Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi ya kuchangia na ninaomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na harakati anazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya mama Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa makubaliano zaidi ya 17 ambayo ameingia kwa maslahi ya Taifa letu. Mheshimiwa Rais anafahamu umuhimu wa sekta binafsi na ndiyo maana yeye mwenyewe amekuwa kipaumbele katika kuja na makubaliano haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, duniani kote, duniani kote na siyo maneno yangu ni maneno ya takwimu kwa sababu wanasema no research, no right to speak, siyo maneno yangu mimi. Duniani kote uwekezaji wa sekta binafsi ndiyo mhimili wa maendeleo ya Taifa lolote duniani kote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu za International Finance Corporation zinasema; kazi zote na ajira zote takribani 90% duniani kote zinachagizwa na zinaletwa na sekta binafsi. Shirika hili linasema 60% ya pato la Taifa kwa nchi zote duniani zinachagizwa na sekta binafsi. Benki ya Dunia inakadiria kwamba 90% ya kazi zote duniani katika mataifa yanayoendelea zinaletwa na sekta binafsi na sisi hata Watanzania hapa ni mashahidi kwa sababu kazi nyingi na ajira nyingi zipo kwenye sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile sekta binafsi ndiyo ambayo kwa takwimu inachagiza zaidi kwenye upatikanaji wa kodi na mapato kwa Serikali duniani kote na hayo siyo maneno yangu. Mataifa makubwa ama mashirika makubwa ya kitaifa ambayo tumeyakasimu madaraka kwa mfano Economic Cooperation and Development yamethibitisha, kwa mfano kodi ya makampuni ambayo hata sisi tunaitegemea kwa kiasi kikubwa kwenye kuendesha Serikali yetu duniani kote inaletwa zaidi na sekta binafsi. Kwa hiyo ni masuala ambayo kwa kweli yamejiweka wazi na yamejitanabaisha wazi kwenye umuhimu wa sekta binafsi na ndiyo maana makubaliano yoyote yanayoingiwa yanachagiza zaidi ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asilimia 75 ya miundombinu yote duniani kwenye uwekezaji mkubwa wowote duniani unamilikiwa na sekta binafsi na ndiyo sekta ambayo imetusaidia kukidhi changamoto za miundombinu ambayo nchi yoyote duniani inayo kwa sababu sekta binafsi ndiyo ambayo inaweza kuwekeza zaidi kwenye teknolojia, ujasiriamali kwa sababu ndiyo ambayo inaweza kukidhi ushindani kuliko uwekezaji ambao unaweza kufanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo ushindani unaokua kwa kasi sana kutokana na maendeleo ya teknolojia huwezi kuacha kushirikisha sekta binafsi ili kukabiliana nao. Kila siku tunasimama hapa na tunasema jamani teknolojia haipigwi ngumi. Ukipiga ngumi teknolojia kwa zama hizi za sayansi na teknolojia umeenda na maji. Huwezi kuacha ku-involve sekta binafsi ili iwekeze kwenye teknolojia iweze kutusaidia sisi kusonga mbele kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunafahamu Tanzania ni nchi ya 141 kati ya nchi 177 kwenye uwekezaji wa biashara na mojawapo ya changamoto kubwa zinazotufanya tuwe nyuma ni changamoto za uendeshaji wa bandari kwa sababu ndiyo eneo ambalo lilipaswa kutuingizia mapato makubwa kama Taifa na ili tuweze kutoka kwenye 141 na tuende kwenye nafasi ambazo zinatufanya kama Taifa tuweze kushindana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kazi yetu kama Bunge ni kushauri na kwenye makubaliano haya kwa kweli tutasimama kidedea. Baada ya miaka 60 ya Uhuru hatuwezi kuendesha nchi yetu conventional, hilo ni jambo ambalo haliwezekani. Ni lazima tukubali Tanzania siyo kijiji. Ni lazima tukubali sisi tupo kwenye ushindani. Haiwezekani meli zichukue siku 4.5 mapaka tano kushushwa bandarini, wakati jirani yetu anatumia siku moja kushusha mzigo wake. Kwa akili ya kibiashara wafanyabiashara wote hawawezi kuja kwako kwa ajili ya biashara. Kwa hiyo, lazima tukubaliane wote tunasemaga hapa Serikali haiwezi kuwekeza yenyewe kwa sababu ya namna ambavyo Serikali zetu zinajiendesha, kwa hiyo ni lazima tu-involve sekta binafsi kwa sababu ndiyo sekta ambayo kwanza inafanya research kwa haraka sana na pia inaweza ku-adapt kwa sababu ya sera ya sekta binafsi inaweza ku-adapt mazingira kwa haraka sana, kwa hiyo hata teknolojia ina adapt kwa haraka mno. Kwa hiyo, ni lazima tu-involve sekta binafsi katika kuhakikisha maendeleo ya Taifa letu tunapiga hatua kwa kasi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, humu ndani hakuna Mbunge ambaye siyo Mtanzania, wote sisi ni Watanzania na hakuna Mbunge ambaye hana uzalendo kwa mama Tanzania, kila Mbunge humu ndani ana uzalendo wa hali ya juu sana kwa mama Tanzaniam kwa hiyo hakuna Mbunge ambaye anaweza kuidhinisha mkataba unaoenda kuuza rasilimali kubwa kama ya bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nielezee kuhusiana na mkataba; mkataba ule hakuna Mbunge humu ambaye ni mangungu wa Msovero hajui kusoma, wala hajui maslahi ambayo sisi kama Taifa tunaingia. Ule mkataba ni kwa sababu baadhi ya watu wanapenda kuwasomea wenzao baadhi tu ya vifungu labda nusu kingine hamalizii, lakini nitakupa mifano miwili tu ya umakini wa ule mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huko nyuma tukienda kwenye ku-solve migogoro inayohusiana na mashirikiano kati ya sisi na makampuni ya kimataifa tulikuwa tunatumia sheria za wengine katika kutatua migogoro yetu sisi wenyewe, lakini mkataba huu umesema; migogoro yoyote itakayohusika na uendeshaji wa bandari kwenye mikataba ya HGA hata kama tutaenda kutumia usuluhishaji kwenye platform za kimataifa, tutatumia sheria zetu za Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria ya Uingereza ambayo inasemwa itatumika ni ile kwenye mkataba wa nchi kwa nchi kwa sababu sisi wote ni independent states, hatuwezi kutumia sheria ya Tanzania ama sheria ya Dubai kwa sababu lazima twende kwenye neutral point. Kwa hiyo, mikataba ya uendeshaji wa bandari itakuwa determined migogoro yake kwa kutumia sheria zetu za Tanzania hata kama tukienda ICSID ambako ndiyo migogoro mingi inaenda kutatuliwa hata kama tukikaa South Africa sheria ambayo itatumika kwanza ni Sheria ya Tanzania. Kwa hiyo, ni mkataba ambao unaangalia maslahi ya Watanzania kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye suala la ukomo; mkataba huu hauwezi kuweka ukomo kwa sababu tutakuwa hatujitendei haki kama Watanzania. Mkataba wa uendeshaji wa bandari ndiyo ambao utaweka ukomo, ukiweka miaka 15 ukomo ina maana mkataba huu miaka 15 ikiisha na mkataba huu utaisha. Sasa leo tuweke miaka 40 uendeshaji wa bandari tunaenda kuweka miaka 25, sasa inakuwaje tujifunge sisi wenyewe? Kwa hiyo, ndiyo maana nasema umakini umefanyika kwenye mkataba huu ili kuhakikisha kwamba maslahi ya Taifa yanalindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho Watanzania wana hofu kwa sababu uwekezaji huko nyuma kuna baadhi ya watu wasio waaminifu wamewahi kutuingiza hasara Taifa letu. Kwa hiyo, sasa lazima vilevile tushauri na tutoe angalizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Bunge ni tunaisimamia Serikali na kuishauri, hatuwezi kuhusika kwenye kutunga mkataba halafu baadaye pia tukaja kuusimamia huo mkataba husika, lakini tunataka tuwaambie watendaji ambao wamekasimiwa haya madaraka, huko nyuma kama Taifa tumeingia hasara sana, safari hii tutatoa macho kweli kweli, hatutakubali. Tutahakikisha mikataba yote inayopitiwa na inayopitishwa ina maslahi kwa mama Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo tutahakikisha tunatoa macho, tunasimamia na kama kuna mtendaji ambaye ataweka masuala yoyote ambayo yana maslahi binafsi au kwa kikundi cha watu kwa kweli tutahakikisha wanawajibishwa kulingana na sheria yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)