Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kushukuru maoni ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Elimu, Utamaduni na Michezo lakini pia nitumie nafasi hii kuwashukuru wachangiaji wote. Tumepata wachangiaji takribani 16 na michango hii yote tutaiwasilisha kwa maandishi kila hoja. Tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala kubwa hapa kwenye Wizara yetu ni habari ya bajeti. Mambo mengi mazuri yamezungumzwa yafanyike, reforms na kikubwa kabisa ambacho kimezungumzwa hapa ni suala zima la bajeti. Hili ni kweli kabisa, bajeti upande huu wa masuala ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo hii ambayo leo tumekuja kuomba Bunge letu bilioni 35. Kama alivyosema Waziri mwenzangu Mheshimiwa Mwigulu, kwamba hili ni eneo ambalo kimsingi tunaendelea kuangalia namna gani tuendelee kuliboresha kwa kushirikisha sekta binafsi na wachangiaji wengi wamesema tuone namna gani tunashirikisha sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tutakwenda kukarabati uwanja wetu wa Benjamin Mkapa. Hivi sasa kuna mechi ambayo tunaisubiri kati ya Tanzania na Niger itachezwa mwisho wa Mwezi wa Sita na niwatangazie Watanzania kwamba, mara baada ya mechi hii kukamilika tutafunga uwanja huu tayari kwa ukarabati. Ninashukuru sana kwa maoni ya Kamati walivyosema kwamba tubakize Benjamin Mkapa kwa ajili ya mechi kubwa tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa tunautumia uwanja huu ambao una uwezo wa viti takribani 60,000 hata kwa ajili ya shughuli mbalimbali za matamasha kama vile mahubiri, sala mbalimbali tulikuwa tunatumia lakini sasa tutatumia viwanja mbadala na uwanja huu ubaki kama hazina na alama ya Taifa letu. Kwa hiyo, tutakwenda kukarabati uwanja huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukarabati tunatarajia kujenga recreation center pale nyuma ya uwanja wa Benjamin Mkapa na recreation centre nyingine itakuwa hapa Dodoma, itakuwa ni viwanja viwili Dodoma pamoja na Dar es Salaam, kama alivyosema Naibu Waziri tayari Mkandarasi amekwisha kabidhiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunakwenda kujenga arena, wamezungumza hapa watu wanahitaji arena, haya ni maeneo ya kipaumbele, tayari tuna eneo la Kawe pale tutajenga arena pia tutajenga stadium mbili hapa Dodoma na nyingine tunatarajia kujenga Arusha ikiwa ni maandalizi pia ya kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ukidhi AFCON tunahitaji viwanja nane vya Kimataifa, lakini kwa kuwa tumeomba pamoja na Kenya na Uganda ukichanganya na wanatatarajia kuja Wakaguzi (Inspectors) kutoka Makao Makuu ya CAF hivi karibuni, tayari nimeongea na Waziri wa Michezo wa Kenya na Waziri wa Michezo wa Uganda tunaona namna gani ya kuhakikisha kwamba tunakidhi vigezo na masharti ili tuweze kufanikiwa AFCON 2027. Kwa hiyo miundombinu ya viwanja ni maeneo ya vipaumbele lazima tuone
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nimeshawasiliana na Waziri mwenzangu wa TAMISEMI pamoja na Waziri wa Elimu. Waziri wa Elimu tumekubaliana kwamba suala la somo la michezo liwe ni miongoni mwa masomo ambayo yanaweza kufundishwa na kufanyiwa mitihani liwepo kwenye mitaala, kwa hiyo, kuna mafunzo ya amali. Suala la masomo ya sanaa, muziki iwe ni miongoni mwa masomo ambayo yako katika curriculum zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kushirikiana na Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Elimu tumekubaliana kuwa, hakuna kusajili shule ya msingi au sekondari hadi watuthibitishie wana viwanja mahali hapo. Mtoto hawezi kwenda shuleni miaka saba bila kushiriki michezo, O – level miaka minne, A – Level miaka miwili bila kushiriki michezo, anakuja kukutana na michezo University, lazima tuwazoeshe wakiwa wadogo. Kwa hiyo, hiyo ni miongoni mwa mikakati ambayo tunayo kuhakikisha kwamba eneo hili la michezo linaendelea kuboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango mbalimbali, kuna hoja hapa kwamba kampuni ya betting ili ipate leseni kigezo iwe ni kudhamini timu ya mpira na sisi kama Wizara jambo hili tunaona ni muhimu tunalichukua tuone namna gani ya kulifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kushirkisha sekta binafsi pamoja na CSR, tuwe na sports academy za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilithibitishie Bunge lako mpaka sasa Wizara imesajili sports academy kutoka ngazi mbalimbali 180. Hivi sasa hata wadau binafsi wanatengeza viwanja kwa mfano Azam Complex. Pale Morogoro wamekuja kuomba vibali wanaweka uwanja pale, kuna Mmasai mmoja yeye amesema anataka eneo lake litumike kwa ajili ya uwanja wa michezo na ameingia makubaliano na Italy na analeta wataalam wa kufundisha michezo kwa vijana kutoka Italy. Kwa hiyo, hii ni sehemu ambayo pia ni miongoni mwa vipaumbele vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala limezungumzwa hapa la Ndondo Cup. Tunaamini kwamba Ndondo Cup ni eneo la kukuza vipaji, pia kwenye mchango wa Mwenyekiti wa Kamati amesema kwamba tuone namna gani ya kurasimisha eneo hili la Ndondo Cup, nasi tunasema kwa kuwa ni eneo ambalo linarasimisha vipaji, Ndondo Cup inaendelea kuwa muhimu kweli. Kwa hiyo, tutaweka utaratibu kwa kushirikiana na wenzetu wa TFF kuona namna gani vibali vinaweza vikatolewa taratibu na wadau wanaotaka kuendesha mashindano haya waweze kushirikishwa na kutambulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kushirikiana na sekta binafsi kama Mabenki kuweza kuuza haki za majina ya viwanja. Kuna baadhi ya viwanja ukienda nchi nyingine unakuta uwanja una jina la benki fulani labda CRDB. Kwa hiyo, hayo ni maeneo ya kimkakati ambayo tunataka tuhakikishe kwamba tunashirikisha sekta binafsi na tuweze kuendeleza eneo hili la michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mikoa tumezungumza hapa imeonekana kama wasanii wengi, wachezaji wengi wanatokea Dar es Salaam, niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa kwamba katika kila Halmashauri tuna Afisa Michezo, katika kila Halmashauri kuna Afisa Utamaduni na Sanaa maeneo haya kuna Kamati maalumu za kichezo na Mwenyekiti wake kwa ngazi ya Wilaya ni DAS na kwa ngazi ya Mkoa ni RAS. Kwa hiyo, nitoe wito sasa kwamba Kamati hizi zinapaswa kukutana na kuweka mikakati ya kutosha na hivi sasa tunakwenda katika michezo mtaa kwa mtaa, tunakwenda katika suala la sanaa mtaa kwa mtaa, tumeingia makubaliano ya michezo mashuleni kwa kushirkiana na FIFA tutatoa mipira 2,000 kila Mkoa katika spirit ya kuendeleza michezo mtaa kwa mtaa. Kwa hiyo, tayari tumekwishaingia makubaliano (MOU) pamoja na FIFA kwa kushirikiana na TFF ili kuona ni namna gani tunaboresha na tunahamasisha suala zima la michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na swali pia inakuwaje kwamba labda watu wanataka kusajili masuala ya sanaa wasafiriki kutoka mikoani? Sasa hivi kupitia Wizara tunataka kuweka utaratibu wa ku–digitalize. Kwa hiyo, unaingia kwenye www.sanaa.basata.go.tz mahali hapo unaona taratibu zote za kusafiri hauhitaji kusafiri. Unaweza ukawasiliana na Maafisa wetu walioko katika ngazi za Serikali za Mitaa, kila halmasahauri tuna Maafisa Michezo, Maafisa Utamaduni, tunataka kuendeleza eneo hili kwa sababu tunajua linaajiri vijana wengi kabisa na baada ya sensa vijana wapo takribani zaidi ya milioni 30, kati ya idadi ya watu milioni 61 zaidi ya 51 percent ni vijana, ni lazima tuweke mikakati ya kuhakikisha kwamba vijana hawa wanashirikishwa na wako imara kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, tunao Mfuko wa Utamamduni, na mfuko huu kazi yake ni ku-support kutoa mikopo. Tumeshatoa mikopo takribani shilingi 1,077,000,000. Sasa tunaangalia namna gani ya kufika nchi nzima. Mikopo hii wanapewa watu wote; awe ni msanii maarufu, hata asiye maarufu, wote wana haki pale ambapo vigezo na masharti vimezingatiwa. Kwa hiyo, tunaendelea na mazungumzo na Mabenki yetu na taasisi za kifedha. Lengo ni kwamba hizi benki zina branch katika kila wilaya na kila mkoa. Tumeshaanza mazungumzo na benki mbalimbali ikiwa ni pamoja na National Bank of Commerce kuona ni namna gani tunaweza tukaingia makubaliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa na fedha ya kukopesha, tunaipeleka benki, tunasema sasa wewe benki utoe kwa niaba yetu. Huu ni mkakati ambao tumeujadili hapa Bungeni kwa pamoja, pia kuona ni namna gani tunawezesha vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, huo ni mkakati ambao tunao, tunataka kila mwenye uwezo wa kupata fursa, kupata mitaji ya kuendeleza masuala ya utamaduni, sanaa na michezo, waweze kupata mitaji. Kwa hiyo, Wizara imedhamiria kuleta mageuzi na tuko imara kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la vazi la Taifa, niwahakikishie Kamati kwamba suala hili ni jambo ambalo tuko makini, tuko serious. Mchakato huu ulishafanyika hapo awali na ulienda hadi ngazi za Wizara, lakini Wizara tulitoa maelekezo mengine kwamba warudi kupata maoni mengine. Wameshamaliza kukusanya maoni Visiwani na Bara na hivi karibuni watakwenda kuwasilisha ripoti maalum kabisa. Tumeshawapa deadline, wahakikishe kwamba suala la vazi la Taifa linakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mdundo wa Taifa, tayari tuna Producer’s Kit ili mtu anapotaka kuweka nyimbo, aweke nyimbo yenye Mdundo wa Taifa. Kwa hiyo, hili la vazi la Taifa tunaelekeza Kamati kwamba wahakikishe wanakamilisha suala hili mapema kabisa liweze kukamilika kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kama nilivyosema, maoni yote tunachukua, lakini tunaendelea na suala zima la kubidhaisha Kiswahili. Tunataka Kiswahili kiwe na manufaa, vijana wetu waweze kufundisha Kiswahili, waweze kutoka nje ya nchi, na waweze kuwa Wakalimani. Tuna ushirikiano na nchi mbalimbali kama tulivyosema awali, Ujerumani na hata Spain tayari wameshatuomba tuwapeleke walimu wetu kujifunza Spanish. Kwa sababu ukijua Kiswahili lazima ujue na lugha ya pili ili kuweza kutafsiri; kama ni Kiarabu, kama ni Kifaransa, au lugha nyingine. Maana ukijua tu Kiswahili peke yake, bado, lazima tuwe na lugha ya pili. Kwa hiyo, tunaendelea na mkakati wa kubidhaisha lugha yetu ya Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye mara kwa mara amekuwa akitoa hotuba hata ngazi ya AU kwa lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo, Watanzania wenzangu, Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kutumia lugha yetu hii ya Taifa. Mataifa mengine wanathamini sana lugha zao, wanajali lugha zao. Tumeshatoa kamusi, tuendelee kutumia lugha yetu, tufurahie lugha yetu. Vilevile tunazo filamu kwa lugha ya Kiswahili. Tuwe tunapenda kuangalia sanaa zetu na utamaduni wetu, tuufurahie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja kwa upande wa filamu kuhusu vibali. Vibali vya Filamu tunaendelea kuvitoa kupitia Bodi ya Filamu na sasa hivi mambo mengi tunafanya online, haihitaji mtu kusafiri. Pia tunatoa documentary, siyo tu filamu za kawaida, documentary za kufundisha, Historia na documentary mbalimbali. Huo ni mkakati ambao tunao. Huko nyuma tulikuwa tunatoa filamu 200 kwa mwaka hivi sasa niwahakikishie Wabunge tunakwenda mpaka filamu 2,000 kwa mwaka. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo limechukua vijana wengi na vijana wengi wanakuwa maarufu ndani na nje ya nchi. Kwa hiyo, hii ni mikakati ambayo tunaendelea nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli yeye amekuwa ni chachu upande wa michezo, amekuwa ni kinara kabisa upande wa michezo. Taifa letu leo linajulikana ndani na nje ya nchi. Tumeendelea kupata maombi mbalimbali. Hivi sasa timu ya cricket Taifa wana mashindano yao ya kimataifa, wameshaleta maombi, tunaomba Tanzania mtu-host. Hii yote ni kutokana na uongozi bora wa Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha kabisa anapenda michezo, lakini siyo tu michezo, hata masuala ya utamaduni na sanaa. Watu wa utamamduni na sanaa tunamtambua kwa jina la Chifu Hangaya. Tuko naye, yuko vizuri. Mheshimiwa Rais ameacha alama maeneo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, sasa naomba kutoa hoja.
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.