Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na neema kwa kutujalia uzima. Nikupongeze wewe kwa usimamizi na uendeshaji mzuri wa Bunge letu tukufu. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake imara na dhamira yake ya dhati ya kuleta mabadiliko makubwa katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Mohammed Mchengerwa, Naibu wake Dada yangu, Mary Masanja na timu yao kwa kazi kubwa na nzuri wanaoiyafanya kwenye Wizara hii. Hii ni miongoni mwa Wizara muhimu kwenye uchumi na ukuaji wa uchumi wetu. Kama Taifa linaloendelea, tunahitaji kuwa na sekta imara ya utalii na ninyi ni watu sahihi kwa sababu mnaifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, sikuweza kupata nafasi ya kusimama kuchangia, lakini naomba nifikishe mawazo yangu kwa maandishi ili kusaidiana na kaka yangu Mchengerwa na dada yangu Mary kueleza mambo machache.
Mheshimiwa Spika, nianze na utalii; nipongeze jitihada kubwa zinazofanyika katika kuvutia watalii nchini. Kwa takwimu za Wizara ni kwamba zaidi ya watalii milioni 1.4 wametembelea hifadhi na mbuga zetu za wanyama. Haya ni mafanikio makubwa sana, lakini nadhani bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuongeza tija zaidi. Natambua yapo maeneo mengi ambayo kama tutaweka mkakati wa kuyafikia basi tunaweza kuwa na idadi kubwa zaidi ya tuliyonayo sasa. Kwa mfano, Mkoani kwangu Singida tuna ardhi nzuri na hali ya hewa rafiki kwa watalii, uwepo wa Ziwa Singidani lenye ndege adimu, lakini nyumba za utamaduni (tembe, vibuyu na vipeyu). Hili ni eneo ambalo linaweza kuongeza tija kwa watalii kwa kuwa sio kila mtalii anakuja nchini kuangalia wanyama, wengine hufuata kujifunza tamaduni, mbali na hilo Singida ni mkoa ambao uko katikati ya nchi hivyo kutangazia dunia kuwa ukiwa hapa ndio utakuwa katikati kabisa mwa Tanzania kila mtalii atatamani kuona Singida inafanana vipi.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa Singida kuna mlango wa mkondo wa bonde la ufa katika Kijiji cha Kinyamwenda, lakini bado hakuna jitihada za makusudi kulihifadhi eneo hilo ama kulitangaza kwa nguvu katika kuvutia utalii.
Kuhusu mapori ya akiba; mkoani kwangu kuna mapori ya akiba ya Mgori na Rungwa ambayo ni muhimu kwa ustawi wa Taifa letu. Mapori haya ni sifa na fahari kwa wananchi wa Singida. Lakini kuna mambo ambayo kama Serikali tunapaswa kuyapa kipaumbele. Wanawake wa Singida bado ni masikini hivyo, naomba uwepo wa mapori haya ukawe na baraka kwao. Wengi walikuwa wakihemea kuni kwenye maeneo ya jirani nje ya mapori, lakini kwa sasa wanakutana na vitendo viovu. Itoshe kusema basi ukatili huu dhidi ya wanawake ukomeshwe na Wizara ione umuhimu wa kusaidiana na jamii kwa kuwapa wanawake hawa majiko ya gesi ili wawe mabalozi wazuri wa kulinda mazingira ya ndani na nje ya mapori haya. Kwenye maeneo mengine yanayohusika na Hifadhi za Taifa kama Ngorongoro, mamlaka imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na jamii kupitia CSR, basi na huku ikawe hivyo.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulichangia ni kuomba Wizara ya Maliasili na Utalii itenganishwe kuwe na Wizara ya Utalii na kuwe na Wizara ya Maliasili na Mambo ya Kale. Kwa nini nasema hivyo Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikitumia muda mwingi kushughulikia migogoro ambayo inatokea kwenye mapori ya hifadhi badala ya kutumia muda huo kutafuta namna bora ya kutangaza vivutio vyetu na kuutangaza utalii wetu ambao una vivutio vingi ambavyo bado hatujavitangaza vizuri.
Mheshimiwa Spika, nawasilisha na naunga mkono hoja.