Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwanza nimpongeze CEO wa Simba kwa kuwa na roho ngumu kuwepo humu ndani leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye Kamati yetu, niongeze sauti kidogo kwenye eneo moja la utamaduni na nataka kuzungumia umuhimu wa utamaduni. Kwa kweli utamaduni ni dhana muhimu sana katika kufikia Tanzania ambayo tunaitaka kimaendeleo. Changamoto nyingi ambazo tunakumbana nazo tungeweza kuzitatua kama tukizingatia dhana hii ya utamaduni. Mara nyingi tukizungumzia utamaduni watu wanazungumzia habari za sanaa, maigizo, nyimbo ngoma za asili, hizo ni sehemu muhimu, lakini sio utamaduni pekee, ni sehemu muhimu ya utamaduni, lakini haiwezi kuwa pekee yake, lakini muhimu ni kwamba utamaduni kwa kweli ni mtindo wa maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo yale mawazo, desturi, tabia ya kijamii, mkusanyiko wake ndio tunapata utamaduni. Kwa mfano, tunapozungumzia ubunifu, ili tuweze kuwa na ubunifu maana yake tunahitaji kujenga utamaduni wa ubunifu, kwa mfano kuwa na tabia ya kujaribu na kutokuogopa kukosea. Kama tukisema kupambana na rushwa, sheria pekee yake haitoshi, lazima tujenge utamaduni wa kukataa kwa mfano shortcut na ujanja ujanja katika Maisha, ni utamaduni. Ukiwa na jamii ambayo utamaduni wake ni ujanja ujanja, shortcut hata utunge sheria ngumu namna gani, bado rushwa itakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo utamaduni ni jambo la msingi sana katika kukamilisha ambayo tunayataka. Hata sasa hivi Mheshimiwa Rais anapanua mambo ya demokrasia, maridhiano na yenyewe inahitaji kujenga utamaduni wa kidemokrasia, ikiwemo utamaduni wa kupingana kwa hoja bila kuchukiana, utamaduni wa kustahimiliana tunapotofautiana na utamaduni wa kuheshimu sheria na haki za watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo utamaduni wa kuheshimu sheria ni muhimu sana, unaweza ukawa na sheria nzuri, lakini kama hamna utamaduni huo itakuwa ni changamoto. Kwa sasa hivi lazima tupongeze kwamba nchi yetu ina utamaduni mzuri kwenye michezo. Tuna timu mbili kubwa Yanga na Simba tunashindana, tunataniana, tunacheka, hatugombani, jambo jema ni utamaduni mzuri sana. Hata kama wenzetu ndio hivyo tena lakini tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kutokana na umuhimu wa utamaduni nchi yetu hii tangu tulipoanza, hotuba ya kwanza ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Tanganyika kama Republic katika Bunge Mkutano wa Tano wa Bunge, tarehe 10 Desemba, Mwalimu Nyerere alitangaza kufanya mabadiliko makubwa mawili katika Serikali yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, badiliko moja ambalo alifanya aliamua kuanzisha Wizara Maalum ambayo wakati huo aliita Ministry of National Culture and Youth, baadaye wakatafsiri wengine wakaita Wizara ya Mila za Taifa na Uongozi wa Vijana. Kwa hiyo, ukienda Waziri wa kwanza wa Wizara hii alikuwa anaitwa Bwana Kundya, Mbunge wa Singida alikuwa anaitwa Waziri. Mheshimiwa Sima, Mbunge wako wa kwanza alikuwa Kundya huyo na alikuwa Waziri wa Mila za Taifa na Uongozi wa Vijana. Kwa hiyo, Mwalimu aliamua kuanzisha Wizara Maalum, baadaye wakafuata wengine akina Chedya na kadhalika, lakini hatimaye akaja Meja Jenerali Sarakikya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo kwa muda mrefu tukawa na hii Wizara na katika historia ya nchi yetu ni mara mbili tu tumekuwa na Wizara dedicated kwa ajili ya utamaduni na sanaa. Mara ya kwanza ni hiyo ilikuwa tarehe 10 Desemba, 1962, mara ya pili ni mwaka jana tarehe 8 Januari, 2022. Pale ambapo Mheshimiwa Rais aliamua kuunda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kwa hiyo, ni uamuzi ambao ni mkubwa na unaakisi malengo yale ambayo Mwalimu Nyerere aliyatanganza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale aliposema Makamu Mwenyekiti sisi Kamati hatuwezi kuelewa, katika kipindi ambacho Mheshimiwa Rais ameamua kufuata nyayo za Baba wa Taifa 1962 tukiwa watu milioni 10, inawezekanaje tumeunda Wizara Maalum watu milioni 61 halafu unapunguza bajeti ya maendeleo, hili haliwezi kueleweka. Kwa hiyo tuombe sana Serikali ilione jambo hili kwamba ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda niende katika jambo la pili, of course siwezi kumaliza hotuba yangu bila kuipongeza Timu ya Yanga kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Wameijengea heshima nchi, dunia imeona, nchi imeona, lakini Mheshimiwa Rais ameona jambo kubwa sana hili. Kwa hiyo, tunawapongeza na nadhani mambo mazuri huwa yanaigwa, nishauri kwa mfano, pale Dar es Salaam tuna Mkuu wa Mkoa pale, Albert Chalamila, mahiri sana, machachari, pengine angeweza kuamua wale ambao wamefika robo fainali awaandalie lunch ya Mkuu wa Mkoa pale. Kwa hiyo, mtu akiingia robo fainali Mkuu wa Mkoa anaandaa lunch, akiingia fainali dinner kwa Mheshimiwa Rais, tatizo liko wapi? Kwa hivyo jambo hili watu wasiwe na nani na nini, inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, pale Ubungo tuna mabingwa 30 wa ndondi, 30 Jimbo la Ubungo pekee yake kwenye mambo ya ngumi. Nataka niwapongeze vijana hawa na kwa niaba yao niwataje wachache tu kwa sababu ya muda. Nimtaje Binti yetu Amina Mohamedi, hongera sana; Mariam Macho, hongera sana; Iddi Pialali, hongera sana; Hassan Ndoga, hongera sana, Mfaume Mfaume, hongera sana kwa kazi kubwa ambayo ameifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wasanii wote kutoka Jimbo la Ubungo wanamuziki ambao walishinda tuzo za muziki nimpongeze sana kupitia kwake Ndugu yetu Dulla Makabila ambaye aliibuka kuwa msanii bora wa kiume wa singeli, hongera sana Dulla Makabila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni ombi kwa Mheshimiwa Waziri, Dar es Salaam na hasa Wilaya ya Ubungo tuna mashindano ya Ndondo Cup. Tunayo maombi mawili, ombi la kwanza atusaidie sana Mheshimiwa Waziri, vile Viwanja wa Kinesi na TP ni viwanja muhimu ambavyo vinatumika kwa ajili ya mashindano ya Ndondo Cup, lakini havijakaa vizuri. Tumwombe sana, tena sasa Mwenyekiti anaaongea, amwangalie Mwenyekiti wake aweke kiwanja pale, jambo jema kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, suala la Ndondo Cup tunaomba liingie katika mfumo rasmi wa kiligi litambuliwe. Kwa sababu linaibua vipaji vya vijana wengi sana, otherwise Mheshimiwa Waziri sisi kama Kamati kama alivyosema mwenzangu tunampongeza kwa kazi nzuri, ana hamasa nzuri, juzi amewatia vijana wetu hamasa nzuri sana pale Algeria, ile tumeshinda lakini tumeshindwa kikanuni. Kimchezo tulishinda, lakini kikanuni tukashindwa, lakini Waziri amechangia sana kwa hamasa zako. Tunashukuru kwa hamasa kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa, vijana wanawaka moto na tunaamini mwaka huu timu zetu zaidi ya mbili zitaenda vizuri katika Mashindano ya Kombe la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)