Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niwe miongoni mwa Wabunge ambao wamepata fursa hii adhimu ya kuzungumza kuhusu azimio hili ambalo tunakwenda kulipitisha, azimio ambalo limepata kuzungumzwa na Watanzania wengi sana huko nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa kuwaomba Watanzania kwamba shughuli ya leo tunayoifanya tunaifanya kwa niaba yao Kikatiba, hofu waliyokuwa nayo na sisi mwanzoni tulikuwa na hofu hiyo hiyo, lakini baada ya kujiridhisha kwa kupitishwa na wataalamu wetu kwenye jambo hili hofu yetu imeondoka, na nataka niseme kuanzia sasa tutaendelea kuwapa elimu wenzetu walioko nje ya Bunge hili na tukitoka hapa tukirudi majimboni tutakwenda kuifanya kazi hiyo vizuri pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, makubaliano haya ya ujumla sehemu zote ambazo Watanzania wana hofu tutakwenda kuzikazia zaidi kwenye mkataba mmoja mmoja kwenye miradi inayokwenda kuingiwa, na sisi hapa hatupo kwa ajili ya kuyashauri hayo ambayo wao wana hofu nayo na sisi tunaona kwamba ni ya msingi na kwamba Serikali inapokwenda kuingia mkataba mmoja mmoja ikayakazie. Mambo hayo ni pamoja na mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, Serikali baada ya azimio hili kupita waende wakafanye valuation ya Bandari yetu ya Dar es Salaam, na ambao kwa kweli kwenye appendix I ndipo ambapo mwekezaji au wenzetu wamechagua kwamba tukashirikiane nao. Kwa hiyo, ni muhimu sana kufanya valuation ya bandari ili tujue asset tulizonazo kwenye bandari yetu, tujue reliability zilizopo kwenye bandari yetu na kwa ujumla tuujue mtaji wetu uliopo kwenye bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni muhimu sana kufanyika kwa sababu tunakaribisha mwekezaji mwingine na anaondoka mwekezaji mwingine TICTS aliyekuwepo pale. Kwa hiyo ni muhimu tukafanya valuation, tujue mtaji, lakini vilevile tujue future earnings, lakini vilevile tujue market value ya asset zetu, ni muhimu sana jambo hili lifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ni la muhimu sana kufanyika ni feasibility study. Tufanye feasibility study ya miradi yote ambayo tunafikiri kwamba au ambayo tutakwenda kukubaliana na mwekezaji anayekuja kabla ya kuingia mikataba naye tufanye feasibility study. Kwa nini nasema feasibility study? Feasibility study itatuambia kwamba katika bandari ambazo mwekezaji ameonesha nia na katika maeneo ambayo mwekezaji ameonesha nia anatutoa pale kwa uwekezaji wake kutupeleka wapi? Kwa mfano mpaka sasa bandari zote 86 zinazohudumiwa na TPA zinapokea meli 4,686; feasibility study itatuonesha kwamba kwa uwekezaji anaoenda kufanya atatupeleka kwenye kupokea meli ngapi kutoka hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili mpaka sasa tunapokea tani za mizigo milioni 20.709 uwekezaji huu unaokuja feasibility study itatuonesha kwamba ukifanyika tutafikia level ipi? Katika hizo tani milioni 20 tunazopokea za mizigo milioni 18 zote ni za Bandari ya Dar es Salaam ambalo ndio eneo kwa phase ya kwanza mwekezaji ameonesha interest. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine feasibility study ikatuoneshe kwamba kutoka kwenye makontena 823,404 ambayo tunayapokea kwa sasa, uwekezaji huu utatupeleka kwenye makontena mangapi? Kwamba baada ya uwekezaji na baada ya bandari kwenda kwenye full swing tutakuwa na uwezo wa kupokea kontena ngapi?

Ndugu zangu Watanzania na ndugu Wabunge wenzangu hivi ndio vipimo ambavyo kwenye mikataba inayoenda kufanyika mbele lazima tuwe navyo ili miaka kadhaa baadae tuweze kujitathmini kwamba uwekezaji huu tulioupokea na tunaouridhia umetusaidia au umeturudisha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uwekezaji huu unaofanyika tukafanye feasibility study ili tujue kwa sasa tuna magari 200,938 hayajahudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam, tunatarajia mzigo uongezeke kwa uwekezaji unaokuja na magari yanayohudumiwa waongezeke ajira za Watanzania ziwepo na chain yote ya uchumi ionekane kwa uwekezaji unaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bandari yetu na katika vitu kwa kweli ambavyo tunahamasika na tunakubalina sote kwamba tunamhitaji mwekezaji ni ili kuongeza mzigo ambao bandari inahudumia wa nchi jirani. Hivi sasa bandari yetu inahudumia mzigo kutoka nchi jirani tani milioni 7.7 tunatarajia baada ya uwekezaji kufanyika na mikataba tunayokwenda kuingia mmoja mmoja ikatuwezeshe kututoa hapa kwenye kupokea tani milioni saba peke yake kwa maana ya mizigo ya Zambia iongezeke, mizigo ya Kongo ikaongezeke, mizigo ya Burundi ikaongezeke, mizigo ya Rwanda ikaongezeke na Malawi ikaongezeke, Uganda ikaongezeke na nchi zingine kama vile Msumbiji, Sudan, Kenya, Comoro, Angola na Zimbambwe, uwekezaji utusaidie kufika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili watu wengi wamelizungumzia huko nje, wapo waliolipotoshwa, lakini wapo waliokwenda mbali zaidi ya kuzungumza yale ambayo ni hatari kwa umoja wa nchi yetu na mshikamano wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwakumbushe wakati nchi yetu ilipopita kipindi kukubwa cha Covid-19, wakati dunia yote ilikuwa imejifungia ndani haikuzalisha, Watanzania tulikuwa tunatembea mitaani na tulikuwa tunafanya shughuli zetu. Makamu wa Rais wa nchi hii alikuwa ni Dkt. Samia Suluhu ndio alikuwa Mshauri Mkuu wa Rais aliyekuwepo. Tulivuka salama na hatukumtilia mashaka kama ni Mtanzania au siyo Mtanzania. Jambo hili hatupaswi kuliendekeza, yanapokuja mambo ya msingi ya hoja tutofautiane kwa hoja na si kwa kubaguana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawakumbusha Watanzania, miaka miwili iliyopita shughuli za kisiasa hazikuwa zinaruhusiwa kufanyika, hapakuwa na mikutano wa chama cha siasa wala hapakuwa na press conference za kwenye vyombo vya habari, ni Rais huyu huyu ndio alikuja akafungua hiyo minyororo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini wakati ule na yale yalikuwa ni mambo ya kitaifa ni mambo ya kikatiba kama ambavyo tunafanya hili la leo, kwa nini wakati ule hamkuhoji kwamba huyu ni Mzanzibar amekuja kufungulia vyombo vya habari? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza miaka miwili iliyopita kulikuwa na magazeti zaidi ya manne yamefungiwa online tvs, online media karibu vyombo zaidi ya 30, 40 vimefungiwa. Hivi ninavyozungumza ni Rais huyu huyu aliyepo amefungulia vyombo vyote vilivyokuwa vimefungiwa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa kengele ilishagonga, ahsante sana.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie, mpaka sasa...

SPIKA: Mheshimiwa Kwagilwa kwa kuwa umeshaomba, sekunde 30 malizia.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, mpaka sasa hakuna kesi mahakamani ya chombo chochote cha habari wala mwandishi wa habari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)