Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya, niwapongeze pia Watendaji wote wa Wizara na taasisi zote zilizoko chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, wanafanya kazi vizuri na sisi sote tunaona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya Wizara ya Fedha ni kubwa na wao wenyewe wameidadavua katika ripoti yao katika taarifa ambayo wamewasilisha ni nyingi na ni kubwa na wanafanya vizuri, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo kama mawili au matatu ambayo nitajaribu kuzungumzia kwa kifupi. Jambo la kwanza nataka nianzie kwenye eneo la bima. Bima, kuna bima ya lazima na kuna bima za hiyari. Hasa kwenye eneo la bima hapa, katika nchi yetu yapo magari ya Serikali hayana bima, yapo majengo ya Serikali hayana bima, yapo majengo ya kibiashara hayana bima, matokeo yake ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ajali nyingi zinazotokea barabarani nyingine nyingi zinasababishwa na madereva wanaoendesha magari ya Serikali. Sasa matokeo yake magari yale yanawagonga watu, yanagonga mali za watu binafsi, yanasababisha hasara kubwa. Kwa utaratibu wa nchi zote gari ikikugonga au ikagonga mali au ikaleta hasara yoyote, yule anayepata hasara anatakiwa afidiwe na bima. Kwa utaratibu wa sasa hivi wa magari ya Serikali ambayo hayana bima maana yake nini? Wale wanaogongwa wanapata hasara hawana mahali pakujitetea wala pakuomba fidia. Sasa hili siyo zuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Serikali zetu mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar. Zanzibar wameliona na wamerekebisha sheria, magari yao yote ya Serikali yanalipa bima ya lazima ili yakisababisha hasara watu waweze kufidiwa. Tanzania Bara bado, sisi huku bado. Nadhani umefika wakati tuangalie hili, watu wanaathirika, watu wanaumia, watu wanapata majanga mengi na hakuna fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tumeshuhudia kwenye jengo la kibiashara la hifadhi ya jamii pale Dar es Salaam, lift imedondoka na watu wamekwenda mpaka chini wameumia, hawana mahali pa kuomba fidia! Sasa hili lazima Wizara ilitazame na ione kwamba kuna haja ya kuja na mfumo wa kuhakikisha kwamba magari yote ya Serikali, majengo ya kibiashara na mengine yote yaweze kupata bima ya lazima ili kujikinga na majanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana Mheshimiwa Waziri ulifanya kazi nzuri na tulikupongeza kabisa. Mwaka jana katika Bunge hili, aya ya 113 kwenye Sheria ya Bima Sura 394 ulisema hivi: “Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Bima kwa kuongeza wigo wa bima ya lazima (mandatory insurance) kwa kujumuisha masoko ya umma, majengo ya biashara, bidhaa zote zinazoingizwa kutoka nje, vyombo vya baharini na vivuko. Hatua hii ina malengo ya kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha (financial inclusion) na kuleta matumizi sawia ya bima”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili ulileta zuri tukakupongeza Mheshimiwa Waziri, toka Financial Bill ile imepitishwa mwaka jana mpaka leo hii hamjaanza kuifanyia kazi, Kanuni bado hazijatoka kwa nini? Sasa kazi tuliyoifanya mwaka jana mpaka sasa hivi bado hamjaleta Kanuni! Sasa Kanuni hizi tungependa Mheshimiwa Waziri mzilete mzifanyie kazi. Mwaka umemalizika maana yake hii Sheria haijaanza kufanya hii kazi, kwa hiyo, ni vizuri mkaifanyia kazi, ikaanza kufanyakazi ili sasa ndiyo pale nasema tuongeze magari yote ya umma yanayosababisha ajali barabarani yawe na bima ya lazima ili nayo hiyo sasa wananchi waweze kunufaika, ile hasara wanayoipata waweze kufidiwa. Kwa hiyo, hili ni suala ambalo mimi nimeona ni la msingi sana na ni muhimu mkalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ningependa Wizara ya Fedha mlifanyie kazi, ni kuiangalia upya Sheria ya Fedha za Umma Sura 348. Sheria ile Mheshimiwa Waziri ilitungwa mwaka 2011 na kuna marekebisho kadhaa yamefanyika mpaka mwaka 2020. Marekebisho yale yote ukiyaangalia Sheria ile inasema, lengo la Sheria ni kuleta usimamizi mzuri wa makusanyo na matumizi ya fedha za umma na kulipa Bunge madaraka ya kusimamia fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, sasa tulipofika sasa hivi ukiitafsiri maana ya ile ni kwamba inazungumzia cash budget, inazungumzia fedha taslim. Sasa, sasa hivi uwanja mpana tunaouzungumzia kwenye usimamizi wa fedha za umma, tunazungumzia kwa mapana (financial management) siyo cash financial management. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, financial management ni zaidi ya hii sheria hii inavyosema. Financial management kwangu mimi ninavyoona Sheria hii sasa tuiongezee meno, tuiongezee upana, tuitazame upya ili sasa financial management iwe ndiyo msingi wa hii sheria ambayo tunaizungumzia ya mwaka 2001. Maana yake sasa miaka 23 imeshapitwa na wakati ni wazi mambo mengi yamebadilika. Kwa hiyo, sheria hiyo inatakiwa iangalie uandaaji na usimamizi wa bajeti ya nchi, hii sheria inatakiwa iseme. Pia sheria hii inatakiwa iseme usimamizi wa mapato na matumizi ambayo ndiyo inasema sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii inatakiwa inagalie mipango ya kodi mbalimbali na usimamizi wa mali zake, hii sheria lazima iseme. Sheria hii inatakiwa pia kubainisha na kuangalia namna tutakavyoitumia katika kudhibiti hali ya baadae (forecasting) tuta–forecast mambo mbalimbali yanayojitokeza kwenye dunia. Mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza hii sheria inatakiwa iwe ndiyo msingi wa kuweza ku – forecast kuangalia nini tunatakiwa kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo kutafuta vyanzo vipya vya mapato, sheria inatakiwa ituoneshe, zaidi ya hapo kufanya maamuzi ya ushirikiano yaani kuangalia kama major na acquisition na mambo mengine mengi kama kuangalia madeni ya Taifa na mali za Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja lakini naamini Mheshimiwa Waziri ataenda kuiangalia hii sheria ili iwe ya muhimu zaidi, ahsante sana, nashukuru sana. (Makofi)