Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Mimi pamoja na mambo mengine ni mwanataaluma wa Michezo, Wizara hii nasema inanihusu sana. Mimi ni Mwalimu wa Mpira wa Miguu kwa taaluma, nina Diploma C ya CAF. Kwa hiyo nachangia kama mdau wa michezo sio tu wa siasa peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuendelea napenda nitoe pongezi kwa rafiki yangu Paul Nonga ambaye ni kocha mwenzangu, mchezaji wa Mbeya City. Leo ni siku yake ya mwisho kuwa kama mchezaji wa mpira. Ametumikia nchi hii zaidi ya miaka kumi kucheza mpira Yanga na timu zingine pamoja na Timu ya Taifa ya Tanzania. Kwa hiyo namtakia Kheri katika maisha yake mapya ya ualimu na menejimenti ya mpira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze ndugu yangu Waziri, Mheshimiwa Pindi Chana na Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuchukua nafasi ya kuendesha Wizara hii. Mimi nina matarajio makubwa kwao na nawapongeza, naamini kabisa watafanya kitu kutusogeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nina machache tu nataka niwapitishe Waheshimiwa Mawaziri, ni highlights, lakini kubwa zaidi wanafahamu kuna changamoto hii ya jana au juzi kulikuwa na tuzo hizi za wasanii, Mheshimiwa Khadija hapa amezungumzia. Wasanii kutokuwepo ukumbini, kwangu mimi hilo sio kubwa sana, lakini la kwangu nimesikia uvunguni watu wanalialia kwamba tuzo zilikuwa mikono mitupu hazikuwa na chochote. Mwaka jana watu walipata fedha kidogo angalau motisha, lakini mwaka huu kulikuwa hamna kitu, imesikia, wanalalamika uvunguni. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba alifanyie kazi, kama sio sasa hivi basi wakati ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, linguine, naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie kuzungumza na Baraza la Michezo la Taifa. Najua kuna masharti ya usajili wa vyama vya michezo. Mimi ni mdau wa mchezo wa kuvuta kamba, nimekuwa Mwalimu wa kamba Timu ya Bunge na nimewezesha timu hii kuweza kushinda Ubingwa wa Afrika Mashariki kwa upande wa Mabunge kule Arusha, nadhani wengi watakuwa wanakumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa sasa ni matamanio yangu kusajili Chama cha Mchezo wa Kamba. Masharti yanataka kila wilaya kuwe na vyama na nini iendelee mpaka juu, nafikiri ndio sheria, wako sahihi, lakini naomba tuombe kama special case, michezo isiyo maarufu iweze kuanza na tuweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nina mambo mawili makubwa ya kuchangia leo. La kwanza, ni namna ya kupata Timu ya Taifa kwa baadaye kwa maana ya kutengeneza watoto wetu, lakini la pili, manung’uniko yangu au discomfort kwa namna ambavyo Chama cha Mpira Tanzania wanafanya. Kabla ya kwenda popote niwapongeze tu hao watu wa TFF, menejimenti ya sasa wakati wao tunaona achievement kubwa kwa mpira wetu wa Tanzania. Timu ya Walemavu, Timu ya Wanawake, Timu za Simba na Yanga zimekwenda mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Yanga juzi ametoka fainali bahati mbaya hakuchukua, tunawapa pole, lakini tunawapongeza kwa hatua. Kwa hiyo yote haya mazuri ambayo yanasemwa ni wakati wa Menejimenti hii ya TFF. Kwa hiyo nawapongeza sana wale seating leaders.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Baraza la Michezo la Taifa, kiongozi yupo pale mtendaji Neema Msita binti mdogo na timu yake, wengine wote kiujumla nawapongeza kwa sababu haya yote mazuri ya nchi hii yametokea wakati wao wako madarakani. Kwa hiyo niseme tu wanastahili pongezi nawashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kuhusu Timu za Taifa; nadhani tuafahamu wachezaji wengi tunawaona wakiwa wameshakuwa maarufu kwenye Vilabu vya Ligi Kuu, tunawaita National Team, lakini sidhani kama kuna mtu anawajua wachezaji wa Timu ya Taifa ambao wapo leo, lakini miaka kumi iliyopita au kumi na moja tulikuwa tunawafahamu wakiwa wadogo, ukweli hatukuwafahamu. Kwa hiyo kulingana na uchache wa muda naomba tu nishauri machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, niombe jambo hili la kutengeneza future ya Timu yetu ya Taifa liwe la Serikali kiujumla kwa maana ya TAMISEMI na Wizara ya Michezo na Wizara ya Fedha tulichukue liwe jambo la kwetu. Napendekeza Halmashauri zote nchini zielekezwe na Serikali kuwa na academies, kuwe na timu za watoto under twelve, under seventeen zisimamiwe na halmashauri wenyewe. Watu wa TFF au watu wa Serikali kwa maana ya Wizarani watatoa tu utalaam kule chini. Watakuwa na timu ya wataalam kwenda kuangalia facilities ziweje.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mgungusi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Sanga.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza Coach wangu pale ni kitu right kabisa. Kwa Afrika the best development modal ya soka iko Zanzibar ambayo wameitumia Ghana, wameitumia Nigeria, wameitumia Cameroon. Kwa hiyo mfumo mzuri wa kuzalisha wachezaji, upo kwa majirani zetu Zanzibar ambao tunaweza tukautumia na tukazalisha wachezaji wazuri kwa kuwa na academy kwenye kila eneo. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mgungusi, taarifa unaipokea?

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa na nashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni hilo nilikuwa nakazia tu. Kuna kila sababu ya zile halmashauri zetu ziweze kuwa na timu. Tunatenga fedha mapato ya ndani kufanya vitu kama zahanati na vingine vingi vya msingi, lakini jambo la michezo kuwa na timu za watoto kwenye halmashauri ni jambo la msingi. Tunajua unaweza kuwa mzigo mkubwa sana kwa halmashauri, lakini Wizara ya Michezo, Wizara ya Fedha iweze ku-subsidize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapelekewa kule chini fedha za maendeleo hata fedha ya kulea hizi academy kule halmashauri ziwepo. Tuna Walimu wengi wanazalishwa na TFF, hawa watu wanasoma intermediate level wengine wanasoma preliminary ualimu, wengine diploma C, wapo mtaani wanazurura wangeweza kupata ajira kwenye halmashauri zote kuwatengeneza watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mtoto anatengenezwa, professionally tangu akiwa mdogo ana miaka 12, ana miaka 10, akifika huko juu anakuwa na uelewa mkubwa kuliko leo, mtu anatokea mtaani amejilea mwenyewe, anakuja kukutana na Coach Professional akiwa tayari mkubwa amezeeka, hafundishiki. Ni changamoto kubwa, wengine watalaumiwa wahuni, hawazingatii, hawafundishiki kwa sababu ya mazingira kama hayo. Kwa hiyo naomba hilo tu nishawishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, linguine, tumwombe Mheshimiwa Rais kama tunakwama. Ametoa fedha tumejenga madarasa nchi nzima. Miundombinu mingine mingi ya Barabara, kila Jimbo limepata fedha, amesaidia, sidhani kama atashindwa kutusaidie kujenga viwanja vile vya standard nzuri kwenye kila halmashauri, halafu mambo ya malezi tutafanya wenyewe kama halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni suala la manung’uniko yangu. Kutokuwa na furaha na amani namna ambavyo ndugu zangu TFF ya leo wanaendesha hii hali ya mpira wetu. La kwanza kabisa, tunafahamu na wenyewe wanafahamu na Wizara pengine inafahamu kumekuwa na malalamiko mengi dhidi yao. Pengine najua wako kwenye nafasi nzuri kama hizo za maendeleo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha, malizia sentensi.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naam.

MWENYEKITI: Kengele ya pili imelia, kwa hiyo muda wako umekwisha.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sekunde chache nimalizie.

MWENYEKITI: Sekunde thelathini, malizia.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Waziri, naomba asimamie, kuna wataalam ambao ni Walimu wetu wa mpira wanadai TFF fedha waweze kulipwa, lakini kuna watu wengine nafikiri wanafungiwa fungiwa, TFF wanashindwa kuwavumilia, naomba awasaidie.

la mwisho, kuna suala la uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Wanawake amezungumzia Mheshimiwa Chumi, naomba TFF walifanyie kazi. Wizara naikabidhi tutaonana Bunge la Septemba, tutazungumnza vizuri. (Makofi)