, wameweza kuthubutu hawa wapeni basi ukurugenzi waweze kufanya kazi vizuri. Mnavyowaacha na ukaimu wanafanya kazi kwa wasiwasi, wapeni mamlaka ili waweze kutekeleza yale mliyowakabidhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri akija hapa aniambie kabla ya standard gauge haijaanza maana haya ni majaliwa, Mbunge ametoka hapa kusema hayo ni majaliwa, tunaomba kujua reli ya kutoka Tabora - Mpanda mtatubadilishia lini zile pound 40 iwe angalau tu 60 ili ile reli iweze kuwa stable. Kwa sababu wananchi wa Mpanda wapo rehani huku barabara ikiziba huku treni wasiwasi. Kabla standard gauge haijaanza tunaomba uimarishaji wa reli ya kutoka Tabora - Mpanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaenda kwenye standard gauge na tumesema inafika mpaka Karema, Karema tunategemea bandari, lakini hatujaona mwamko wowote wa bandari Karema. Naomba hii mikakati ianze ili wale wananchi wa Karema waone kama na wenyewe wapo Tanzania kwa hii bandari inayopelekwa huko kwa ajili ya standard gauge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja darala la Kavuu; kuhusiana na barabara ya kutoka Inyonga – Majimoto, hii ni Wilaya mpya. Wananchi kutoka Mpimbwe huko Majimoto, Kibaoni, Usevya, Kasansa mpaka wafike makao makuu yao ya Wilaya Inyonga wanatembea siku mbili. Mtu anatoka Kasansa aje Mpanda alale kesho yake aondoke aende Inyonga, hiyo ni Wilaya au kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge wengine hapa wamesema kuhusu masuala ya barabara, hili daraja la Kavuu limechukua miaka saba. Hebu jamani mtuangalie watu wa mkoa wa Katavi, kila siku tunazungumza, tunaomba hili daraja liishe ili wananchi wa upande wa Kibaoni, Usevya, Kasansa waweze kufika kwenye makao makuu yao ya Wilaya siku moja. Tunaomba chonde Waziri akija hapo atuambie daraja la Kavuu litaisha lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza ile barabara ya kutoka Stalike - Mpanda na nikasema pale Mpanda kuna shimo, lile shimo linaisha lini? Ni kero kwa wananchi wa Mpanda, kila siku ajali zinatokea. Nilizungumza Januari lakini mpaka leo hakuna mkandarasi, hakuna kitu chochote, kila kitu kipo vilevile. Tunazungumza mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niunge mkono hoja.