Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Bajeti ya Wizara ya Fedha. Nami namshukuru Mheshimiwa Rais, Waziri wa Fedha na timu yake nzima kwa kuleta bajeti kwa ajili ya Wizara yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza Mheshimiwa Kilumbe hapa akiongea suala la dola na pia kulikuwa na swali asubuhi. Sisi kwetu kwenye majimbo yetu ndipo yalipo masoko ya dhahabu. Soko langu la dhahabu kwenye Mji wa Kahama, kutoka benki zilipo ni mita 50. Sasa najaribu kujiuliza, hivi kweli unaweza kuwa una soko la dhahabu inayochimbwa na wenyeji na ukasema tena hauna dola kwenye mita hizo hizo? Inatupa wakati mgumu sana wa kufikiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Mtemi Mirambo wakati Waarabu wanakwenda kuchukua pembe, wakija na pembe kumi, alikuwa anachukua mbili. Wakitoka huko na bunduki, anachukua bunduki mbili na yeye, badaye wanabadilishana. Sasa wewe unachukua dhahabu, unai-charge shilingi. Milambo alikuwa anachukua pembe kumi. Kwa nini usikate hata kipande cha dhahabu ukapata dola? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tulie kabisa kwamba hatuna dola? Soko la Geita linaongoza leo kwa dhahabu, lakini dhahabu ni dola. Kuna tofauti gani wewe unanunua ndege, inafuata watalii China, inawaleta mpaka Ngorongoro, wanakuja unawatengenezea na chakula, ndiyo wanakupa dola, lakini unakataa dola inayochimbwa kama mihogo kuja nyumbani kwako, unakataa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Mheshimiwa Waziri alifikirie kwa mapana sana. Maana yake kwa muda tunao-delay inaweza ikatuweka kwenye matatizo makubwa, maana watu wanapata riba wakati wanasubiri dola. Pale kwangu Kahama mimi mwenyewe nimetafuta Dola 1,000 nimeshindwa kupata, lakini opposite yake kuna tani za dhahabu. Tuombe tu wenzetu wa Wizara ya Fedha waondoe huo uoga. Wanaogopa nini? Huwezi kuwa na dhahabu ukasema huna dola, haiwezekani. Kwa kweli ni kitu ambacho kinatuhuzunisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala hili la share. Share, ni Wazungu walikaa miaka 100 iliyopita kule Ulaya wakatengeneza huo utaratibu. Utaratibu huo ulivyo sasa hivi, kuna migogoro mingi sana. Nitatoa mfano. Shirika la Ndege la Precision watu wamenunua share, watu wamenunua share hata za Voda, za Tanzania Oxygen, lakini mpaka leo hakuna pa kuuza hata kama unaumwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndege ya Precision inakwenda Mwanza, ina nafasi kumi ambazo hazina watu. Kwa nini mimi mwenye share siruhusiwi kukata against share kwenye ile tiketi ili wakakata kwenye ile share? Kama wewe unasema kwamba mali hii ni ya kwangu, unakataaje? Mimi nina share kwako, kwani mimi nikinunua ng’ombe kwako, si zinagongwa tu mhuri kwamba hizi ni za fulani, akija saa yoyote mpatie. Haiwezekani! Maana yake mtu amenunua share. Leo Voda anachenga hapa wakati alichukua hela za watu, sasa kama hawezi kuuza share, si tukate kwenye vocha? Awe anatukata kwenye vocha, yeye anachukua zile share? Ni kama vile tulimkopesha. Hilo nafikiri, pamoja na kwamba inaonekana utaratibu ni mgumu, lakini wenzetu lazima walifikirie.
Mheshimiwa Naibu Spika, pana suala gumu sana hapa, Mheshimiwa Dkt. Kimei anafahamu. Sisi na Mheshimiwa Dkt. Kimei tumeteuliwa kwenye Kamati ya kuanzisha Benki ya Wachimbaji, lakini kuna mgogoro ndani ya hili suala. Kule Mwanza tulianzisha Mwanza Community Bank, ikatayarishwa vizuri na tukachanga zaidi ya Shilingi bilioni mbili na kitu, lakini ilivyokuja Sheria ya Benki Kuu, inasema wewe kama huna elimu au hukusoma elimu hii ya fedha huruhusiwi kuwa Body of Directors kwenye ile benki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nimekusanya Shilingi milioni 500, halafu nimetoa kwenye benki kama nanunua share, naambiwa siruhusiwi kuwa kwenye Body of Directors. Sasa kwani kupata Shilingi milioni 500, kwa nini usiandike hizo CV zangu kwamba aliuza miwa, mihogo akauza hiki, akapata Shilingi milioni 500! Kwa nini usii-convert hiyo ikawa ni degree au elimu, ukaniruhusu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikupe Shilingi milioni 500, wewe uje na tai na cheti cha degree, nikukabidhi fedha zangu, itawezekana kweli! Tukajitoa na Simiyu Community Bank na yenyewe hivyo hivyo wote tukajitoa, tukasema haiwezekani, lazima mbadilishe, mturuhusu tusimamie fedha zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo najaribu kumwuliza Mheshimiwa Waziri, tutafanya nini kwenye hii benki ya wachimbaji? Mtawapata wachimbaji wenye degree! Mmeshawaambia au mtazua mgogoro tena! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wameshachanga zaidi ya bilioni mbili juzi Arusha lakini mmeshawaambia kwamba sheria ya kuwemo kuja kuchunga hela zako lazima uwe na cheti cha degree ni sahihi kuchunga hela zako. Haiwezekani lazima wenzetu wa Benki Kuu waangalie kabisa, mbona nyie benki zenu ambazo zinaangaliwa na wasomi si nazo zinaongoza kwa ku-collapse, hazi collapse za wasomi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimeweza ku-raise hela sasa hawa wachimbaji wame-raise hela za Mheshimiwa Doto, wame-raise hela zao, halafu wewe hela ziko tayari unaniambia hauruhusiwi kukanyaga humu, sisi tutakuwa tunakula nyie mnatitizama kule, itawezekana kweli? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamuomba Mheshimiwa Waziri na Gavana walifikirie kwa mapana sana ili waruhusu watu waingie wenye hela zao, kwenye board of directors kwenda kuchunga pesa zao. Kwa hiyo, nitakuwa na hela kweli Mheshimiwa Lusinde nishindwe kusaini kujua kwamba huyu ni mwizi na huyu ni mtapeli hatarudisha hela, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, narudia tu kumpongeza Mheshimiwa Waziri nashukuru sana naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)