Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nami niendelee na kuwapongeza Wizara Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuendeleza sekta zote zinazohusiana na Wizara yao. Pia napenda kukushukuru Mheshimiwa Waziri, kwani kwetu kule Zanzibar anajitahidi sana kuweka ushirikiano wa pamoja na kutoa msukumo katika mazingira yote ya utamaduni na kuhakikisha yanakwenda sambamba na Tanzania Bara. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, aendelee na juhudi zake hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda inabidi moja kwa moja nichague moja la kusema hapa. Najielekeza kwenye lugha ya Kiswahili. Lugha ya Kiswali ni ajira, lugha ya Kiswahili ni rasilimali na pia lugha ya Kiswahili inaitangaza Tanzania katika Sekta ya Utalii. Kuna utalii sasa unafanyika kupitia lugha ya Kiswahili, kwamba watalii wanakuja kusikia hiyo lugha ya Kiswahili, kuona nchi yenyewe ambayo imeanzisha Kiswahili na kuona utamaduni wa Mswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye hiyo hiyo lugha ya Kiswahili; ili kukamata soko la ajira ni lazima Wizara hii iongezewe fungu la fedha katika kuwaandaa vijana wetu kwa soko la ajira la ukalimani na ualimu, kwa maana ya kwamba tuwaongezee uwezo na idadi ya lugha ambazo ataweza kwenda kutafsiri na kufanya ukalimani, isiwe tu Kiswahili na Kiingereza, bali na lugha nyingine za kigeni wawe wanazimudu ili kudhibiti hili soko la ajira lisije likachukuliwa na mataifa mengine ambao sasa hivi wao ndio wanajifunza Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiswahili chetu kinajulikana Afrika, kinajulikana duniani sasa hivi na kinaipaisha Tanzania, lakini tukiimarishe Kiswahili chetu kiwe imara. Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha mbalimbali duniani; Kiarabu, Kiingereza, Kiajemi na lugha nyingine. Kwa maana hiyo, Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha. Neno lenyewe Swahili, linatokana na neno la Kiarabu, kwamba ni pwani, pwani. Pia Waturuki wanatumia neno hilo hilo swahil kwa maana ya pwani. Kwa hiyo, ni lugha ya Pwani na utamaduni wa pwani ukaenea duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2022 nilisema na leo narudia tena kwa uchache tu. Kuna maneno tunayatumia ambayo yameungana; Kiswahili, Kiarabu, Kiingereza, mfano taabani, kanuni, madrasa, dhuluma, Askari, barafu; haya ni Kihindi, Kiarabu na Kiswahili tunayatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikwambie sasa, bendera na safari ni neno la Kihispania; vurumai ni neno la Kigiriki, tunalitumia; pashiani, reshani Kijerumani kuna hela, kuna zahanati. Hapa natoa mfano mdogo tu tuone. Hoja yangu ni kwamba tunapotunga haya maneno ya Kiswahili tutumie maneno rahisi na mepesi kama lugha yenyewe, isiwe sasa hivi Kiswahili ni kigumu. Kimekuwa kigumu sana na hapo wanapokaa kuyatunga haya maneno, ushirikishwaji unakuwaje kwa pande zote mbili; Baraza la Sanaa, Baraza la Kiswahili la Taifa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKITA na BAKIZA)? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo hiki sasa hivi kimemaliza muda, naishauri Serikali itapokiunda, iangalie upya muundo wake kama unakidhi vigezo vya sasa na kuitangaza Kiswahili duniani? Kama haukidhi, tufanye marekebisho, tutafute Waswahili wabobezi ambao wapo, waingie kwenye hizi sekta waweke sawa Kiswahili chetu ili kiendane na hadhi na ubora unaotakiwa, kuliko kujaza tu maneno hata hayaeleweki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatoa mfano kwamba Kiswahili ni mchanganyiko wa maneno. Lugha nyingi zinategemeana kwenye maneno mbalimbali yenyewe huko kwenye Kijerumani, Kifaransa, Kigiriki na Kitaliano, yanaingiliana siyo kwenye lugha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, nataka nitoe mfano mdogo kwa watu ambao wamekineemesha Kiswahili, wamekitangaza Kiswahili duniani na kukistawisha. Nina wengi, lakini kwa uchache tu, napenda kumtaja Prof. Mohamed na Dkt. Abdallah, hawa walikuwa walimu katika Vyuo Vikuu vya Uganda na Kenya ambao wanafunzi wao sasa wameshalikamata soko la Ghana na Nigeria, wanasomesha huko Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya utangazaji kuna watu wamekichangia Kiswahili tangu miaka ya 50 na 60 nchi mbalimbali. Mfano, Watangazaji kuanzia miaka ya 1950, kuna Bwana Ahmed Rashid Ally, Sauti ya Afrika, Sauti ya Ukombozi, Cairo; kuna Maimuna Fassy, sauti ya Marekani; Abdulrahim Kaktan, Radio Deutsche Welle; Abdala Mbamba, sauti ya America; Ahmed Rajab BBC na wengine Radio Moscow Abdul Wahidah Hassan Shehe. Tukiendelea, Radio Japan, Rahman Mohamed Dahman, ambaye alitokea Radio Deutsche Welle; Umul Kheir; hao ni wengi na baadhi tu akiwemo Bw. Ramadhani Ally ambaye alitangaza Idhaa ya Kiswahili Czechoslovakia Idhaa ya Prague, pia alitangaza Berlin na baadaye Radio Deutsche Welle, mpaka akastaafu. Mwingine Radio Beijing, Miraji Mpatani, Haroub Othman; tukiendelea, kuna na wengi Radio China. Naomba tuwaenzi, tuwatambue. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, mwisho niseme hivi, neno la Tanzania lina nuru na linapaa duniani. Aliyetunga jina la Tanzania alikuwa ni mwanafunzi kwa wakati huo, ametumia kipaji chake na uwezo wake. Kama ingewapendeza, miaka 60 ya Muungano, Jamhuri ya Tanzania akaletwa huyu mtu tukamwona na Taifa likamtambua kutokana na jambo zuri aliyotufanyia Taifa letu, Tanzania inapaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)