Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu, Wizara ya Fedha. Mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati yetu ya Bjeti, Kamati ambayo ina dhamana ya kuisimamia Wizara hii ya Fedha. Kwenye majukumu yetu pamoja na maeneo mengine tunasimamia Mafungu mbalimbali kwenye Wizara hii likiwemo Fungu la Hazina, Huduma za Mfuko wa Jamii, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Msajili wa Hazina, Deni la Serikali, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu, Tume ya Pamoja ya Fedha na Wizara ya Fedha yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo nataka nizungumzie Fungu moja katika haya. Fungu namba sita, Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali. Bajeti zetu hizi ambazo tumekuwa tukizijadili hapa mara tu baada ya kuzipitisha, Serikali inakwenda kutekeleza bajeti hizi na kule zinakokwenda jicho letu pekee ambalo tunalitegemea ni Wakaguzi Wakuu wa Ndani kwenye Halmashauri zetu lakini na kwenye Taasisi mbalimbali za Serikali zinazopokea fedha kutoka kwenye bajeti hii tunayopitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana 2022/2023 kwa maana ya mwaka huu wa fedha unaokwisha. Fungu hili Na.6 kwa maana ya Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali tulimpa fedha bilioni saba, milioni mia nane na themanini na tisa, laki moja na themanini na nne na mwaka huu tumempitishia bilioni tisa, imeongezeka kidogo na tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha Fungu hili kwa kuliongezea fedha ili likafanye kazi zake za ukaguzi. Tumewapa bilioni tisa, milioni mia tisa ishirini na saba na elfu nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tukafanye mapinduzi kwenye Idara hii ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali ili jicho letu kwenye fedha za umma likaongezeke. Lazima tuifanyie mapinduzi idara hii ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali. Mapinduzi ya kwanza ambayo tunatakiwa tuyafanye ni ya kimuundo, lazima tubadilishe muundo. Nitatolea mfano, Wakaguzi wetu ambao wako kwenye halmashauri zetu wakishafanya ukaguzi wao, wakamwandikia Mkurugenzi, akajibu na Wakuu wake wa Idara, wakapeleka kwenye Kamati ya Ukaguzi na wakapeleka kwenye Kamati yao ya Fedha, ripoti yao moja kwa moja wakiiandika inakwenda straight kwa Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba ukichukua ripoti zote za nchi nzima zikapelekwa moja kwa moja kwa mtu mmoja pamoja na kwamba ni taasisi, hawezi kuwa na uwezo wa kuyachakata yote na kutupa majibu. Hawezi kuwa na uwezo wa kuyachakata yote na kuchukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachopendekeza na ninachoshauri hapa huu muundo lazima tuubadilishe. Lazima tuwe na Mkaguzi Mkuu wa Ndani ngazi ya Mkoa ili sasa wale wa Wilaya wakishachakata taarifa zao na kuziandikia, taarifa ikatue pale Mkoani. Ukishakuwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani kwenye kila Mkoa, definitely itakulazimisha kuwa na ofisi za kanda. Kwa hiyo wa Mkoa atazichakata za Mkoa mzima halafu ata-submit kwenye kanda yake halafu wale wa kanda ndio wapeleke kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali. Kwa kufanya hivyo…
MHE.ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
TAARIFA
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, mzungumzaji anaendelea kuchangia vizuri sana. Nataka nimpe tu taarifa hapo anapopaona kwamba patengenezwe au pawe na Wahasibu Wakuu, Wakaguzi Wakuu wa Ndani wa Mikoa. Nataka nimpe taarifa hawa wapo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ni Makatibu Tawala Wasaidizi, Ukaguzi wa Ndani wa Mkoa, lakini hawana kazi hiyo. Wana kazi ya kukagua wilayani na Ofisi ya RAS tu, kwa hiyo wapo hao. Wapewe majukumu ya kwenda kusaidia watendaji hao wa halmashauri kwenye ukaguzi.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ruben taarifa hiyo?
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa. Ninachokisema hapa, nataka tufanye marekebisho kidogo yule Chief Internal Auditor kwenye Ofisi ya Mkoa, aendelee kubaki pale kwa sababu kila Afisa Masuhuli lazima awe na Internal Auditor, yeye abaki pale afanye mambo yake hayo ya kumwangalia RAS, afanye mambo ya kumwangalia DAS. Sisi tunamtaka Mkaguzi wa Ndani Mkuu Mkoani ajitegemee kabisa separate na yule wa pale kwa RAS.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kwamba, yeye a-consolidate zile zote za wilaya zote ndani ya Mkoa na kuzichakata na kwa muundo huo tukishakuwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani kila Mkoa, definitely itatupeleka kwenye ofisi za kanda ambazo nazo zitachakata, halafu ndio zimpelekee sasa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali. Tukifanya hivyo tuna-ensure mambo mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwenye ukaguzi kinacho matter ni ubora wa taarifa. Tukifanya hivyo tutakuwa tumepata quality assurance lakini tutakuwa tumepata quality control, lakini sivyo hivyo tutakuwa tumeifanya kazi ya Mkaguzi Mkuu, CAG yule kazi yake itakuwa ni rahisi sana anapopita na kazi yake ikiwa rahisi itakuwa accurate, lakini wakati huo huo fedha zetu za wananchi tutakuwa tumezilinda. CAG akishakuwa na kazi ndogo tutataka sasa Serikali imwongezee fedha nyingi ili yeye awe anafanya real time audit. Tukifanya hivyo tutakuwa tumefanikiwa kuzuia majambazi yote yaliyopo ndani ya mfumo wa Serikali ambayo yanaiba fedha zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa tumefanikiwa kuzuia watu wote ambao sio waaminifu ambao wanaiba fedha zetu na kwa maana hiyo taarifa ya CAG itakuwa inakuja ikiwa safi na fedha za wananchi zikiwa salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, utoaji wa taarifa wa Wakaguzi wetu wa Ndani; moja ya eneo ambalo lazima tulifanyie maboresho, kwamba Mkaguzi wa Ndani mathalani Halmashauri ya Handeni Mjini anaandaa taarifa yake halafu anaipeleka moja kwa moja kule kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu. Taarifa yake anaipeleka moja kwa moja halafu Mkaguzi Mkuu yuko chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha. Kwenye ukaguzi huu tunapokagua kuanzia kwa Wakaguzi wa Ndani tunamkagua na huyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha. Haiwezekani wewe uwe unajikagua mwenyewe, unajiletea mwenyewe halafu taarifa unakaa nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kuna tabia ya watu wakipelekewa hizi taarifa za ukaguzi wanazipiga polish wanazing’arishang’arisha hivi, zinawafurahisha furahisha halafu wanakaa nazo. Haitakiwi kuwa hivyo, tunachotaka, taarifa ikitoka kwa Internal Audit wetu wa halmashauri, iende kwa yule Internal Auditor wa Mkoa. Ikitoka kwa yule wa mkoa, iende kwenye kanda, halafu iende kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Pay Master General yeye apewe taarifa tu, kwa sababu ndiye anayekaguliwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanye hayo mapinduzi, wasipofanya haya tutaamini kwamba wana nia ovu ya kuendelea kufuja fedha za Watanzania. Taarifa zote za kikaguzi na taarifa mbalimbali za wachambuzi wa mambo ya kikodi, ya kikaguzi, ya fedha za wananchi, zimekuwa zikionesha kwamba tumekuwa tukipoteza trilioni nne mpaka tano kila mwaka kwa kuibiwa kwa sababu ya mifumo kama hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mapinduzi ya pili ambayo nataka tuyafanye, ni kuwawezesha wakaguzi kuwa conversant kuijua mifumo inayotumika kwenye taasisi zetu. Mifumo kama vile GePG, mifumo kama vile PlanRep, MUSE, ule unaotumika kwenye afya TANePS na sasa tunaubadilisha kuwa NeST na ule wa TAUSI na mifumo mingine mingi ambayo inatumika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Reuben, mfumo wa time uko tayari. (Kicheko)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)