Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa sababu ya muda naomba niende moja kwa moja kwenye hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nataka nirejee watu wawili muhimu sana. Kwanza ni Mwalimu wangu marehemu Mheshimiwa Dkt. Agustino Mahiga pale National Defense College pia na American Political Scientist Joseph Nye. Hawa watu wawili walizungumza jambo moja kubwa sana. Ukitaka nchi iwe na usalama na amani lazima mambo mawili makuu uweze kuyasimamia. Moja ni hard power lakini jingine soft power. Walimaanisha nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hard power walimaanisha Majeshi lakini kwenye soft power walikuwa wanamaanisha cultural values (tuna maanisha sanaa, utamaduni na michezo) kila kitu. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha dhahiri kwamba sasa anahitaji ku-promote eneo hili la soft power (nguvu laini) eneo la michezo na sisi tumejionea tangu mashindano yameanza Mheshimiwa Rais ameonesha uwezo mkubwa sana, lakini mpaka juzi anaamua ndege isafiri kwenda Algeria zaidi ya shilingi milioni 200 zimegharamia ndege ile kwenda, ameonesha dhahiri kwamba anahitaji eneo hili la soft power, eneo hili ambalo linagusa jamii kwa ukubwa wake liweze kuwa promoted. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ninayoiona hapa nikirudi kwenye bajeti, wamesema Kamati na wachangiaji wengine, inasikitisha sana; fedha za maendeleo ambazo ndiyo tunatarajia Wizara hii ifanye vizuri, mwaka 2022 tulitenga Shilingi bilioni 15, mwaka huu tunatenga Shilingi bilioni 11. Sababu gani ya msingi iliyotumika kupunguza fedha hizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nataka niwaombe sana wenzetu wa Wizara ya Fedha, hili jambo walifanyie kazi. Haiwezekani Wizara hii ambayo tunaitegemea iweze kutengeneza mazingira mazuri kwa Watanzania. Ameeleza vizuri hapo Mheshimiwa Anatropia kwamba sasa inatoa ajira na inafanya kila jambo, lakini hebu mathalani tufanye tu kwamba hakuna sanaa, hakuna michezo, hakuna maigizo hakuna chochote nchini. Nchi haiwezi kutawalika. Ndiyo maana tunazungumza kwamba Wizara hii ndiyo soft power ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wewe ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na ndio Mwenyekiti wa leo kwenye kiti hiki. Unayo mamlaka ya kuagiza kwenda kufanya supplementary budget ili turudi hapa. Maana yake kwenye bajeti kuu fedha iwe imeongezwa. Hatuwezi tukawa tunazungumza habari hii ambayo siyo nzuri kutafsirika kwa Watanzania kwamba Wizara muhimu kama hii imepunguziwa bajeti. Tutashindwa kutoa maelezo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili muhimu sana. Tumezungumza hapa kuhusu sport betting. Tumetunga sheria wenyewe, inatengwa 5% kwenye makusanyo hayo ya michezo ya kubashiri. 5% inakwenda Wizarani kwa maana ya Baraza la Michezo Tanzania. Hii 5% haiendi kwa wakati. Siyo tu kwenda kwa wakati, haijulikani. Hata kiwango kile ambacho kinapatikana, kinachopelekwa kule hakijulikani. Maana yake nini? Hapa tunaleta changamoto. Nami nitakwenda baadaye kushauri vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa tunaowapa 5%, hata kuandaa mpango kazi wa hiyo 5% wanashindwa, kwa sababu hawana uhakika na hiyo fedha inakuja wakati gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri, nawaomba TCRA tuweke jambo hili wazi, kwa nini lijifiche? TCRA watoe link kwa Baraza la Michezo Tanzania wawe wanaona kila kinachoingia ili wajue 5% yao ni kiasi gani, waweze kupanga mpango ambao sisi Wabunge tunaweza kujadili, kwa nini tumeshindwa kutekeleza hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michezo hii ya kubahatisha, jambo moja muhimu sana ni suala la maadili. Hayuko mtu huku chini; sasa hivi kila nyumba mtu anaweza kwenda kuweka mashine, watu wakaamua kucheza kwenye nyumba za watu, watoto wadogo, kila mtu. Nani ana jukumu la kusimamia maadili kwenye eneo hili la michezo ya kubahatisha? Tunatengeneza Taifa la namna gani hapo kesho? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ni muhimu sana kwenye eneo la maadili. Fedha hii 5% ipelekwe kule ili pia waweke mpango wao wa kuweza kuhakikisha kwamba suala la maadili tuwashirikishe na Wizara ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie uwanja wa Taifa. Mheshimiwa Waziri aliunda Tume, nami nataka nimwambie, Tume haikuwa na haja. Jambo lile liko wazi, hatuitaji kuunda Tume. Tume inaenda kufanya compromise. Watatuletea majibu ambayo tunayajua. Tangu Uwanja wa Mkapa umejengwa haujawahi kufanyiwa marekebisho, haujawahi kufanyiwa chochote na hatujawahi kutengeneza bajeti hapa kuweka fedha ambayo inaenda kuhakikisha kwamba tunakarabati Uwanja wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wetu tumeujenga zaidi ya miaka 15 lakini hakuna ukarabati, wala huhitaji mechanism hapa. Suala la umeme kukatika litegemee, suala la maji kutokuwepo litegemee, na wala hatuwezi kuja kuwabana Mawaziri hapa kwa sababu hatujatenga bajeti. Ninatachotaka kushauri hapo, jambo la kwanza, wala hatuhitaji Tume hapa. Serikali itenge bajeti kila mwaka kwa ajili ya Uwanja wa Benjamini Mkapa na ndiyo uwanja tunaoutegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunao wadau ambao wamewekeza kwenye michezo. Wako AZAM, NBC, AIRTEL na wengine wote. Wadau hao wote waitwe washirikishwe. Tunapata aibu kwa pamoja, nao wameweka mabango yao pale. Kwa sababu umeme ukizimika, mabango hayawezi kuwaka. Hao pia waitwe washirikishwe ili kuhakikisha kwamba uwanja huu haturudi huku tulikotoka. Hii adha kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa nilichangie muhimu sana, Serikali inatenga maeneo. Huko kwenye Mipango Miji, Halmashauri zetu zinatenga maeneo ya viwanja. Sasa maeneo ya viwanja yanaitwa maeneo wazi. Viwanja vinaitwa maeneo ya wazi. Hapa nataka wakitenga viwanja washirikishe wenzetu wa TFF, ndio wanaojua standard ya viwanja inatakiwa iweje? Nawapongeza sana TFF, wamekuwa na mstari wa mbele kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie eneo moja muhimu sana. Nawashukuru sana Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu, nawapongeza sana Dar Young African, wameleta heshima kwenye nchi hii. Nawapongeza TFF, nawapongeza sana kwa kazi kubwa waliyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)