Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa fursa ya kuchangia leo katika bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumpongeza Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya, kuipa uzito suala zima la michezo. Wote tutakuwa mashahidi baada ya kuona kazi kubwa inayofanyika na hasa kwenye sekta ya michezo, Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa amewekeza ametoa support kubwa kumaanisha kwamba sekta ya michezo imeshika hatamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Rais kwa uzalendo wa kutoa fedha lakini pia kutoa ndege kuisafirisha Timu ya Yanga kwenda kushiriki mashindano ya shirikisho. Na hivyo nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wananchi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuliletea heshima Taifa letu hili. Yanga wamefanya kazi kubwa sana ya kutuheshimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme, na niwe mkweli hapa, kuna watu wanausemasema ushindi wa Yanga; naomba nikwambie kwamba ushindi Yanga tulivyoshinda ni tofauti na ushindi huo wanaouzungumzia enzi za Ukoloni, utaona kabisa Yanga tumeshinda aggregate, maana yake tumeshindwa kikanuni tu. Kwa hiyo niwapongeze sana wachezaji wote wa Timu ya Yanga, lakini niupongeze uongozi mzima na mashabiki wote wa Yanga, kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mimi nataka nijikite hasa kwenye suala zima la sanaa na michezo kwenye Halmashauri zetu hizi za Msalala, Ushetu, Kahama na nyingine. Kwa suala zima la sanaa sisi tunaotoka kwenye maeneo megine, na hili nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, mama yangu, utakapokuja kusimama hapa, mtueleze, hivi hili suala la sanaa, michezo, wasanii kwa maana ya Bongo Fleva, waigizaji; hivi ni Dar es Salaam tu, maeneo mengine hatutambuliki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote ni mashahidi hapa, mtaona, wasanii wetu kwenye maeneo yetu wana vipaji vikubwa mno lakini hawana support. Lakini leo hii utaona vipaji vyote vinatoka Dar es Salaam, yaani ili mtu aweze kutoka kuwa msanii bora, ni lazima aende Dar es Salaam. Sasa wale wanaotoka kwenye maeneo yetu ni lini hasa watakuwa; ni lini hasa Serikali itatengeneza utaratibu mzuri, mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba na wale wanaotoka kwenye maeneo ya vijijini waweze kukua?

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Iddi Kassim, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hamisi Taletale.

TAARIFA

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimpe taarifa babu yangu, Mheshimiwa Sheikh Iddi Kassim, kwamba hawa wasanii ambao tunawaona Dar es Salaam siyo kana kwamba wanasaidiwa na Wana-Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano msanii kama Diamond anatokea Morogoro na Kigoma, amejisaidia mwenyewe kufika pale. Tusiupe mzigo Serikali kwamba watu wanaobakia Morogoro wasaidiwe na watu wa Morogoro. Kwa hiyo taarifa yangu ni kwamba, ndugu yangu, Mheshimiwa Iddi, kama unataka kuhamia Morogoro ili utoke karibu Morogoro, mlezi wa vipaji ni mimi hapa.

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Iddi Kassim, taarifa unaipokea?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo mimi siipokei kabisa kwa sababu ninao akina Babu Tale zaidi ya 20. Narudia; ninao akina Babu Tale zaidi ya 20 wako Kata ya Bulyanhulu, wana uwezo wa kusimamia wasanii kwenye maeneo yale. Tunao wasanii bora kwenye maeneo yetu, hasa Kata ya Bulyanhulu na maeneo mengine Kahama, tunao. Tunao waandaaji tuzo, wapo wengi, Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu. Sasa msitufanye sisi tunaotoka kwenye mikoa huko kuwa ni maeneo tu ya Mawaziri kuja kuzindua Doto Cup, Iddi Cup, Saashisha Cup na kubaki maeneo mengine ni Dar es Salaam tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Wizara iweke mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba…

MHE SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Iddi Kassim, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Saashisha.

TAARIFA

MHE SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba ni kweli nchi hii ina vipaji vya wasanii wengi. Pale Jimbo la Hai tuna Jukwaa la Wasanii, wasanii wengi, na Mheshimiwa Naibu Waziri tulikwenda naye, aliona vipaji vikubwa na yeye mwenyewe akashangaa, akauliza hapa ni Hai au tuko wapi. Kwa hiyo ni kweli tuna vipaji vingi Mheshimiwa Waziri washuke watambue vipaji hivi na kuvisaidia, ahsante sana.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Iddi Kassim, taarifa unaipokea?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo naipokea kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano; tunaye msanii mmoja anaitwa Issa Jim, yupo Kahama. Msanii huyu ni professional boxer, anamiliki mikanda miwili, ameshinda International UBO, anao mkanda huo Kahama; ameshinda pia mashindano ya Afrika Mashariki (WABA); ameshiriki mashindano matano, manne ameshinda moja ametoa draw, yupo Kahama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini toka anaanza kuandaa mashindano haya hakuna support ya aina yoyote ile aliyopewa na wala hatambuliki na wala hata hapa hajaalikwa. Leo tunawaona akina Mandonga wako hapa, lakini kwenye maeneo yetu kule hamuwaaliki. Ni lazima tusimame na tuseme kwamba Watanzania wote tuna haki sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara pelekeni, waelekezeni maafisa utamaduni kwenye maeneo yenu huko kuhakikisha kwamba wanashiriki kuibua vipaji, kusaidia wasanii ili na wao waweze kufika kwenye maeneo haya. Kaka yangu, Mheshimiwa Babu Tale, amesema hapa, Diamond ametokea Kigoma. Leo hii Wana-Kigoma angekuwa Kigoma kule leo tungekuwa tunamhesabu ni mtu wa Kigoma. Tunahitaji tusambaze keki hii kwenye maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri, dada yangu, mhakikishe ya kwamba mnakwenda kuwaelekeza hawa maafisa utamaduni kwenye maeneo yetu ili wafanye kazi. Wasanii hawapewi ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho; leo hii utaona ofisi hizi; BASATA, COSOTA, zote ziko Dare es Salaam. Leo hii msanii anayetoka Kata ya Bulyanhulu anaandaa kazi yake. Ili apate kibali maana yake ni kwamba aandae kazi akiwa Bulyanhulu, apande gari aende akapate kibali Dar es Salaam, na mwisho wa siku akirudi huku bado hawa watu wa COSOTA anakuwa hana hati miliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini mkazi wa Bulyanhulu atatoka aende Dar es Salaam kupata kibali; kwa nini msifungue ofisi hizi au mkawakaimisha hawa maafisa utamaduni kwenye maeneo yale ili kuhakikisha kwamba wawasaidie wasanii wetu kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za usafiri, msanii anatoka hana ndugu wala rafiki Dar es Salaam, anajichanga changa anakwenda mwenyewe Dar es Salaam, matokeo yake ni nini, anaingia kwenye mambo mabaya ambayo yatamhatarishia maisha yake. Kwa hiyo niombe sana kwamba wasanii wetu hawa wanahitaji kupewa ushirikiano kwenye maeneo yao hayo ya huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kodi mbalimbali. Leo hii tumeona ili mtu aandae kibali, tamasha, kwa mfano pale Shinyanga kuna taasisi inaitwa HolySmile. HolySmile yeye mwenyewe amejichanga changa ameamua kuanzisha sasa tuzo mbalimbali, kutafuta ni nani msanii bora na ni nani mwimbaji bora. Lakini ili apate kibali, gharama yake anatakiwa alipe 1,500,000. Hebu punguzeni, pia muone namna ya kupunguza gharama hizi, ni kubwa sana kwa wasanii hawa wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo mnayotoa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kassim.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie la mwisho; mikopo hii mnayotoa mnawapa wasanii wakubwa, kwa nini hamuwapi hawa wasanii wanaochipukia huku chini? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kassim.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. Lakini kwa kumalizia ninaomba pia Mheshimiwa Waziri aongee na Kampuni ya Barrick kama alivyosema Mheshimiwa Sanga hapa, waweze kutujengea uwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.