Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pili nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri wanazofanya katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni muhimu Mheshimiwa Waziri atambue kwamba jeshi letu la askari wa wanyama pori linahitaji kufanyiwa tathmini ya kina ili lifanye kazi kwa weledi mkubwa na kufuata misingi ya sheria.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za wananchi kuingia hifadhini, lakini baadhi ya askari hawa wamekuwa wakiua watu, wakijeruhi watu na wakipora mifugo ya watu kiholela. Kwa kweli mwananchi anayeishi karibu na hifadhi mimi naamini ndio wahifadhi wa kwanza kama mahusiano yatakuwa mazuri. Kwa sasa wananchi ni bora akutane na chui au simba ataweza kujiokoa kuliko kukutana na askari wa wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana, jeshi hili kwa jinsi linavyokiuka utawala wa sheria na kunyanyasa sana wananchi. Haikubaliki na haipendezi.
Mheshimiwa Spika, suala la pili ni wanyama kuvamia makazi ya watu hususani tembo. Hili tatizo linaendelea kukua kwa kasi sana na wanyama hawa wakivamia maeneo ya wananchi wanasababisha uharibifu mkubwa wa mazao, lakini wazee na watoto wanapoteza maisha na fidia kwa matukio haya kwanza hayaendani na hali iliyopo ya uhalisia kwa sasa, lakini pia hayatolewi kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu Wizara hii iweke mkakati madhubuti kuweza kushughulikia matatizo makubwa wanayokumbana nayo wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi hizi, wananchi hawakupenda kuzaliwa wala kuishi pembezoni mwa hifadhi, ila wamejikuta wamezaliwa karibu na hifadhi. Tunaomba muwasaidie, Mheshimiwa Waziri Mchengerwa nakuamini. rekebisha hii sekta, okoa wananchi walioteseka kwa muda mrefu, angalia kwa jicho la ziada jeshi hili, wananchi wa maeneo haya mioyo yao inavuja damu kwa mateso makali, rudisha mshikamano na umoja wa jeshi hili na wananchi. Nashauri watumie nguvu hizo kupambana na majangiri na sio wananchi ambao makosa yao yanarekebishika.
Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.