Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na heshima ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika bajeti hii ya Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kuendelea kutupa uhai na afya ili kuendelea kuitumikia nchi yetu kupitia Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza mchango wangu, nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kipenzi chetu, mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan; Waziri mwenye dhamana na viongozi wote wanaomsaidia Rais katika Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu leo tunaposimama hapa kuzungumza na kutathmini kazi ya Wizara ya Fedha tunayo furaha kwamba miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa sababu Wizara hii imesimama imara, lakini watumishi wa umma wanalipwa mishahara na stahiki zao kwa sababu Wizara hii imesimama imara; tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka kuanzia kwenye hali ya fedha nchini. Na hili kwa sababu sitapata nafasi ya kuchangia kwenye Bajeti Kuu, nimeamua hivyo, sitachangia kwenye Bajeti Kuu, kwa hiyo mchoko wangu wote unaohusu Wizara ya Fedha nataka niumalizie hapahapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni suala la hali ya fedha. Taarifa inaonesha kwamba katika mzunguko wa fedha mpaka Desemba, 2022 mzunguko wa fedha ulio rasmi katika nchi yetu, fedha zinazopita kwenye benki na zinazopita kwenye mobile wallets, yaani hizi M-Fedha, Tigo Fedha na nini, ni kiasi cha shilingi 30 kati ya 100. Katika kila shilingi 100 ni shilingi 30 tu ndiyo inayoonekana kwenye benki na kwenye hizi mobile wallets. Shilingi 70 nzima iko mikononi mwa watu, haijulikani iko wapi. Nyingine inaweza ikawa iko nje, nyingine imefichwa. Waziri wa Fedha analifahamu hili vizuri. Nilitaka kujua Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Wizara yake wamejipangaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu hawakuacha fedha nyumbani bila sababu, wana sababu. Sababu ya kwanza ni hii Sheria yenu ya Anti-Money Laundering. Mtu akipeleka fedha milioni 10 tu vyombo vyote vimemtolea macho. Wameamua ya nini, wanaweka nyumbani, wanatulia wanakuwa salama kuliko kufuatwafuatwa. Namna gani ata-harmonize hii hali ili watu waweze kuleka fedha benki?
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni tozo za transactions na za kikodi zilizoko kwenye benki; mtu anaona ya nini, acha niweke fedha zangu ndani. Wafanyabiashara wameweka fedha zao ndani. Kati ya kila shilingi 100 ni shilingi 30 tu ndiyo inayoonekana kwenye vyombo vya fedha, zote nyingine hizi ziko huku.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hilo tu, kingine wanataka kuelimishwa tu, kuna ignorance katika masuala ya fedha. Wako watu kwenye minada ya mifugo wanataka wapate fedha cash, wapo watu kwenye migodi, hasa wachimbaji wadogo wanataka wapate fedha cash, kwa hiyo fedha inatembea huko mikononi; wapo watu katika kuuza mazao wanataka waone fedha cash. Tutafanya nini, tuawahamasisha namna gani watu? Maana yake hali hii si nzuri. Benki zetu nyingi sasa zimepoteza liquidity, hali ya liquidity kwenye benki imekuwa ni mbaya kiasi ambacho sasa benki nyingi zinashindwa kukopesha. Ukienda benki wanakuzungusha miezi miwili, miezi mitatu, wanashindwa kukopesha, liquidity hakuna. Fedha iko nyumbani kwa watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya nchi ukifika ukianza kushuka kwenye asilimia kama hii kadri unavyokwenda ndiyo unaitisha sasa fedha zote zirudi Benki Kuu ubadili fedha kwa sababu watu wanaficha fedha. Na hili nataka niseme, ni lazima sisi kama nchi kupitia Wizara yetu ya Fedha tufike mahali tukae na wafanyabiashara wakubwa na wa kati kuwahamasisha, kuwaeleza sasa nchi ni salama, hakuna matishio ya fedha zao ili waweze kuruhusu fedha zirudi benki. Hali si nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini unapokuwa na shilingi 30 kati ya mia ndizo inayozunguka, hata kodi za Serikali unakusanya kwenye shilingi hizi 30, kwa hiyo na Serikali nayo inapoteza. Lazima utueleze tunafanyaje kutoka hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine linahusu sera za kikodi; hili ni letu sote. Sera za kikodi zimechangia sana kuua biashara. Leo hii mmekwenda mpaka na Mheshimiwa Waziri Mkuu kutatua matatizo Kariakoo. Kariakoo imekufa kwa sera za kifedha ambazo sisi wote tunahisika, sitaki kuwatupia lawama ninyi peke yenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka sera nyingine za kulinda viwanda ambavyo havipo. Na viwanda vingine tulivyoamua kuvilinda wala vyenyewe havijilindi, vinachukua raw material asilimia 90 kutoka nje zinasema hizi zinaingia kwenye mnyorro wa thamani kumbe wanachukua majora kutoka nje wanakuja ku-print hapa. Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba sera za kikodi zemechangia sana. Leo biashara ya vitenge ilikuwa nchi zote jirani walikuwa wanakuja kuchukua vitenge Tanzania, sasa vitenge tunakwenda kuchukua Malawi, tunakwenda kuchukua Zambia kwa sababu kontena la futi 40 hapa nchini kodi yake ni milioni 378, lakini Zambia ni milioni 30, Kenya ni milioni 35.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi unafikiri ukishafika mahali ukawa na sera za kikodi za namna hiyo unachotaka ni nini? Kinachotokea ni kwamba unavutia biashara kwa wenzio unaua biashara ndani, ndiyo yale yanayotokea pale Kariakoo. Tunataka kwenda kuwakamua watu wachache wanaoingiza kidogo, inashindikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lazima niesme kwamba kwa sababu sitachangia kwenye Bajeti Kuu, nataka nilieleze hili kwamba sera zetu za kikodi ni lazima tuzitazame ili zituwezeshe kufika mahali kufanya sekta hii binafsi ambayo inaajiri watu wengi iweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nilieleze ni suala la maamuzi tunayoyafanya hapa Bungeni ikiwa ni pamoja na kupitisha bajeti. Mheshimiwa Waziri wewe unakumbuka bajeti iliyopita tulipokaa hapa umetangaza kushusha kodi inayoitwa hotel levy inayotozwa na halmashauri zetu kwa kila mpangaji anayelala kwenye guest house. Ukatoa kwenye asilimia 10 kuleta kwenye asilimia tano. Lakini nataka nikwambie zipo halmashauri nyingi mpaka sasa zinaendelea kutoza asilimia 10 na watu wanalalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuwa na Serikali ambayo huku juu wakisema chini hawatekelezi, ukiwauliza – maana sisi ni wawakilishi wa wananchi – unawauliza wanasema hayo yalisemwa huko hatuna waraka. Mimi nilifika mahali mpaka baadhi ya watendaji wa Serikali nikawauliza hivi ingekuwa imepandishwa mngesubiri waraka? Lakini kwa sababu imeshushwa mnasubiri waraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri, unapofika mahali ukatoa maelekezo hapa ya kifedha katika nchi, na wewe ndio Waziri wa Fedha, toa waraka kwenda kwenye vyombo vyote vinavyohusika kusimamia utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii najiuliza sasa wale wanaoendelea kutozwa asilimia 10 mpaka sasa Serikali itawarudishia? Na nitakuomba utakapokuwa unafanya majumuisho hapa ueleze, maana nisije nikaonekana labda mimi nasema uongo. Lakini ninachosema ni sahihi, kodi ya hotel levy ilishushwa kutoka asilimia 10 kuja asilimia tano lakini zipo halmashauri mpaka sasa zinaendelea kutoza asilimia10…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu umekwisha eeh? Naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)