Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi kuchangia katika mjadala huu. Awali ya yote naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi ambaye ametuwezesha kubakia hapa leo na kujadili bajeti ya Mapato ya Wizara ya Fedha na Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuwepo katika Wizara hii ya Fedha na Mipango. Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana wote sisi hapa ni mashahidi. Uwezo wake mkubwa sana wa kutafsiri sera kutoka kwenye makaratasi na kuja kwenye vitendo. Wote ni mashahidi na mwenye macho haambiwi tazama. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na tuna muomba Mheshimiwa Rais aendelee kuchapa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya maneno ambayo baadhi labda yanaweza kutokea tokea na watu kukosoa kosoa basi ndiyo ada ya binadamu kusema. Hata wahenga husema, “Mwenda hidimani ndiye mkosa.” Unapokuwa unafanya kazi vizuri basi lazima kutatokea maelekezo kwa nia safi tu na kukosoa kosoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mfano wa hili pengine labda inawezekana wengine nimewaacha kwamba mwenda hidimani ndiye mkosa ni pale kwa mfano upande wa michezo anaweza kusema hapa Mheshimiwa Waziri kwamba pale Mayele bora angepiga shuti badala ya kutoa pasi, lakini kwa kuwa amefanya kazi nzuri ndiyo amepata kukosoa lile. Lakini mwingine anaweza kusema Chama alikuwa asitoe pasi badala yake apige. Kwa hiyo ndiyo mwenda hidimani ndiye mkosa. Tuendelee kufanya kazi na ninaamini kabisa mafanikio ya kazi hii itapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwapongeze sana na kuwashukuru sana Kamati ya Bajeti, kuanzia Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, ninawapongeza sana na ninawashukuru sana. Kamati ya Bajeti wanafanya kazi nzuri na kubwa sana ya kiuzalendo. Na kwa ushahidi wa hilo Kamati ya Bajeti inakosa hata muda wa kailula, muda wote wao wapo kazini ni kwa sababu ya uzalendo wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa namna wanavyotupa ushirikiano mkubwa sana. Lakini si kwa umuhimu, naomba nimpongeze sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kwa kiasi kikubwa anatupa maelekezo na kunishauri vizuri. Ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niende kwenye hoja kwa maslahi ya muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na hoja ya Mheshimiwa Kilumbe. Mheshimiwa Kilumbe amezungumzia kwamba asilimia 70 ya fedha zilizopo Tanzania ziko mikononi kwa watu na haziko katika mifumo rasmi ya kifedha zikiwemo benki na ametoa pendekezo kabisa kwamba kwa kuwa suala hili lipo basi Wizara ya Fedha ichukue majukumu au jukumu lake la kutoa elimu. Ninacho mhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Fedha inatoa elimu siku hadi siku kupitia vyombo vya habari vyote nchini lakini hata kwa mtu mmoja mmoja. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kuchukua fursa hii ya kutoa taaluma kwa wananchi wetu kuwahimiza na kuwashajiisha waweke fedha zao katika mikono salama ambazo ni benki zetu na mifumo rasmi ya kifedha au ya sekta ya fedha ambazo zipo. Huko kwenye benki zetu kuweka fedha ni salama zaidi kuliko kuziweka kwenye nyumba zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nijielekeze kwenye hoja ya ndugu yangu kaka yangu Mheshimiwa Hassan King. Hoja ya kwanza mahususi amesema kwamba watumishi wazee wetu ambao wamestaafu kwa bahati mbaya sana wanachelewa kupewa fedha yao ambayo ni haki yao ya msingi. Mimi nimhakikishie Mheshimiwa kwamba suala hili tumelichukua na tunaenda kulifanyia kazi. Lakini nimuombe tu ile hoja mahususi ya watu mahususi ambao amewataja pale naomba tukimaliza tu hii bajeti basi tuonane anikabidhi yale majina. Nimhakikishie kabisa, mimi niko na Mheshimiwa Waziri, tutayafanyia kazi haraka iwezekanavyo. Kwa sababu amenitisha kidogo ametumia msamiati mkubwa sana kwamba wazee hawa wanadhulumiwa. Na jambo ambalo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linamkosesha raha na kumnyima usingizi ni suala la…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ahsante sana. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)