Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara hii. Kwa sababu ya muda mfupi naomba kuungana na wenzangu wote waliochnagia kuhusu bajeti ya Wizara hii, kwa sababu haswa ndio kilichofanya nisimame kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunathamini maana saa nyingine tunasema hii Wizara ipo kwa bahati mbaya au kwa kitu gani? Michezo, Sanaa na utamaduni ni jambo mtambuka inayowagusa kuanzia watoto wa miaka miwili, mitatu, ukiona wale watoto wadogo mpaka wana-act namna gani, Mayele anafunga goli na wengine wana-act kama Joti anavyotembea ina maana wame wa-inspire watoto toka wakiwa wadogo, lakini mpaka wazazi mpaka wazee huku tunashabikia michezo, tunafatilia tamthiliya ili tupate amani, lakini ukiangalia bajeti inayotengwa kwenye Wizara hii kwa kweli inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemei bajeti kuu ya bilioni 35, naangaliaga bajeti ya maendeleo kwa sababu Serikali kama imeajiri watendaji sehemu ya mishahara ikaenda kama mishahara zingine kama oc zinaenda akama oc. Lakini bajeti hii ya maendeleo ambapo kwa mwaka uliopita ilitengewa bilioni 15 lakini mpaka mwezi Februari wizara hii imepata bilioni 5 peke yake na sijui kama sasa hivi wameongezewa sawa na 31%. Tunaongea habari ya kuboresha viwanja, tunaongea habari ya kujenga vyuo, tunaongea habari ya kufufa chuo cha sanaa cha Butimba sijui wizara inaweza kufanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongea habari ya kuweza kuhifadhi urithi wa ukombozi wa Afrika kwa bajeti hii ndogo kwa sababu Waziri wa Fedha yupo na Serikali hii iko hapa, nafikiri hilo watakuwa wameshalichukua. Lakini vinginevyo nampongeza sana Waziri, nampongeza pia na Naibu wake pamoja na watendaji wa Wizara kwa kweli tuseme kama ni upele umepata mkunaji. Tumeona kwa namna gani michezo Tanzania inapanda, hawa ni wachapakazi nawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunaona ni kwa kiwango gani amepaisha michezo Tanzania. Mama Samia Suluhu Hassan Mungu ampe uwezo, Mungu amlinde kwa sababu kwa kweli watanzania wameona kwa namna gani ametoa motisha kubwa. Kila mtu anafahamu ameanza ku-motivate wachezaji mara milioni tano, ameongeza dau milioni 10 ameongeza dau milioni 20, ametoa usafiri, anakaa na wachezaji wanakaa wanakula pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo kubwa sana la kuiga kutoka kwa viongozi wetu. Nampongeza sana lakini siyo yeye tu nawapongeza na Mawaziri. Nampongeza Waziri Mkuu kule kwake utasikia Namungo FC, nawapongeza Mawaziri huku ukienda kwenye majimbo yao michezo mingi, vipaji vingi vya wachezaji vinabebwa na Wahehsimiwa wengi Wabunge pamoja na Mawaziri. Ukienda huku utasikia Gekul Cup utasikia Issaay Cup, utasikia sijui Massay Cup. Wanatoa jezi, wanatoa mipira, chakula na nafikiri Wabunge wengi kwenye maeneo yetu ndio tunachokifanya na kuwasaidia wasanii kurekodi miziki na kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawapongeza sana lakini kwa kweli bajeti iongezwe tuone ni namna gani wanaweza wakafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya kuwa–support tumeona michezo Tanzania nawapongeza hata wanayanga wameweza kuibeba sifa ya nchi kwa kuweza kuingia fainali hongera sana, tunaendelea kupongeza timu nyingi wamekuja huku Serengeti Girls tumewapongeza wamepata sifa ya kuingia kwenye World Cup, Tembo Worriors, wamekuja vijana wa riadha Gabriel Geay, kina Isumbi yaani kwa kweli nawapongeza, hii yote ni kwa sababu tunawa–support. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwamba vipaji hivi vinaanza toka utotoni. Hawa watoto wadogo kama timu kubwa inapata makocha hivi kwa nini hawa watoto wadogo tusianze kuwajenga kuanzia leo. Sisi zamani tulikuwa na maeneo ya wazi ambayo tunacheza michezo kama rede sijui hata inapotelea wapi? Lakini ni michezo ya kuwajenga watoto hasa kwa akili. Sasa maeneo yote yale ya wazi yamejengewa hakuna maeneo ambayo watoto wanacheza wanafungiwa ndani. Michezo ingesaidia Watoto kuwajengea akili pamoja na kuweka mahusiano na kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Waziri katika kuhitimisha pengine uwaelekeze sasa kama ni Wakurugenzi au kwenye maeneo yote huko ya kata ya vijiji, waendelee kutenga maeneo wazi watoto wanacheza barabarani, wengine wanafungiwa ndani. Ili kutoka pale waendelee kujengewa uwezo lakini wapo taluma ya michezo, sanaa na utamaduni waanze kufundisha, waingie kwenye mitaala wafundishwe kuanzaia shule za msingi, sekondari, mpaka vyuo vikuu. Tuweze kupata vipaji kwa sababu hii ni ajira tosha. Ukichukua vijana watano wa Tanzania ukaambiwa chagua wangapi Kwenda shamba wengine kwenye michezo, kwa kweli watatu wataenda kwenye michezo. Kwa hiyo, michezo ni ajira kwa vijana wengine wanapotea kwa kukosa support na kwa hiyo hii ingia kwenye mitaala vijana wafundishwe, wawe-couch kuanzia huku chini siyo timu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kusemea ni bahati tuliyopata Tanzania ya kuwa center ya kuhifadhi urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika. Hapa naomba tu kwamba tunamuenzi Baba wa Taifa yeye ndio aliyesema Tanzania haiwezi kuwa huru, mpaka Afrika yote iwe huru na kwa heshima hii, sisi tumekuwa center ya kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tujenge hili ambalo limeanza kujengwa kutoka 2003 kwa msaada wa UNESCO na Tanzania kwa kweli ni center nzuri ya utalii wa kiutamaduni na tunapata wageni wengi wa kuja kujifunza kwetu, hasa hawa ambao sisi tumewasaidia katika Ukombozi wa Bara la Afrika hasa nchi za Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watakwenda kupata kumbukumbu zao kuna maeneo mengi ya kuhifadhi ikiwepo Dar es Salaam, Mazimbwi, Kongwa pamoja na sehemu zingine. Kwa hiyo, kote huku kuhifadhiwe ijengwe kumbukumbu nzuri, wahifadhi makaburi, watafute zile documents za zamani kuwe na maktaba kubwa na ukumbi ili wenzetu wakute hizi historia. Tanzania ni nchi ya pekee iliyokuwa na uzalendo kusaidia nchi za Afrika Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa uletwe Muswada wa kisheria wa kuweza kuhifadhi hizi kumbukumbu za kiutamaduni ili utamaduni huu usiweze kupotea.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Yustina.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga hoja mkono. (Makofi)