Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante, awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kutupa uhai na uzima kusimama leo hapa kuja kujadili jambo lenye maslahi na uchumi na jamii katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi kwa sababu kama ulivyosema walioomba kuchangia ni wengi.
Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa nataka niseme msemo mmoja ambao msemo tunautumia; maa filbidhi ilaldaras; kwenye weupe ukisugua utatia doa, kwenye weupe ukisugua utaweka doa. Maana ukisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambaye leo hajaruhusu kusema kwamba maelezo haya yaende kwenye Hansard. Watanzania huko nje wamemsikia Mheshimiwa Waziri amesema jambo moja baada ya lingine, ametaja maslahi ya Mkataba huu, ametaja chanzo au chimbuko la Mkataba huu, ameusema na Mkataba wenyewe, amechambua, amesema na faida tofauti tofauti. (Makofi)
Kwa hiyo, Watanzania tunawaomba acheni kusikia yale maneno ya watu wengine kule, hebu sikilizeni ile hotuba ambayo imesomwa na Mheshimiwa Waziri hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Mwenyekiti wa Kamati alimaliza ndio maana nikasema kwenye weupe ukisugua utatia doa; amesema kwa niaba ya Bunge lako hili tukufu na ameishauri Serikali na ameunga mkono hili azimio kwa sababu yale aliyoyaeleza sisi sote tunayakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mimi niseme kuna kitu kimoja, kwa nini watu wamezungumza yale huko nje? Kwa sababau kuna mazingira ya ushindani wa bandari yetu na kuna mazingira ya hawa wawekezaji katika bandari. Kuna ushindani wa wawekezaji katika hii bandari, sasa wengine ukisikia wanachangia huko nje wanachangia, lakini akili zao hazijasalimika. Hili neno naomba liwe noted. Kweli wametoa maoni, lakini wametoa wakati akili zao hazijasalamika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna watu wanatoa maoni haya akili zao ndani kuna vifurushi vya nongwa, wengine wanatoa maoni katika mkataba huu lakini akili zao kuna vifurushi vya tamaa kwamba kwa nini amepata mtu mwingine, wengine wanatoa maoni lakini ndani ya akili zao kuna kifurushi cha ubaguzi. (Makofi)
Sasa huwezi ukawa akili yako haiko salama ukajadili jambo likaenda salama kwa Watanzania. Naomba Watanzania wamesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kitila Mkumbo alisema nchi hii ina sera, ubinafsishaji umeanzishwa zamani, uwekezaji na sera zake upo toka enzi ya Rais Mkapa umewekwa, lakini Chama cha Mapinduzi tunayo sera hiyo. Kwa hiyo, Rais huyu huyu angetokea sehemu yoyote ya Tanzania hii angefuata sera za uwekezaji angefuata na sera za Chama cha Mapinduzi na ndicho ambacho kinachosema na ndicho kinachoongoza kusema hayo. (Makofi)
Kwa hiyo, hakufanya Rais huyu kwa sababu ya Uzanzibari, hakufanya Waziri, hakusaini kwa sababu ya Utanzania na sera yetu, mageuzi yetu ndio yaliyoturuhusu tufanye haya na tumefanya tumejirekebisha kama walivyozungumza wazungumzaji wengine na ndipo tukafika hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini hebu kila mmoja avute akili yake atizame kuna kikatuni kimoja kilikuwa kinaitwa cha nipashe, kinakuwa kina mdomo mrefu na masikio makubwa kinampasha mtu, halafu chukueni ile sura ya kile kikatuni mlinganisheni kuna mtu fulani alikuwa anazungumza maneno hayo utapata. Sasa sisi hatuwezi kusikiliza umbea kama huu ambao wao walikuwa wakiuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja ambayo imeshughulikia alisema haya ni makubaliano na makubaliano haya yanaweka msingi wa kitu kitakachokuja kufanyika, hiyo mikataba itakayokuja kujengwa huko mbele. Huu sio mkataba wameshazungumza watu, huu sio mkataba, tunawatoa hofu Watanzania wayasikilize hayo maelezo vizuri, lakini mikataba itakuja mmoja mmoja katika eneo moja moja.
Mheshimiwa Spika, ukienda katika mkataba huu kuna appendix I ambayo kuna mambo ambayo phase one project zitakazofanyika. Kwa hiyo, ndani ya project zile zitakapofanyika ndipo kutakuwa kuna hiyo mikataba midogo midogo na mimi nilitoe hofu Bunge hili na wananchi wa Tanzania sio kwamba kila kilichotajwa kwamba kitafanyika kwa yote. Ukisikia kutafanyika development, ukisikia kutafanyika improvement ukisikia kutafanyika management, ukisikia kutafanyika operations, kuna miradi au kuna phase au kuna project ziko katika hatua tofauti tofauti. Ziko nyingine tutaanza kweli ku–develop kwa sababu ni kitu kipya, lakini kuna vingine vinatakiwa kufanyiwa management, lakini kuna vingine vitafanyiwa operation. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ukitazama kuanzia hiyo gati zero mpaka gati number seven utakuja kuona kwamba ni kweli, ukiijua ile bandari kwamba kuna maeneo kutafanyika operation na kuna maeneo mengine wao wata-improve lakini wataachiwa bandari wenyewe waendeleze. Sasa na mimi na stick pale pale kwenye ushauri wa Kamati kwamba ni lazima tuhakikishe hiyo mikataba sasa iwe ina tija kwa Watanzania. Tuhakikishe hiyo mikataba wanashirikishwa wadau husika tutakapoingia hiyo mikataba mmoja mmoja, lakini pia mikataba hiyo ni lazima itoe ukomo au itaje ukomo kama wananvyosema wengine na maoni mwengine ambayo Mwenyekiti ameshauri na Wajumbe wengine Wabunge wengine wameshauri.
Mheshimiwa Spika, lakini hofu nyingine kwamba huu mkataba hauna ukomo, mkataba huu unao ukomo nao umetajwa, sisi kama Wabunge wa Bunge lako hili tukufu tumekaa hapa kwamba tunaelewa nini kinaendelea, sasa tuwaombe Watanzania kile kifurushi walichochanganyiwa kule nje sicho, vifurushi vile vinatokana na mambo tofauti tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwenye ajira za Watanzania ndani ya mkataba huu cha kwanza ni kulinda ajira zilizokuwepo, lakini kutokana na faida na utanuzi ina maana zitapatikana na ajira nyingine. Sasa hapa ndipo tutakapojua kwamba tulikuwa tukipotoshwa ajira haziendi kutolewa, haziendi kuondolewa, tunaenda kuongeza ajira katika mkataba huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye manufaa tumeambiwa kwamba siku za kuteremsha makasha zitatoka kuanzia 4.5 mpaka siku mbili, ina maana hiyo ni tija, lakini pia meli kutoka siku tano mpaka saa 24 ni tija hiyo, lakini fedha ambazo zitakusanywa kutoka trilioni 7.7 mpaka trilioni 26.7; haya ni maendeleo makubwa kutokana na haya mageuzi. Sasa sisi kama Wabunge ndio tukasema kwamba hili azimio tunaiunga mkono Serikali kwa sababu tuko katika masuala ya kiuchumi na bandari zetu zina ushindani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, DP World yeye ana market nyingi sana, lakini isitoshe anataka kutuunga mkono ili reli yetu ambayo tumeianzisha ya Standard Gauge ipate mzigo, sasa tushaanzisha reli ipate mzigo halafu tuna ufinyu wa kushusha bandarani unafikirri tutaendelea wapi. Reli itakuja kuwa ya abiria... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nashukuru kwa nafasi. (Makofi)