Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kibali kilichotuwezesha wote kuwepo hapa leo, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama yangu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa anayoendelea kuwa nayo juu yetu na ahadi yangu ni ile ile, hatutamwangusha, tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya nchi hii inaacha alama wakati huu wa utawala wake wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri kwa miongozo mingi ambayo amekuwa akinipa, Mama yangu experience yake na yeye inanifaa mpaka mimi sasa. Kwa kweli namshukuru sana najifunza mengi kutoka kwake na naamini naiva zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru Watendaji wa Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu, Ndugu yangu Saidi Yakubu na Naibu Katibu Mkuu Ndugu yangu Nicholas Mkapa na Watendaji wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa. Vilevile, naishukuru sana familia yangu, mapenzi ni mengi kwa kweli na wananchi wenzangu wa Muheza kwa kuendelea kuniunga mkono, kuniongoza na kunipa ushirikiano wa hali na mali, ninyi ni vyuma kweli kweli na Muheza inarudi kwenye ramani vizuri kama ambavyo tulikuwa tumekubaliana ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kuzipongeza timu zetu. kwanza kabisa, ninaipongeza timu ya Dar es Salaam Young Africans ambao wamekuwa washindi wa pili, niseme tu kikanuni kwa sababu Yanga hawakufungwa kwenye hizi mechi mbili za fainali bali walishindwa tu kuchukua ubingwa kwa sababu ya kanuni. Kwa hiyo, tunakubaliana wamefanya vizuri sana na wameiletea sifa kubwa nchi na hata zile fedha ambazo Mheshimiwa Rais alikuwa anatoa pamoja na ndege matunda yake yameonekana. Hongereni sana Dar es Salaam Young Africans. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Klabu ya Simba kwa kufika robo fainali ya ligi ya Mabingwa wa Afrika. Robo fainali ya ligi ya Mabingwa wa Afrika siyo nafasi ndogo na Simba imekuwa wakirudia mara kwa mara kiasi kwamba lengo sasa hivi ni kuivuka na ninaamini mkijipanga vizuri msimu huu unaokuja pengine tunaweza kuona maajabu. Vilevile, niwapongeze kwa outstanding performance consistently kwa miaka mitano iliyopita iliyosababisha mpate nafasi ya kushiriki Super League. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Super League ni league ya vilabu vya Afrika ambavyo vinahusisha timu nane. Tuna nchi Hamsini na kitu kwenye Bara hili lakini vilabu ni nane tu vilivyopata nafasi ya kushiriki. Ni vile vilabu ambavyo performance zao zinaonekana zina mashiko kweli kweli na vigezo vingine vingi ambavyo wameviweka, Klabu ya Simba imevifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kama timu ya Yanga na yenyewe itaendele na performance iliyoifanya mwaka huu basi pengine tutakuwa na timu mbili kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika wakati naongea nae kwamba, tuna vigezo Klabu ya Yanga inatakiwa ivifikie ili tuwe na timu mbili. Kwa hiyo kila la heri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujibu hoja kadhaa ambazo zimetangulizwa na Waheshimiwa Wabunge kabla Mheshimiwa Waziri kuja kuhitimisha hoja yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubaliane na hoja ya Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, kwamba utamaduni ni mtindo wa maisha na ni zile kawaida za watu na namna tunavyoishi, kwamba matatizo mengi ambayo tunayo yangeweza kuondoka kama tungeyatengenezea utamaduni na kuusimamia ukatekelezwa, hili nakubaliana nae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tuna mambo mengi na miongoni mwa mambo ambayo yamesemwa ni kuhusiana na taasisi zetu kushindwa kufikisha yale malengo ya maduhuli ambayo tulikuwa tumepanga kwamba tutayakusanya. Sasa kwa sababu ya muda nitoe mfano wa taasisi yetu moja tu ya COSOTA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumekubaliana kwamba COSOTA mwaka 2022 itakusanya shilingi bilioni 1.35 lakini walishindwa kufikisha na sababu zipo wazi. Sababu moja ni kwamba mazingira na sheria ambazo zilikuwa zimetumika kuweka matazamio yale wakati ule yalikuja kubadilika hapo katikati na yakwafanya wawe chini ya kiwango kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 2022 ambayo yalikuwa yanatuelekeza kwamba tutaaanza kukusanya zile kodi kwenye devices ambayo haijaanza mpaka sasa hivi lakini yenyewe tuliijumlisha kwenye makusanyo yao. Vilevile elimu kwa wale ambao wanatakiwa kulipa ile mirabaha na ushirikiano mdogo ambao tunaupata, lakini hilo ndugu zangu Wabunge tunalishughulikia na hasa wana Kamati ambao walilileta. Miongoni mwa mambo ambayo tumeyafanya hivi karibuni kwa maelekezo ya Waziri, nimewaomba COSOTA wanipe majina na idadi ya fedha wanazodai kutoka kwa wale wadaiwa wao sugu na wamefanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nitumie Bunge lako tukufu kutoa salamu kwa wale ambao ni wadaiwa sugu kwa COSOTA kama wanaona kwamba kutumia kazi za sanaa ni halali yao bila kuwalipa hawa wasanii waliozifanya kazi hizi wajiandae. Bunge hili litakapokwisha mimi kwa maelekezo ya Waziri nitakwenda mwenyewe mtaani kuhakikisha kwamba tunazifungia sehemu hizi na hazifanyi shughuli zinazozifanya za kutumia kazi za sanaa za nchi hii bila kuwalipa wasanii ambao wametoa machozi, jasho na damu katika kuzitengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niihakikishie Kamati kwamba hili tutalifanya na mimi kama msanii sitakaa hapa nione kwamba wasanii wengine wanadhulumiwa na haki zao hazipatikani kwa sababu tu ya matakwa ya watu kutotaka kutoa ushirikiano. Hiyo ni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ilikuwa ni hoja ya ndugu yangu Mheshimiwa Sanga kuhusiana na CSR za kampuni zinazotekeleza miradi mikubwa nchini zitusaidie kutengeneza miundombinu ya michezo kwenye nchi hii. Huu mpango sijui Mheshimiwa Sanga umeupata wapi lakini ni kweli kwamba sisi tulikuwa nao tayari sijui ni kidege gani kimekuibia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ina maelekezo ya kujenga stadiums mbili Arusha na Dodoma, miongoni mwa vyanzo vya mapato ni CSR za miradi mikubwa katika sekta ya fedha, nishati na madini. Sasa, tayari Wizara imeanza kufanya mawasiliano na Wizara husika nilizozitaja hapo na nikuhakikishie mawasiliano yanaendelea vizuri na tutalifikia lengo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia nyingine ambayo tumeipanga ni kuhimiza Corporate Social Investment, Wawekezaji wafanye uwekezaji wa kijamii ambapo unaweza kujenga viwanja ukavipa jina la Kampuni yako na kadhalika. Hilo nalo tunalifanyia kazi na nikuhakikishie tuko katika hatua nzuri na hili tutafanikiwa. Kazi tuliyopewa ni kujenga viwanja na hizi Arena na Mheshimiwa Sanga hizi fedha tutazipa na Arena na Stadium zitajengwa katika nchi kama ambavyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais yametoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mgao wa mapato wa viingilio. Hili ningetaka kujibia. Hili ni suala la kisheria na kikanuni Mheshimiwa Sanga na kitu ambacho hakiwezi kubadilika ni ile asilimia 18 ya VAT na asilimia tatu ambayo inakwenda kwa BMT. Hayo mengine ni ya kikanuni ambayo TFF inakaa na wadau wake ambao ni vilabu kabla ya msimu kuanza na wanakubaliana. Sasa kwa maoni yako na maoni ya Wabunge wengine wengi ambao walishayatoa kuhusiana na jambo hili, sisi tutaielekeza TFF wakati inakaa na wadau wake ambao ni vilabu kabla ya msimu ujao kuanza, waangalie haya makato kuona namna amabayo wanaweza wakawapunguzia vilabu vyetu mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli mimi kwa sababu ya kuwa mtu wa mpira humu ndani ndani, nafahamu namna ambavyo vilabu vinaingia gharama kubwa za kuendeshwa na namna ambavyo zinapitia wakati mgumu hata wakati mwingine kufika kituo kingine kwa ajili ya kucheza mechi zao. Kwa hiyo, tutafanya kadri tunavyoweza TFF waliangalie wasiwape mzigo vilabu vyetu na yale ambayo yanaweza kuongeleka na yakabadilika yatabadilika mtuachie sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la shule za michezo ulisema Mawaziri wawili wamepita. Nikuhakikishie Waziri Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana anakwenda kufanya miundombinu ile kwenye shule zetu za michezo hilo halitashindikana. Hivi ninavyokuambia tenda itatangazwa hivi karibuni ya marekebisho kwenye viwanja vyetu vya michezo na ujenzi wa viwanja vipya vya michezo kwenye zile shule zetu 56 utaanza. Kwa hiyo, kama lilishindikana huko sasa hivi halishindikani kaa utulie uone muziki ndugu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dada yangu Mheshimiwa Khadija (Keisha), alizungumzia kuhusiana na tuzo. Hili nalo nililiombea ruhusa maalum kabisa kwa Mheshimiwa Waziri ya kwamba hili suala la tuzo Mheshimiwa Waziri niachie mimi na nimekwishakabidhiwa. Tutakapomaliza Bunge hili la Bajaeti naanza kushughulika nalo kwa ajili ya tuzo zinazofuata. Kwa hiyo, hili niachie mimi wala usiwe na wasi wasi nalo na tutalipatia suluhisho. Tuzo za mwakani nikuahidi Dada yangu zitakuwa za aina yake na zitakuwa za picha tofauti kabisa na ilivyokuwa huko nyuma. (Makofi)

(Hapa kengele I;ilia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mambo mengine ya kusema lakini naamini Mheshimiwa Waziri ameya – capture na atayasema wakati wa kuhitimisha hoja yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)