Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi hii, na mimi naomba moja kwa moja nianze kwa kuunga mkono hotuba hii na niwashauri Waheshimiwa Wabunge tuipitishe hii bajeti bila ya ukakasi lakini bajeti hii lazima iboreshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kwenda katika mchango wangu rasmi ningempongeza kwanza Mheshimiwa Rais ana maono mazuri sana, ana ndoto nzuri sana ametueleza jana wakati tulivyokuwa katika hafla ile ya kuipongeza klabu kubwa kabisa yenye historia kubwa katika nchi hii klabu ya Yanga ambayo imeshakuwa mabingwa sasa mara 29 wanakwenda kutawazwa leo jioni hii kuwa mabingwa wa 29 katika Premier League. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amejipambanua kutaka masuala ya michezo utamaduni, yaweze kupewa kipaumbele stahiki na ameona kwa kupitia sports diplomacy kwamba kumbe Tanzania inaweza ikapata recognition ikatambuliwa nchi za nje kupitia michezo na nimefurahi sana tuliupokuwa kule Algiers Mheshimiwa Waziri alipata nafasi ya kuweza kukutana na wenzake wa pale Algiers, Algeria Mawaziri wenzake kuizungumzia habari ya Tanzania na michezo. Vilevile nimeona seriousness ya Serikali katika kupeleka mawaziri wawili, Waziri wa Serikali ya Muungano lakini Waziri Mwita kutoka Zanzibar. Hii inaonesha kabisa dhamira ya Mheshimiwa Rais kupeleka nguvu ya kutosha katika michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuchukizwa na jambo la kupeleka bajeti ndogo. Mwaka jana tumepeleka billion 35.4, mwaka huu tunaomba tena 35.4 haya maono ya Rais yatafikiwa vipi? Ndoto ya Rais inafikiwa vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi hata siku moja na hata ukiangalia dhima ya Wizara. Dhima ya Wizara ni kukuza kuwezesha na kuendeleza utambulisho wa Taifa, maadili ya kiutamaduni, sanaa na michezo na wenyewe wakasema kabisa ili wafikie malengo haya lazima wawafikie wadau wafanye mageuzi kwenye taasisi wafanye utawala bora na uendelezaji wa miundombinu ya michezo huwezi ukafanya mambo hayo kwa bajeti hii tutakuwa tunataniana humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Wabunge wengi waliozungumza kuhusu bajeti, lakini vile vile kamati imesisitiza suala la bajeti. Sasa kwa nini sasa Bunge lako hili lisiichukue hoja hii kama hoja mahususi ikapelekwa mbele ya Kamati ya bajeti ili Kamati ya bajeti itakapofanya majumuisho na kujadiliana na Serikali suala la kuongeza bajeti likawa ni moja kati ya mambo yaliyoibuliwa kutokana na mijadala hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba kwa kuwa michezo ya kubahatisha kwa sehemu kubwa sana inategemea sports, inategemea michezo. Iwe kwenye betting ama kwenye casino au michezo mingine kutokana na hili nataka nikupe figures hadi Mei 2023 hadi Mwezi uliopita, Serikali imekusanya bilioni 146.9 na imevuka malengo ya kukusanya bilioni 131.5 sasa kwa fedha zote hizi zinatokana na sports unapelekaje 35.4? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hayo mambo hayaendi na kwa hali hiyo, napendekeza suala la michezo ya kubahatisha iwe chini ya Wizara ya Michezo nafikiri ni suala muafaka. Yawezekana tumechelewa lakini Serikali ilichukue suala hili, michezo hii ipelekwe chini ya Wizara ili fedha zote hizi zipelekwe kwenye michezo. Huwezi kuwa na kitu kinachozalisha bilioni 146na hadi Juni watafika hawa bilioni 170 halafu ukawape bilioni 35 ni mzaha. Hata Rais ndoto zake hazitaweza kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine. Sports betting inategemea sana mpira wa miguu sana. Hapa Tanzania 90% ya wanaocheza betting wana bet katika michezo ya mpira wa miguu hivyo industry ile inafaidika na mpira wa miguu. Tunarudisha nini na kwa hali hii nilikuwa nashauri Serikali ichukueni hili suala kwamba iwe ni sharti la kikanuni ya kupata leseni kwamba Kampuni ya Betting ili ipate leseni ilazimike kudhamini premier league clubs ama championship club hapo tutakwenda kusaidia nchi yetu katika michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hili hatuna budi kupongeza zile kampuni ambazo zimejitokeza sasa hivi, kuweza kudhamini clubs zetu mbalimbali naomba nizitaje chache tu. M-Bet wanaidhamini club moja iko hapa Msimbazi inaitwa nini? Simba, kuna kampuni inaitwa Meridian wanadhamini timu ya KMC, kuna Kampuni ya Ten Bet inadhamini Dodoma Jiji. Lakini bingwa wao Sports Pesa wanadhamini Young Africans, wanadhamini Namungo, wanadhamini Singida Big Stars. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tarimba.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa lakini Wizara toeni recognition kwa hawa watu ambao wanafanya vizuri ku-sponsor michezo yetu nchini. Naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)