Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Shabani Hamisi Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa napenda kuipongeza Wizara hii ya Michezo, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kile alichokifanya kwenye hii Wizara kutuletea Mawaziri majembe. Kikubwa ambacho naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Waziri kutoka Tanga, Ndugu yangu Hamis Mwinjuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anachaguliwa nakumbuka nilikuwa Marekani, lakini Waziri alikuwa na kidevu cheusi kabisa hakina mvi hata moja, alikuwa anakicheka cha kwangu, Mheshimiwa Waziri leo hii ana kidevu cheupe kwa sababu ya mzigo mzito wa Wizara aliyopewa. Wizara kubwa, Wizara ambayo inachangia furaha ya nchi nzima, Wizara ambayo Bunge lako lina furaha kwa sababu ya hii Wizara, ila Wizara hii inatia aibu, tunakaa hapa mbele Wizara ina bajeti ndogo kuliko Wizara yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ana mapenzi ya dhati na hii Wizara, tuseme wazi ameingia madarakani Mheshimiwa Rais akaelekeza watu wa michezo ya kubashiri wapeleke pesa asilimia tano inayopatikana. Yote hayo ni kupambana na hii Wizara ili ikapate pesa. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ambao tunasimamia hii Wizara, ni aibu kusema mengi, Wizara haina pesa hii, tunamtia mvi ndugu yangu Mwana FA na dada yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niongee kidogo, leo hii hawa Wizara imeletewa Fungu bilioni 900 Mwezi wa Pili, mwaka huu. Ukimuuliza Waziri hapo hajui hiyo miiloni 900 ya nini, tuseme ukweli kwa heshima niliyonayo…

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, … kwako na …

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hamisi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mgaya.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nampongeza anachangia vizuri Mheshimiwa Taletale, lakini nataka tu aweke rekodi vizuri sio bilioni 900 ni milioni 900, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Hamisi taarifa unaipokea?

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea na nimezoea kuzungumza kuhusu ma-b kumbe kuna ma-mi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inapelekewa milioni 900 ya kitu ambacho wao hawajui, leo dada yangu Mheshimiwa Waziri, leo naondoka na shilingi yake, ikiwezekana akamtafute Waziri wa Fedha, maana yake hapo mbele hayupo. Tujue je, hiyo milioni 900 anayopewa, inawezekana hata Mheshimiwa Rais ameelekeza hii five percent iende kwao, lakini pia hajui hiyo milioni 900 waliyopewa ya mchanganuo gani. Kwa hiyo, niombe tunataka kujua hizo pesa zinazokuja kwenye Wizara yetu ya Michezo zinakuja kwa utaratibu upi, kwa namba ipi? Maana ukisema leo hii Wizara imeletewa milioni 900 Mwezi wa Pili, wakati watu wa michezo ya kubashiri kila mwezi wanatoa pesa, kwa hiyo, wananyimwa haki yao. Nani wa kusimamia haki yao kama sio sisi kama Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kingine hapa, maendeleo ya michezo tuangalie wenzetu kama Senegal, Senegal ni nchi ambayo ina wananchi milioni 16, Tanzania tuko zaidi ya milioni 60, Senegal ukitazama mashindano makubwa ya ndani ya Afrika yote Senegal wamechukua. Sisi tupo tu, tunahangaika kubebesha mzigo kuipa TFF. Nimpongeze sana Ndugu yangu Karia na timu yake, tunahangaika kubebesha mzigo kumpa Mama Samia. Jamani juzi nimesema mimi ni kipenzi cha yule mama, wanamtia presha mama yangu. Watafuteni utaratibu, watafute njia ya kuangalia jinsi gani hii Wizara itapata pesa, tuwe wawazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wakae, hii ni michezo ya kubashiri, waibebe kama ilivyo waipeleke Wizara ya Michezo, wanashindwa nini? Leo hii tunakuja kuzungumzia michezo hapa, kuna Wizara ina zaidi ya trilioni tatu, Wizara ya Michezo ina bilioni 35, ni udhalilishaji huo, ni aibu kwa Wizara na ni aibu kwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia. Kama tunataka kumsaidia Rais positively, lazima tuangalie tunakwama wapi? Lazima tuangalie tuna dhamira gani, dhamira ya kutaka kumsaidia Rais, hii michezo ya kubashiri…

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu, Nchi kama Uingereza labda tuseme ni nchi kubwa wao wana michezo ya kubashiri ya nchi, wanasema Gaming Board ya Nchi, lakini ile michezo ya kubashiri inapeleka 50 percent kwenye Wizara ya Michezo, tunaona inaendelea. Basi nizungumzie nchi ya jirani yetu hapo Kenya, utaratibu wao wamesema mpaka 2030 watatoa bilioni 11 kwenye Wizara ya Michezo, hiyo ni kwa mwezi, lakini tazama sisi tuna bilioni 35, humo kuna mshahara wa Mwana FA sijui kuna mshahara wa nani, khaa! Kuna vitu vingine vinaumiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna dhamira ya kuisadia hii Wizara ambayo nimeona jana Mheshimiwa Rais amesimama anatamba kwamba ana dhamira ya dhati ya kuisaidia Wizara ya Michezo, lakini leo hii sisi tunashindwa kukaa, kujadili jinsi gani Wizara ya Michezo itasonga mbele. Tuongee wazi, leo hii mimi na ujana wangu na kutembea tembea kwenye baadhi ya nchi, Wizara za Michezo zinatazamwa, lakini leo hii kwenye Bunge lako Tukufu tuongee ukweli ndio Wizara ambayo tumeipuuza, hatutaki kuisika, inadhalilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme neno langu la mwisho, nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri kama sijaelezewa ile asilimia tano aliyoelekeza Mheshimiwa Rais inakuja kiasi gani mpaka amepata milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)