Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri pia nimesoma maoni na mapendekezo ya Kamati, ninakubaliana na maoni na mapendekezo ya Kamati kwa vitu walivyoshauri namna bora ambavyo tunaweza tukaboresha mfumo wetu especially wa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia eneo moja tu na ni kwa wema sana, kwa sababu mimi naamini namna bora ambazo tunaweza tukafanya kusaidia nchi yetu ni pamoja na kujengea uwezo Wizara hii, kwa sababu Wizara hii kila Wizara nyingine zote tukilia hakuna barabara, tukilia hakuna maji, tukilia kuna shida hatuna madawati, hatuna madarasa, bado tutanyooshea mikono, tutawanyooshea vidole Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami siamini kama kweli Serikali haina mapenzi na wananchi wake, siamini kabisa. Kwa hiyo, ninaamini sana Wizara hii pamoja na Serikali lengo lake ni kuhakikisha kwamba wanajenga uwezo wa Watanzania kukusanya kodi wenyewe, ili baadaye wakitaka kuzitumia wazitumie kwa kuona maendeleo ambayo walikusanya kodi leo barabara inapitika, mimi naamini hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na makandokando yote lakini kama Wizara ya Fedha kwenye kitengo cha kukusanya kodi, itakusanya kodi kama inavyostahili sidhani kama kaka yangu Mwigulu kama ambavyo muda wote amekuwa akisimama humu akiambiwa sasa peleka pesa, peleka pesa sidhani kama wanazo fedha halafu hawataki kupeleka, siamini kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitazungumzia mwenendo wa ukusanyaji wa kodi na upotevu wa mapato kwenye Taifa letu. Kwanza hazijabadilika sana, takwimu hazijabadilika sana za wanaolipa kodi mpaka sasa hivi tunavyozungumza hazijabadilika sana, bado range haijafika milioni tano, yaani hapo haizidi hapo kama imezidi haizidi hapo. Kwa hiyo bado tuna tax base ndogo mno ambayo tunalazimika kuwaminya wachache ambao ndiyo tunaowahesabu kama ndiyo walipa kodi. Kwa hiyo, bado hoja yangu ya kuongeza tax payers, kuongeza tax base idadi ya walipa kodi kwenye nchini kwetu ni hoja ambayo nitaendelea kuizungumza, kwa sababu naamini tukilipa kodi wengi tutakuwa tunaminyana kidogo kwa sababu tuko wengi tunachangia, tofauti na mkiwa na walipakodi wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna nchi nyingine jirani na tukisema tunataja majirani siyo kwa sababu kwetu hatuthamini, tunajaribu kwa sababu kama tuko kwenye uwanda mmoja, kama tuko African Community pamoja, ninaamini tunajifunza humu kwa sababu kuna agreements nyingi tunaingia vikao pamoja mpaka miaka ya fedha tumeirudisha nyuma, wote wameirudisha nyuma nchi zao, tumekuwa pamoja tunamaliza Juni 30, Mwaka wa Fedha unaanza tarehe 01 Julai, East Africa yote, ndiyo maana tunasema kama ni mifano ambayo haihusiani na Malaysia huko na wapi, basi ya humu pia tuisikie kwa sababu ni East African community.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nchi kama Kenya ambayo tax base yao ni angalau ni watu milioni saba wanalipa kodi plus, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, amezungumza pia hata namna ambavyo GDP Kenya, Rwanda mchango wa mapato ya kodi kwenye GDP sisi ni asilimia 11, natamani sasa tuone namna gani tunaweza tukaboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma taarifa ya Wizara ukurasa wa tano ambayo ameeleza mwenyewe Mheshimiwa Waziri, miongoni mwa vipaumbele vyake, Mwaka wa Fedha uliopita na Mwaka wa Fedha huu ni kukusanya, kudhibiti upotevu wa kodi na kuhakikisha kwamba wanadhibiti matumizi bora ya fedha za umma, which is nzuri sana, lakini ukienda kwenye mikakati yake kwenye kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali anasema kufanya doria kwenye mipaka, lakini pia kidhibiti mifumo ya TEHAMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shida yangu iko hapo kwenye Mifumo ya Tehama, kwa sababu kama tunazungumza digital economy na hatuzungumzi namna bora ya kudhibiti upotevu wa fedha; kwa sababu takwimu zilizotajwa na Viongozi wa Serikali ni kwamba tunapoteza shilingi milioni 500 mpaka shilingi bilioni moja kwa siku kwenye mifumo ya Tehama. Nataka niwaambie hizo ni takwimu zilizotajwa na Serikali. Nawapa benefit of doubt, lakini tukienda into details, ni zaidi ya hizo fedha tunazopoteza kwenye mifumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuko tayari kuwasaidia Serikali. Kama kweli hatuna resources, tuna vyuo, tume-train vijana wetu, wana uwezo, wana elimu kubwa ya cyber security, tumeshindwa kutumia investments zetu za shule, tumeshindwa kusomesha vijana kwenye vyuo ambavyo tunaweza kusema tunaviamini ili wazuie upotevu wa fedha, tuko tayari. Mimi nipo tayari kusaidiana na Waziri tukutafutie wataalam the best, na ni Watanzania. Wengine wamechukuliwa na nchi nyingine kwenda kusaidia kudhibiti upotevu wa fedha. Sisi tunao watu wetu ambao ukiongea nao wanakwambia wewe Mchaga gani hupendi hela? Watu wana mipango yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana, probably kuna possibility kubwa sana ya kwamba wanaopiga hizo pesa ni watu wa kwenye mifumo huko huko. Ndiyo maana hawatafuti suluhisho la kudumu la kuzuia upotevu wa fedha. Watanzania sio wapuuzi kwenda kuweka fedha zao kwenye mifuko ya rambo nyumbani kwao. Siyo kwamba hawapendi nchi yao, hawataki kulipa kodi ndiyo maana wanapeleka huko, usalama wa fedha zao ni changamoto. Tunaweza tukatumia fedha ndogo sana kutengeneza mfumo ambao utatusaidia kuwa na strong cyber security ili kuwe na uhakika wa fedha za watu wetu, ziwe na usalama wa kueleweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na Wizara nzima waangalie how best tunaweza tukatumia teknolojia, tukatumia investment zetu zote na resources zetu zote kuweka mfumo wa udhibiti wa upotevu wa mapato ya kidigitali. Sasa hivi dunia haizungumzi mapato, magendo eti mpakani yaani mpaka naona vibaya kwamba kwa nini nipo kwenye…, kwa sababu naona kama tunazungumza miaka ya 1980 huko. Kwa nini hivi vitu bado vipo? Siyo sawa. Naona kama tunafikiri kurudi nyuma, badala ya kufikiri kwenda mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, tangu Bunge la Kumi, Bunge la Kumi na Moja, Bunge la Kumi na Mbili tunazungumza hivi hivi kwamba mifumo haioani, yaani mifumo haisomani, na tuna kitengo cha teknolojia. Eti hatuna kompyuta, hatuna laptop. Yaani bado tunazungumza hivi vitu hii nchi! Mimi nafikiri siyo sawa. Ifike hatua sasa habari ya mifumo haioani iishe. Kwa sababu mimi naamini kwamba hivi vitu ni vidogo vidogo ambavyo mnaweza mka-deal navyo kwenye Wizara huko huko. Kwa sababu kama una Wizara nzima ina-deal na masuala ya teknolojia, kwa nini bado unahangaika eti mifumo haioani? Sioni kama ni sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro mingine kama ya Kariakoo ambayo inajitokeza pale, ni vitu ambavyo mimi naamini, kaka yangu wewe Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Waziri wa Fedha, hivi vitu unaweza kuvi-clear kabisa. Watu wataona hawaumii sana kama wanalipa kodi wengi. Ningekushauri, natamani kuiona Tanzania ambayo hatutumii fedha tena, yaani tumeenda cashless kabisa, kwa sababu ndiyo dunia inapoenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza nikakushauri kwamba ukitangaza leo unabadilisha fedha, utaona fedha zitakakotoka kuja BOT. Kwa sababu unahitaji kuwekeza kwenye kuwapa watu elimu waone hawapigwi, yaani hawapigwi. Ndiyo dunia inavyotaka twende. Halafu jipe time, wekeza kwenye kuelimisha watu. Kwa sababu Watanzania wanatamani tuongee hivi taratibu, yaani kwa sauti ndogo tu kwamba ni wajibu wa kila Mtanzania kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hawaelewi, tutumeni sisi wengine. Mimi nitajitolea hata kwenda kuwa Balozi. Jamani, usipolipa kodi barabara haipitiki, hatutapita. Tukisema hakuna madarasa, maana yake tunategemea tulipe kodi sisi. Bila hivyo, tutaendelea kwenda kuomba huko misaada huko nje na kila siku tunalalamika deni la Taifa linakua, lakini tukilipa kodi wenyewe, tunachagua wenyewe cha kufanya.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.