Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kunipa hii nafasi na uwezo wa kusimama hapa, lakini pamoja na wewe kunipa nafasi hii kusimama hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ilikuwa nizungumze kidogo kwa rafiki yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu hapa, naona leo alikuwa yuko doro doro kwa sababu jana Yanga ilitoka draw halafu Simba kashinda saba, ndiyo maana alikuwa yuko mnyonge mnyonge, ule ndio unyonge wake. Lakini sasa mimi nataka nimtoe unyonge na ninataka achangamke kutokana na haya ambayo nayaeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye paragraph ya 36 katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameelezea pale huduma za pensheni na mafao ya watumishi ambapo kwenye randama tumekwenda kuangalia katika Fungu 23 ambayo ni Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye pensheni mimi nina hoja mbili, ya kwanza, wazee ambao walishastaafu wanapata taabu kupata pensheni zao na kupata viinua mgongo vyao, hususan wa kutoka Zanzibar. Hawa wa kutoka Zanzibar ni lazima wafunge safari waje zao Dodoma ili kuja kufwata mafao yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo wanakwenda, wanarudi mafao yale hawayapati, mwisho kinachotokea wanafanya maamuzi ya kusamehe. Kwa maana hiyo naweza nikasema kwamba Wizara ya Fedha inawadhulumu wazee wetu wastaafu wa Jamhuri ya Muungano ambao wanaishi Zanzibar kwa sababu baadaye mwisho wanaamua kusamehe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo majina hapa, na mimi mwenyewe nimeshughulikia kesi hizi moja baada ya nyingine. Kuna jina la mzee Mohamed Seif Maftaha ambaye ni marehemu, urithi wake unashughulikiwa na na Bi. Pili Ramadhani Saidi. Huyu nimekuja mpaka nimegonga mwamba, mpaka leo mafao yake hajapata, pia kuna Bi. Zuleha; hajapata; kuna Bi. Ruzuna. Hawa wote nimewaleta mimi nimewaweka hapa Dodoma, hawakupata. Tatizo liko wapi Mheshimiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, mikoa au kanda zote kuna ofisi ndogo ya Hazina, lakini kwa nini Zanzibar hamuweki ofisi ya Hazina kuondosha huu usumbufu? Ingekuwepo Ofisi ya Hazina hawa watu wangelishughulikia kulekule, ingekuwa ni rahisi. Kwa hiyo tunawatesa wazee na tunawadhulumu fedha zao. Lakini mimi naahidi hapa nitaendelea kuwafuatilia hawa wazee. Na Mheshimiwa angalia sana katika pensheni, angalia sana katika sehemu hiyo, watu wanadhulumiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili kwa Mhasibu Mkuu; tulitembelewa hapa na Jumuiya ya Wazee Wastaafu. Jumuiya hii wana malalamiko mengi, yanafika hata 30, lakini kubwa wanalosema ni kwamba pensheni zao wanalipwa siyo kwa mujibu wa sheria, sheria haifuatwi, Sheria ya PSSF haifuatwi, na ile nyongeza iliyotoka Hazina nayo pia haifatwi. Kwa maana hiyo wazee wanadhulumika. Ombi lao wanasema Mheshimiwa Waziri uunde task force uwasikilize malalamiko yao; usipounda task force hawa wazee nao wataendelea kudhulumiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina mfano mmoja. Kuna mzee mmoja alisema analipwa pensheni ndogo, tukazungumza na maafisa wako, siku ya pili alipewa pensheni anayostahili na akapewa malimbikizo yake. Sasa wazee kama hawa wako wengi. Kwa hiyo tunaomba hawa wazee uwashughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Fungu Na. 10; kwa mujibu wa Katiba fungu hili linasimamia uhusiano wa kifedha. Uhusiano huu wa kifedha hapa nimekusudia kuzungumzia mikopo ya nje. Mikopo ya nje ambayo inaingia katika nchi hii inastahili kwamba Zanzibar mgao wake ni 4.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanya tafiti kupitia taasisi hizi zifuatazo; Wizara ya Fedha yenyewe, IMF, World Bank, African Development Bank, Tanzania Coalition on Debt and Development (TCDD) na taasisi nyingine. Nimegundua kwamba hata asilimia mbili Zanzibar katika ile mikopo ya kutoka nje hapati. Na mikopo ya nje ni suala la Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ukitaka kujua kwamba ni suala la Muungano, akikorofisha Zanzibar mkopo unazuiliwa. Kulikuwa kuna mkopo hapa wa NCC ambao ulikuwa unakuja kwenye REA lakini ilivyotokea vurugu kule Zanzibar mkopo huu ulizuiliwa kwa sababu mkopo ni Muungano. Sasa hii asilimia nne utakaposimama Mheshimiwa Waziri, ninaomba utupe majibu ya kutosha hii asilimia nne ipatikane.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, nimefanya utafii kupitia IMF sasa hivi ni kigezo kipi kinatumika katika kupata mikopo Zanzibar. Nimeona document ya Tanzania kwenye IMF kwamba mnatumia financing gap ili ku-finance au kupata mikopo ya nje. Finance gap ya mwaka 2021/22 ilikuwa 866. Sasa je, tunatumia financing gap, hiyo financing gap mnachukua na financing gap ya Zanzibar au mishatumia hiyo financing gap, kwamba mnatafuta 4.5, na hapa tutazame. Hiki kigezo kimewekwa tangu mwaka 1994 wakati wa mzee Malecela katika tume yake, sasa je, bado ni valid ibakie hiyohiyo 4.5? Na sasa hivi kuna variables nyingi sana zimebadilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dk.t. Mwigulu, atakapokuja hapa nataka anipe ufafanuzi katika suala hili la 4.5 katika mambo mawili, je, ilikuwa ikilipwa kwa mikopo yote? Kwa sababu kuna mikopo ya basket fund tunajua haziwezi kuhusika. Lakini cha pili, je, hii rate ya 4.5 ni valid? Mbona mkienda IMF mnatumia financing gap. Ninataka uje utupe ufafanuzi, kama hatukupata ufafanuzi sisi Wabunge ambao tunatoka upande wa pili kule hatuwezi kuomba maji hapa, hatuwezi kuomba elimu hapa, hatuwezi kuomba afya, tunashughulikia huu uhusiano. Kwa hiyo uje utuambie uhusiano huu ukoje na nini kinapatikana katika uhusiano huu, kipi kilistahili kupatikana katika uhisiano huu; lakini je, bado factor hii ipo, na mnatumia sasa variables nyingine kwenda kukopea. Sasa tunataka Mheshimiwa uje utupe ufafanuzi, kama sitaridhishwa na majawabu yako nimekusudia nikamate shilingi. Nitakamata shilingi ili tupate ufafanuzi kwa sababu hakuna uwazi katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mikopo inatoka World Bank ilikuwa inashughulikia masuala ya utoaji wa haki, zikajengwa mahakama Tanzania nzima. Lakini mkopo ule wa World Bank kule Zanzibar haukufika. Kuna mikopo ilikuwa ikishughulikia kutatua msongamano katika miji mikuu, msongamano ule tukajenga madaraja maeneo chungu nzima, mkopo ule kule Zanzibar haukwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika hii REA tunayozungumzia, portion ya REA tunatoa fedha ambazo nyingine unachangia kutokana na tozo ya mafuta, lakini nyingine tunachangia kutokana na mkopo. Sasa huu mkopo unatoka nje na haukuja kwenye basiā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili hiyo.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaunga mkono hoja endapo nitapata ufafanuzi, vinginevyo nitashikilia shilingi. Nashukuru.