Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo kwenye hotuba iliyoko mbele yetu na kwa sababu ya muda nienda straight kwenye hoja zangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu tumekuwa tunatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara, nyingine za nchi na nyingi pia za jasho la walipa kodi. Kwa bahati mbaya sana barabara hizi zimekuwa zikichukua muda mfupi sana kwa sababu kwanza viwango vya ujenzi ni dhaifu, utunzaji wake ni dhaifu lakini pia tunatumia makandarasi ambao baadhi yao hawana viwango vya kuweza kujenga barabara kwa uhakika. Badala ya kutengeneza barabara angalau tumalize miaka kumi ili tuhame kutoka eneo moja twende eneo lingine tunarudi mle mle huku maeneo mengine hayana barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wabunge wanazungumzia juu ya kubandua barabara za lami kujenga nyingine wakati mikoa mingine wako kwenye udongo. Miaka 54 ya uhuru tunabandua lami na kurudisha lami pale pale wakati wengine wako kwenye udongo hawajui ni lini watapata barabara za lami. Kwa hiyo, tatizo kubwa ni kwamba hatusimamii vizuri barabara zetu. Ifike mahali tuwe na standards za ujenzi wa barabara nchi nzima. Tuamue kwamba mkandarasi ambaye anashindwa kukidhi vigezo vya matengenezo tunayoyataka asipate kandarasi. Kwa sababu ya kubeba wakandarasi mtu anaharibu huku anapelekwa kule, matokeo yake tunaingiza hasara kubwa kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwenye barabara nyingi, niseme kabisa barabara zilizotengenzewa ndani ya miaka kumi ya uongozi wa Awamu ya Nne zote ziko kwenye hali mbaya. Nyingi zina mashimo mengi, nyingi zina migongo, nyingi zinaanza kuchimbika kuanzia pembeni, Awamu ya Nne barabara zote zimeharibika. Pamoja na kuwa anasifika kwamba alitengeneza barabara nyingi lakini kaziangalieni, nimefanya utafiti barabara nyingi za uongozi wa Kikwete ziko kwenye hali mbaya kwa sababu usimamizi ulikuwa mbovu. Hatuwezi kuwa na barabara za lami za kutosha kama tunashindwa kuweka standards kwa ajili ya barabara zetu za lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, tumekuwa tunatoa fedha kidogo kidogo kwenye ujenzi wa barabara matokeo yake tunaweka vyombo vya ujenzi barabarani kwa muda mrefu na tunalipa wakandarasi waelekezi kwa muda mrefu, tunapoza fedha nyingi sana za walipa kodi kwa kitu ambacho hakitakiwi. Tunapotengeneza barabara miaka minne, mitano haijakamilika lakini vyombo vinalipiwa, mkandarasi mwelekezi analipwa, how much are we wasting? Ni pesa nyingi sana tunapoteza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe na utaratibu, tunapopanga kutengeneza barabara tuitengee muda, ndani ya mwaka mmoja, miwili ikamilike ili tuokoe fedha na faini tunazolipa kwa ajili ya kuweka vyombo barabarani wakati huo hatutoi fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara zile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la reli. Suala hili ni uchumi wa Taifa. Ni jambo la ajabu kwa nchi inayotegemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 80, leo tuna reli kwanza sio za standards, zinabomoka kila siku, lakini kwa kiwango kidogo, ni aibu mpaka leo. Sambamba na kwenda kwenye uchumi wa viwanda, sambamba na kwenda kwenye uchumi wa kati, suala la reli halikwepeki. Kwa hiyo, katika mawazo yote ya Serikali ili tuweze kwenda pamoja lazima suala la reli lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza nilianza kuumizwa na Waziri wa Fedha. Kwanza alikuja na mpango wa kwanza kwamba lazima tutengeneze reli ya kati kwa standard gauge, tulipokwenda Dar es Salaam kwenye semina anasema kwamba tunatafuta wabia na nchi ambazo tuna-share matumizi ya reli hiyo, hatuwezi kutegemea watu wa nchi nyingine, pengine kwao reli si priority lakini ndani ya nchi yetu reli ni priority. Kwa hiyo, ni lazima tujipange sisi wenyewe kuhakikisha kwamba tunajenga reli zetu? Leo tunategemea Burundi, Burundi kwake pengine reli si priority, au Rwanda, it is not their priority, au Kenya, sisi kama sisi tunafanyaje?
Kwa hiyo, suala la reli ya kati na matawi yake ina-cover karibu mikoa 15 ya nchi hii. Wengi wamezungumza kwa msisitizo tunaomba wakati wa ku-wind up kesho tuambiwe tarehe ya kuanza na kumaliza kujengwa reli ya kati na kwa standard gauge, halikwepeki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la upungufu wa mabehewa. Kuna shida kubwa ya upungufu wa mabehewa ya abiria. Reli yote hii ya kati mabehewa ni machache sana matokeo yake imeleta matatizo makubwa. Leo Wabunge walikuwa wanazungumzia suala la bei kwenda juu pamoja na kuwepo kwa walanguzi, shida kubwa ni mabehewa machache. Leo ndani ya Wilaya ya Kaliua kwenye stop station ya Kaliua kwa siku moja, kwanza treni ni siku mbili tu kwa wiki, lakini hiyo siku mbili eti siku kumi, can you imagine? Watu kumi kwenye kituo kwa wiki mara mbili! Reli iko kwenye wilaya yao, wengi hali ya uchumi ni mbaya, hawana uwezo wa kutumia 50,000, 60,000 kwa basi angalau reli ndicho chombo chao wanaambiwa siti kumi. Matokeo yake watu ambao si wasafiri na wanakwenda na vitambulisho wananunua wanakwenda kuziuza mitaani kwa wale wasafiri. Matokeo yake mtu badala ya kununua tiketi shilingi 23,000 ananunua shilingi 40,000 na huwezi kuzuia kwa sababu mabehewa ni machache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Waziri, amesema ameongeza mabehewa, lakini mengi ni ya mizigo, mabehewa ya mizigo kutoka 530 mpaka 704, lakini suala la mabehewa ya abiria ni shida kubwa. Pia tuongeze angalau route. Kwa kweli ni jambo la ajabu kuambiwa kwamba Wilaya ya Kaliua reli yote ya kati kituo kimoja, kwa wiki moja wasafiri watu 20, kwa kweli inasikitisha sana. Hatuwezi kukwepa suala la kuendelea kulanguliwa kwa tiketi kama hatuongezi mabehewa lakini pia kama hatuongezi angalau routes za treni tuweze kusaidia wananchi ambao treni pia ni tegemeo lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeki, suala lingine ni la mafao ya watumishi wa iliyokuwa TRC waliohamia RITES. Mwaka 2007 walipohama kutoka TRC kwenda TRL waliambiwa watalipwa mafao yao leo ni karibu miaka kumi hawajawahi kulipwa. Tunaomba Waziri wakati ana-wind up atuambie wale watumishi waliohamishwa kutoka TRC kwenda TRL mwaka 2007 mpaka leo hawajalipwa haki zao wanalipwa lini haki zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye barabara za Tabora. Mkoa wa Tabora mpaka tunapoongea umeunganishwa na mkoa mmoja tu, Mkoa wa Singida. Mwanza moja kwa moja mpaka Tabora bado, Mbeya bado, Shinyanya bado, Kigoma bado. Tunaomba sana, kuna barabara hii ya Nyahuwa – Chanya, ni kipande kidogo tu pale, kilometa 85.4 imetengewa fedha kidogo. Ni yale yale ninayoyasema, tukitenga fedha kidogo kidogo tunaleta gharama zaidi. Hebu tuhakikishe kwamba tunaweka fedha za kutosha barabara hii ikamilike ili angalau tuunganishe Dodoma na Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini barabara nyingine ni barabara ya Urambo - Kaliua. Ni barabara muhimu kweli kweli, imetengewa shilingi bilioni tano tu, sasa hizi ni za uchambuzi au za kufanya nini? Barabara ile ni fupi, kilometa 28, tunaomba Mheshimiwa Waziri aweke fedha ya kutosha angalau ikamilike. Leo ukienda pale una mimba changa inatoka, barabara hali ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni ya Kazilambwa - Chagu. Tunashukuru angalau kwa kipande kidogo imekamilika, kutoka Kazilambwa kuja Kaliua tayari, Kazilaumbwa kwenda Chagu kwa maana ya kuunganisha Tabora na Kigoma bado. Fedha iliyowekwa ni kidogo sana labda ni kwa ajili ya uchambuzi, sijui. Naomba barabara hii na yenyewe iweze kutekelezwa ndani ya bajeti hii ili angalau tuunganishe Mkoa wa Tabora na Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni ya kuunganisha kutoka Mpanda – Ugala – Kaliua, Ulyankhulu – Kahama. Ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Kaliua, Mpanda na Kahama. Barabara hii imewekewa fedha kidogo ya uchambuzi, tunaomba kwa bajeti ya mwaka wa kesho ihakikishe inajengwa kwa lami, ni barabara nzuri sana kwa ajili ya uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la viwanja vya ndege. Kiwanja cha Tabora ni matatizo, leo ni mwaka wa nne tangu kimetengewa fedha ya ukarabati, hakikamiliki kwa nini? Nashangaa Wabunge wanaosema kwamba ndege ni anasa, ndege siyo anasa, tunataka uchumi wa kati, tunataka wawekezaji. Leo unamtoa Mchina kutoka Dar es Salaam aingie kwenye makorongo afike Tabora saa ngapi? Angetaka apande ndege straight afike Tabora aangalie eneo la kuwekeza, arudi kwenye shughuli zake. Kwa hiyo, viwanja vya ndege ni uchumi wa nchi hii. Tunaomba Mheshimiwa Waziri akija atuambie kiwanja cha Tabora lini kitakamilika kwa gauge kubwa, kipanuliwe kiweze kuwa kiwanja ambacho kinaingiza ndege kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanja kile ndege kubwa haziingii. Ndege ndogo, nauli kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora ni shilingi 450, 000 nani mwenye uwezo huo? Gharama ni kubwa, wananchi wengi hawawezi. Kuna Mbunge kasema hapa tukiweza kuwa na viwanja vikubwa, ndege nyingi zikatua, zenye upana mkubwa hata gharama zinapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie kidogo kuhusiana FastJet, Wabunge wanasema kwamba FastJet ni rahisi, FastJet ni gharama kuliko maelezo, ni aibu. Kwanza mimi niseme FastJet ni wezi, ni wezi kabisa. Leo unachangishwa begi shilingi 200, 000, maji nusu lita shilingi 3,000 hii ni aibu, ni wizi wa hali ya juu. Anakwenda kuchukua maji kwa jumla jumla shilingi 300 kwa nusu lita anakuja kuuza shilingi 3,000 huu ni wizi, hakuna gharama ya unafuu wa aina yoyote.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Magdalena.