Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia tena wa kwanza, muda ukiniruhusu nitakuwa na maeneo matano.

Mheshimiwa Spika, kwanza, ni suala la msingi wa kisera; Chama cha Mapinduzi kilibadili mwelekeo wa kisera za kiuchumi na kisiasa miaka ya 1990 na mabadiliko mojawapo yaliyokuwa kwenye sera za kiuchumi ni kwamba tuliachana na sera za Serikali kuhodhi nyenzo za uchumi kama ilivyokuwa kabla.

Mheshimiwa Spika, miaka 20 ya CCM ilifanya tathimini kuhusu utekelezaji wa sera zake na mwaka huo ikatoa tafsiri ya ubinafsishaji na inasomeka hivi; “Ubinafsishaji hauna maana ya Serikali kukabidhi mali ya umma kwa watu au taasisi binafsi. Ubinafsishsji maana yake ni mambo matatu yafuatayo:-

(i) Kuanza ama kuuza baadhi ya hisa za kampuni za umma kwa wawekezaji binafsi; ama

(ii) Kuingia ubia na makampuni binafsi au watu binafsi wa ndani au nje ya nchi;

(iii) Kukodisha kampuni ya umma kwa taasisi au watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, hii ndio misingi ya sera ya ubinafsishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkutano Mkuu wa CCM wa Nne uliweka mazingatio mawili katika Sera ya Ubinafsishaji; kwanza, ni Serikali kuchagua taasisi au mtu binafsi kwa uangalifu ili awe mtu au tassisi yenye uwezo wa fedha na teknolojia, ujuzi wa biashara wa soko linalohusika na manufaa kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, Mkutano Mkuu ulielekeza kwamba mashirika na rasilimali muhimu ambao ni msingi na nyeti kwa maendeleo ya Taifa yanaendelewa kumilikiwa na dola. Mkutano Mkuu ukataja mashirika hayo na rasilimali hizo kwamba ni pamoja na Bandari, Reli, Posta na Simu na Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu hii mpaka leo TANESCO inamilikiwa na Serikali asilimia 100, ni kwa sababu hii Reli inamilikwa na Serikali, ni kwa sababu hii Bandari, Posta na Simu kwa maana ya TTCL inamilikiwa na Serikali. Kwa maelezo hayo azimio lililopo mezani lipo ndani ya sera za msingi za kiuchumi za CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, azimio hili lililopo mezani halihusu Bandari kuuzwa, azimio lililopo mezani linahusu uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari. Chama cha Mapinduzi kisingeruhusu Serikali yake kuingiza azimio hapo la kuuza bandari kwa sababu ni mali ya Serikali, lakini Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kamwe asingeruhusu kuingiza humu azimio ambalo linauza bandari kwa sababu ni kinyume na sera yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia Wabunge hawa walioko hapa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wala wasingepokea azimio la namna hiyo. Kwa hiyo tuwatoe wasiwasi Watanzania tunachojadili hapa kipo ndani ya misingi ya kisera za kiuchumi za CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni hofu ambayo imejitokeza; kwa unyeti wa bandari mara baada ya kusikia taarifa hizi za kubinafsisha bandari, wananchi wengi waliingia hofu na kusema kweli sisi kama Wabunge lazima tuzipokee, kuzielewa na kuzishughulikia hofu na hisia za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sisi tunafanya mambo yetu hapa na kuzingatia mambo mengine ambayo ni matakwa ya wananchi wetu. Kwa hiyo, hizo hofu ni lazima tuzishughulikie na ninaamini baada ya Bunge hili tutakuwa tumefanya kazi kubwa ya kutoa hofu za wananchi wetu kuhusu jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kimsingi tangu tuanze ubinafsishsji hakuna jambo ambalo limewahi kupokelewa bila hofu. Mtakumbuka wakati tunabinafsisha NBC kulikuwa na hofu kubwa na mjadala ulikuwa ni mkubwa sana. Mtakumbuka mpaka TBL na TCC hiki kiwanda cha Sigara ilikuwa ni mjadala mkubwa. Mimi nakumbuka nilikuwa chuo kikuu mwaka 2005/2006 tuliamua ku-beggar eneo kwa ajili ya kujenga Mlimani City, tuliambiwa Chuo Kikuu kimeuzwa, lakini tulisimama imara, Rais Kikwete akatusimamia. Sidhani kama leo kuna Mtanzania atalalamika kuhusu Mlimani City. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hofu ya pili inayoeleweka lazima tukubali kwamba hatuna historia nzuri sana kwenye ubinafsishaji. Kutokana na historia ya baadhi ya mambo wananchi waliingia hofu kwa sababu katika baadhi maeneo tulipigwa kwa kweli lazima tukiri, na kwa sababu hiyo hofu zinaeleweka na hofu hii Mheshimiwa Mkapa aliwahi kuieleza wakati wa NBC. Baada ya kelele kubwa sana za NBC Rais Mkapa alitulia akauliza tatizo ni nini? Ndipo akarekebisha wakati wa NMB. Ndio maana akauliza nifanyeje, akashauriwa kwamba NMB Serikali iwe na ubia, lakini vilevile ili ipate mtaji, watumishi wako wote wa Serikali na wengine wapitishie mtaji NMB. Ndio maana unaona leo NMB ni taasisi imara na inafanya kazi vizuri sana. (Makofi)

Kwa hiyo, katika mchakato wa ubinafsishaji Serikali imekuwa ikirekebisha pale panapohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, sitaki kulizungumzia sana kwa sababu Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri wamekwishaeleza kwamba azimio linahusu nini. Azimio hili kama alivyosema Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri tunazungumzia kuanzisha mahusiano ya kiuchumi na kijamii kati ya nchi mbili Serikali yetu na Serikali ya Dubai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo tukisharidhia Serikali inakwenda kufanya kazi yake ya kawaida ya kuingia kwenye mikataba. Kwa hiyo, hapa tulipo waheshimwa wananchi hatuna mkataba wa TPA na DP World, wala hiyo sio kazi ya Bunge hili hiyo ni kazi ya Serikali. Kwa hiyo, hilo jambo lieleweke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma Mkataba huu kama alivyosoma Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri appendix I inazungumzia maeneo tutakayoingia kwenye miradi ni Bandari ya Dar es Salaam, akifanya vizuri Serikali inaweza kumwalika ndivyo mkataba unavyosema aende kwenye maeneo mengine. So, it is not automatic tunazungumzia Bandari ya Dar es salaam na baadhi ya maeneo, Berth Zero, Berth Four, Berth One to Four, Berth Five to Seven, kwa hiyo, ipo wazi jambo hili lieleweke.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne, Waheshimiwa Wabunge, sisi kama Wabunge tuna jukumu pale ambapo kunakuwa na upungufu kwa kuzingatia hisia za watu na hofu zao na mapendekezo yao kurekebisha pale ambapo inahitajika kurekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka kupendekeza kwa kuzingatia Ibara ya 22 kwa sababu watu pia wanasema Mkataba huu hauna namna ya kurekebisha. Mkataba unarekebishika kwa Ibara ya 22 imeweka wazi kwamba inawezekana kurekebeshika, kwa sababu kengele imelia nitaachia hapo, lakini nataka kupendekeza maeneo ya kurekebisha ikafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, moja ni suala la timeframe; hili limezungumzwa sana na wananchi kwamba mkataba hauna timeframe na wataalamu wetu wametoa maelezo kwamba mikataba ya namna hii kimataifa ni kawaida kutokuwa na timeframe. Hata hivyo, waende wakaangalie sisi ni Bunge la Taifa wala sisi sio Bunge la Kimataifa, kama hizo ndizo hisia a wananchi na ndio matakwa ya wananchi, angalieni uwezekano wa kurekebisha hata mkisema not exceeding 25 years that is fine ili kutoa hiyo hofu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni Ibara ya 23(4) kile kipengele kingeweza kuondoka kile ambacho kinaaeleza kwamba mkataba hauvunjiki. Kimsingi Mkataba unavunjika mle mle ndani. Kwa hiyo, waangalie lugha iliyotumika ili kuwaaminisha wananchi wa Tanzania kwamba inawezkana kuvunja Mkataba.

Mheshimiwa Spika, jambo la tano na mwisho, ni mambo ya kuzingatia kwenye mikataba ijayo kwa wataalamu wetu, yapo mengi lakini la kwanza, kwenye ile bandari yetu pale kwenye appendix I, kimsingi ni maeneo ambayo tumekwishafanya uwekezaji. Kwa hiyo, tunatarajia mkataba ambao mtakaoingia uta–focus zaidi kwenye eneo la uendeshaji kuliko uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, pili, kwa maoni yangu ni maeneo ya mifumo ya TEHAMA; hili ni eneo sensitive linahusu usalama wa nchi, tuombe sana watu watu wa TCRA na e-Government wawepo, asiachiwe mwekezaji peke yake. Lazima watu wetu wahusike kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, kila nchi kuna nchi zimebahatika kuwa na waasisi, nyingine hazina. Sisi ni moja ya nchi ambazo tuna waasisi kama ilivyo Marekani wana George Washngton - Rais wao wa kwanza aliwaachia misingi. Msingi mkubwa ambao Marekani wanaulinda kwa wivu mkubwa ni liberty kwa sababu ndio walioachiwa kwa maana ya uhuru wa watu wao.

Mheshimiwa Spika, sisi tuna waasisi nchi hii, Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Karume ndio waasisi wa Taifa hili, na walituachia misingi kama ambavyo ilivyo kwa Marekani tunapaswa tusiiguse. Msingi mama wa Taifa hili mwalimu alisema; “silaha na sifa yetu kubwa ni umoja.” (Makofi)

Kwa hiyo, nchi yetu ni mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, bila shaka tutatofautiana kimtazamo kuhusu sera na mikakati, lakini kamwe tofauti zetu zisiende kugusa misingi mama ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi Kitila Mkumbo natoka Kijiji cha Mgela, Kata ya Mtoa, Tarafa ya Ishedede Wilaya ya Iramba - Singida lakini mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo - Dar es Salaam, hilo limewezekana kwa sababu ya umoja wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna nchi ambazo Wabunge wao ni Wabunge wa makabila sio Tanzania, tunataka na tunatamani huko tuendako watoto wangu, watoto wa wajukuu zangu mimi atoke Iramba akagombee Ubunge Pemba, atoke Pemba akagombee Ubunge Bukoba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuwaombe na tuwasihi wanasiasa na sisi viongozi tuepuke kauli na ambazo zinagusa misingi mama, tutofautiane kisera, hiyo inatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kwa dakika moja tu naomba nitoe wito kwa wataalamu wetu. Wataalamu wetu mmesikia hofu, hisia na matamanio ya Watanzania. Watanzania hawapingi ubinafsishaji wa bandari wanataka mikataba iwe mizuri, kwa hiyo wataalamu wetu hilo lizingatiwe. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo nilikuwa nakusikiliza mchango wako. Samahani hapa mwishoni hapa badala ya hili neno ubinafsishaji linaweza tena kutuma ujumbe mwingine. Nadhani kuna tofauti ya uwekezaji na ubinafsishaji. Hitimisha hoja yako kwa sekunde thelathini.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wataalamu wetu mzingatie hilo ili uwekezaji uwe mzuri.

Mheshimiwa Spika, mwisho tuliombe Bunge lako la kuanza nalo katika mikataba itakayoingiwa tuombe ije hapa kwa mujibu wa sheria tuliyonayo kwa sababu ni nyeti na ni muhimu mikataba hii ije tuipitie kama ambavyo sheria inasema itakuwa ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)