Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ningependa kuanza kwa kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Mary Masanja.

Mheshimiwa Spika, kiukweli Mheshimiwa Waziri Mchengerwa anafanya kazi nzuri kama vile Mayele alivyofanya kwa timu ya Dar es Salaam Young Africans. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumesikiliza hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge na wengi walikuwa wakizungumzia maeneo yenye migogoro ya ardhi kati ya hifadhi, vijiji na vitongoji mbalimbali hapa nchini. Vilevile…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Deo Ndejembi, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nampa tu taarifa Mheshimiwa Ndejembi kwamba kule Algeria aliyeleta kaushindi kale kagoli moja alikuwa ni Juma sio Mayele. Kwa hiyo, lile goli moja sio la Mayele ni la Juma.

SPIKA: Mheshimiwa Deo Ndejembi, unapokea taaria hiyo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, sipokei taarifa hiyo kwa sababu niliposema Mheshimiwa Mchengerwa ni kama Mayele ni kwa sababu Mayele ndio top scorer katika mashindano yale, kwa maana ndio nyota wa mchezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zilizungumzwa hoja za Kamati ile ya Mawaziri Nane. Katika maeneo ambapo timu ile ya Mawaziri Nane ilipopita kuna maeneo ambayo hakuna migogoro kabisa na tayari taarifa ile ilikuwa imekwishapelekwa katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa. sasa nitumie Bunge lako hili kuwataka Wakuu wa Mikoa wote waliopelekewa taarifa ya migogoro yote ambayo imekwishatatuliwa waweze kwenda site (field). Kwa sababu tumesikia taarifa hapa Wabunge wakisema wanabaki kule mikoani na hawapeleki taarifa hizi kwa wananchi. Basi, hawa Wakuu wa Mikoa waende kule field kwa ajili ya kupeleka taarifa ya utatuzi wa migogoro ile kwa wananchi kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo ningependa kulizungumzia jioni hii ya leo ni suala la uanzishaji wa maeneo mapya ya kiutawala. Hili ndilo limekuwa chanzo kikubwa cha migogoro. Kuna vitongoji na vijiji vinaanzishwa katika hifadhi. Sasa sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, safari hii tutahakikisha hatuanzishi maeneo mapya ya utawala bila consultation ya Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii lakini vile vile Wizara ya Ardhi, kuhakikisha kwamba maeneo yanayosajiliwa hayatokuja kuwa na migogoro siku za usoni. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya ahsante sana.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tumeona hiyo imekuwa ni changamoto sana. Kwa kusema hayo machache naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)