Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri lakini cha pili nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa jinsi alivyoweka mguu wake asilimia 100 kwenye suala la michezo Tanzania, nina kila sababu ya kujivunia kama mdau wa michezo nchini kuona kwamba Mheshimiwa Rais ameweka asilimia 100 mguu wake kuona ana-support michezo nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nimpongeze sana Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo na kuna mambo nitakayomshauri hapa, lakini nimpongeze pia ndugu yetu Mapana kwenye BASATA. Naenda haraka kwa sababu dakika ni chache na hii inaonyesha kwamba hii Wizara pia kuna changamoto, huu muda ilitakiwa tuchangie mambo mengi sana kwa ajili ya ku-support Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Mapana wakati kuna siku mimi nilisimama hapa nilisema, “BASATA imegeuka kuwa mahakama ya wasanii” lakini Dkt. Mapana ameibadilisha BASATA sasa imekuwa ni sehemu ambayo wasanii wanapata haki zao. Kwa hiyo ninampongeza sana Mtendaji Mkuu wa BASATA kwa kile ambacho anakifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina hoja zangu. Kabla ya hapo pia niipongeze Yanga kwa yale ambayo wameyapata kule Algeria na ni wamefanya kitu kizuri na kwa sababu ya Yanga pia hata Simba tumeweza kuhudhuria jana kwenye mwaliko wa Mheshimiwa Rais na wanamichezo wengine, kwa hiyo, tunawapongeza. Pia niipongeze timu ambayo pia ni sehemu ya uongozi timu ya Singida Big Stars kwa kuingia kwenye michuano ya Shirikisho, mwakani Big Stars Singida tunaingia kwenye Shirikisho Barani Afrika na tuwahakikishie Watanzania tutafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya kwanza iko kwenye michezo kwenye viwanja. Mheshimiwa Waziri mwaka jana tulitenga bajeti hapa ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa viwanja. Hakuna sehemu inasomeka kwenye bajeti yenu suala la shilingi bilioni 10 popote pale halisomeki. Sasa mimi niwape tu ushauri kwa bajeti ya shilingi bilioni 35 hii hamuwezi kufanya kitu chochote, lazima mtoke out of the box kwenye kutafuta ni namna gani mtasaidia ujenzi wa viwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fanyeni kama Zambia niliwashauri, jambo la kwanza, tunajenga mradi wa SGR, mradi wa SGR Mkandarasi yule ilitakiwa CSR yake tumpe kazi ya kujenga uwanja mmoja, angeweza kuwasaidia na mkaondokana na changamoto hii. Tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, CSR ya ujenzi wa Mwalimu Nyerere mngempa kazi ajenge bwawa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zambia walifanya hivyo kwenye coper belt wamejenga viwanja vyao kule kwamba CSR inayotokana na migodi tunajenga viwanja. Sisi kwa shilingi bilioni 35 hapa tutaendelea kupigana chenga, kwa sababu gani Mheshimiwa Waziri? Shilingi bilioni 35 itaenda kujenga nini kwenye viwanja vyetu vya nchi yetu? Nikuombe tokeni nje, tafuteni watu, tafuteni wadau waweze kuwa-support kujenga viwanja. Tafuteni fedha kwenye makampuni haya. Mgodi kama wa Barrick mwaka huu wametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mashule, Makete nimepokea karibu shilingi milioni 540. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barrick wapeni task wajenge angalau uwanja mmoja. Nendeni pale GGM, pale Geita Gold wajenge uwanja mmoja. Mimi nawapa mbinu tu za kuweza kupata fedha ili muweze kusaidia kujenga viwanja nchi hii, tofauti na hapo ni danadana tutamaliza miaka mitano kwenye Ilani tutakuwa hatujatekeleza kitu na mpango wa Mheshimiwa Rais ku-support michezo nchini utakuwa haujafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ni kwenye suala la reforms. Kuna sheria ambazo zipo ndani ya TFF na taratibu. Moja kati ya jambo ambalo ningetamani TFF na Watanzania ni suala la kwenye makato kwenye mapato ya viwanja kwa wachezaji wetu. Hizi timu zinatumia gharama kubwa sana kwenye uendeshaji. Sasa inapotokea timu imeenda kwenye mechi imecheza, yale makato ya mapato kwa maana ya gate fee ni lazima Serikali ione, lazima TFF waone jinsi gani ya kuzi-support timu zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea tu mfano kwenye ule mchezo ambao ulipita mchezo wa Simba Sports Club dhidi ya Yanga ambapo kwenye mchezo wa Simba Sports Club dhidi ya Yanga zilipatikana jumla ya shilingi 410,000,000 lakini Simba wameenda kuambulia shilingi 183,000,000. Angalia mgawanyo pale, kuna VAT, kuna gharama ya tiketi shilingi milioni 22, kuna uwanja shilingi milioni 47, kuna FA (Chama cha Mkoa) shilingi milioni 18, kuna Bodi ya Ligi shilingi milioni 25, kuna TFF shilingi milioni 12. Saidieni hivi vilabu. Mheshimiwa Waziri nikikwambia bajeti ya kuifanya klabu ikae camp. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikikaa camp Simba Sports Club kwenye mchezo wa Yanga they are spending zaidi ya shilingi milioni 100. Sasa leo unaenda kupata zaidi ya shilingi milioni 410 kwenye mchezo wao wanaenda kupata shilingi milioni 138 tu, zaidi ya shilingi milioni 300 zimeenda kwenye mifuko ya watu wengine. Mheshimiwa Waziri mimi nimekuwepo kwenye mpira, ukienda hawa watu ambao wanapatiwa hizi fedha wana udhamini kutoka Azam. Azam anavyotoa udhamini kuna fedha inaenda Bodi ya Ligi. NBC anavyotoa udhamini kuna fedha zinaenda Bodi ya Ligi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wana faini kwa wachezaji kila siku unasikia sijui Morrison kafungiwa analipa shilingi milioni tatu, sijui ukisikia Simba imefanya nini, imelipa shilingi milioni tano, ukisikia sijui Yanga imefanya jambo gani inalipa shilingi milioni 10. Hawa watu they accumulating a lot of money. Hizi fedha zingine waweze kuvisaidia vilabu vyetu vikaendesha kwenye mambo yao ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri ambalo nataka kukushauri, kwanza kukupongeza ni jinsi gani ambavyo sekta ya uigizaji Tanzania inafanya vizuri, ninakuomba Mheshimiwa Waziri BASATA, Bodi ya Filamu Tanzania wanafanya jambo zuri sana, hapa nitoe complement yangu kwa huyu mtu anaitwa Leah Mwendamseka (Lamata) amefanya jambo moja kwenye uigizaji, anatengeneza series, amefanya jambo zuri sana sasa Tanzania inaenda kutambulika angalau kwenye uzalishaji wa series umeenda kwenye jambo zuri, anazalisha vizuri. Huyu mtu tumpongeze na tuone hata wadau wengine ambao wanafanya hii kazi ya uzalishaji kwenye Bongo Movie na kwenye uigizaji tuweze jinsi ya kuwa-support. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua hawa waigizaji wakienda sehemu kuigiza, vibali vya kupata vya kuigizia maeneo fulani ya Serikali inakuwa ni ngumu kupata. Tuweze kutengeneza mazingira ambayo inaweza kuwasaidia ili filamu zetu Tanzania ziweze kuzalishwa katika ubora. Kwa hiyo, ninatoa complement kwa Lamata kwa jinsi alivyoifanya Jua Kali na kampuni inavyofanya vizuri na kwenye nyanja za Kimataifa nadhani katika uzalishaji ameenda vizuri sana. Kwa hiyo, nipende kupongeza kwenye hilo na niombe Mheshimiwa Waziri waigizaji nchini waweze kuangaliwa kwa jicho la karibu ili mazingira yao ya kufanya kazi yawe katika ubora, hasa maeneo ya kuigizia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri ni jambo la shule. Mlisema mnajenga shule za michezo nchini na tunaye Leonard Tenga hapa yuko hapo juu, anajua kabisa tulikuwa na Makongo ikazalisha wachezaji wengi ambao wamekuja kulisaidia Taifa letu. Leo hii alipita hapa Waziri Bashungwa huyo hapo nyuma, alituahidi kwamba mnajenga shule, akapita Waziri Mchengerwa akaahidi anajenga shule, unakuja wewe anaahidi mnajenga shule, hamna shule iliyojengwa hata moja, shule za michezo nchini ambazo zinaenda kuzalisha specific kwa ajili ya kuzalisha soka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Makongo ilizalisha wachezaji wengi kwenye Taifa letu. Fanyeni mchakato wa kujenga shule, hata mkianza na mbili za mfano, sisi wadau wa michezo watajisikia amani kuona kwamba mnaenda kulisaidia Taifa letu. Kwa hiyo ni vema….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kw Amuda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana muda wetu umeisha.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kengele ya pili?

MWENYEKITI: Ee ndiyo, unga mkono hoja muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niseme naunga mkono hoja lakini nilikuwa na jambo kubwa sana kuhusu mfuko wa maendeleo. Wanakusanya fedha lakini hatujui ni kiasi gani kimekusanywa hadi leo. (Makofi)

MWENYEKITI: Utaleta kwa maandishi.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)