Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nianze kuwa kutoa mfano rahisi, kama ambavyo tunafahamu kwamba Kariakoo ni kitovu cha biashara cha Tanzania nzima na hivyo hivyo Dubai ni kitovu cha biashara cha dunia kwa sasa; kwa sababu gani? Wamefikaje hapo wenzetu? Wamefika hapo kwa sababu ya umahiri na weledi katika sekta ya usafiri na usafirishaji. Leo ndiyo maana utatoka hapa Tanzania utaunganisha ndege Dubai, utafanya shopping Dubai, utafanya mambo mengi Dubai. Wamefika hapo kwa sababu ya weledi na umahiri wao na eneo la bandari ni eneo mojawapo la umahiri na ndiyo maana wameweza kuongoza bandari zaidi ya 50 duniani maana yake wana uwezo mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kuchangia kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kwenda Dubai mwaka jana kuhudhuria Dubai Expo na msingi wa kuhudhuria Dubai Expo ndiyo ukamfanya apate nafasi ya kuzungumza na mtawala wa Dubai mambo mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi zetu mbili ambayo mazungumzo hayo ndiyo yaliweka msingi wa hati ya makubaliano (MoU) iliyosainiwa mwezi wa pili mwaka jana na baadaye mazungumzo yakafanyika kati ya wataalamu wa nchi zetu mbili ambao wamekuja sasa na haya makubaliano kati ya nchi mbili ya IGA ambayo tunayaridhia leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais kama asingeeda Dubai mwaka jana inawezekana pengine leo tusingekuwa tunajadili namna ya kuridhia mkataba huu.

Mheshimiwa Spika, katika mkataba huu baada ya kuwa nimeusoma na kusikiliza maelezo mengi ya wanasheria nimeuelewa vizuri katika maeneo mawili makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza la kiutawala; mkataba huu kiutawala ni mkataba kati ya nchi mbili; Tanzania na Dubai na ni mkataba ambao unatoa mwongozo kwa mikataba rasmi, mikataba mahususi ya miradi ambayo itatekelezwa baadaye. Kuna upotoshaji ambao ulifanyika uonekane kama vile mkataba huu tayari ni mkataba wa kazi. Huu siyo mkataba wa utekelezaji, huu ni mkataba ambao unatoa mwongozo wa jumla kwa miradi yote ambayo Kampuni au Shirika la Bandari na hii Kampuni ya DP World wataingia baadaye katika maeneo mbalimbali na mikataba hiyo ambayo itaingiwa baadaye ndiyo itakuwa na muda maalum wa utekelezaji. Inaweza ikawa miaka 10 kufanya kazi hii, miaka mitano kufanya kazi hii, miaka 15 kufanya kazi fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakimaliza phase one ile ndiyo wataingia sasa kutokana na matakwa ya bandari yetu, Shirika la Bandari letu litakavyopendekeza ndiyo wanaweza wakaenda kwenye maeneo mengine kutoka kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala hili kumekuwa na upotoshaji mwingi sana wa makusudi na wengine siyo wa makusudi kwenye mitandao ya kijamii, na mimi napenda nizungumze mambo mawili makubwa ambayo yamekuwa yanapotoshwa. Wanasema mkataba huu huu haurekebishiki lakini ukisoma kifungu hapa kimesomwa, Waziri kasoma na wewe mwenyewe kila mtu hapa amesoma kifungu cha 22 kinaruhusu marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkataba huu hauvunjiki, kifungu cha 23 kinaruhusu unaweza ukavunjika lakini kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwenye kifungu cha 20 na kifungu cha 20 kimeweka umakini kwamba huwezi kuamka tu asubuhi unavunja mkataba, haiwezekani. Tutumie kwanza njia za kidiplomasia na diplomasia ya uchumi tumeanza kuizungumza zaidi ya miaka 20 iliyopita itatumika. Tukishindwa kwenye diplomasia twende kwenye Kamati yetu ya Pamoja kati ya Tanzania na Dubai. Kamati ya wataalamu wakae pamoja wajadiliane kwa undani, ikishindikana kabisa ndiyo tutakwenda kwenye usuluhishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hawa wenzetu, kwa kweli ukisoma baadhi ya maoni ya wenzetu nadhani walikuwa wanapotosha wengine ni wanasheria kabisa walikuwa wanapotosha tu kwa makusudi, mwingine anasoma kifungu hakisomi mpaka mwisho, mwingine anasoma kifungu kimoja kinachofuatia hasomi, halafu anajaribu kupotosha umma wa Watanzania, hilo lilikuwa ni kwa upande wa kiutawala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuichumi mkataba huu unapata uhalali wa kiuchumi (economic justification) kwa sababu kuu tatu; kwanza mkataba huu kama mwongozo unaweka nidhamu katika usimamizi wa fursa za uwekezaji na kusimamia viwango vya utendaji. Mkataba huu kama mwongozo unalazimisha taasisi zitakapokuwa za utekelezaji kuwa na weledi, umahiri na uzalendo katika utendaji wa kazi wao. Kwa hiyo, sisi kama Wabunge tukisharidhia mkataba huu tunaipa Serikali mandate sasa ya kwenda kuingia mikataba midogo midogo ambayo watazingatia viwango, watazingatia umahiri, watazingatia weledi katika utendaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hii ndio ilitumiwa na wenzetu wale tunaita Eastern Tigers Singapore, Indonesia, Korea ya Kusini na Malaysia walipiga hatua kutokana na mwenendo kama huu na huko nyuma tulifanya makosa, tulikuwa tunaingia mikataba wakati mwingine moja kwa moja bila kuwa na mkataba wa mwongozo kama huu, matokeo yake tukawa tunapata shida mbalimbali. (Makofi)

Kwa hiyo, Serikali imeona kwamba ili turekebishe shida ambayo tulikuwa tunazipata tuwe na mwongozo wa jumla ambao utakuwa ni kama reference kwa mtu yeyote ambaye atakuwa anafanya makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wawekezaji duniani kote wanahitaji mambo manne makubwa; kwanza wanahitaji umeme wa uhakika, na ndio maana Serikali inawekeza matrilioni kwenye uzalishaji wa umeme; tuwe na uhakika, waje hapa wakijenga viwanda na wanahitaji umeme, wapate umeme wa uhakika wazalishe bidhaa. Vitapita wapi? Vitapita humu kwenye njia za usafi na usafirishaji. Wanahitaji gharama nafuu za usafiri na usafirishaji ndio maana tunaboresha bandari, tunaboresha viwanja vya ndege, tunaboresha barabara, tunaboresha reli ya SGR, yote hii tunafanya kuweka matrilioni huko ili kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la tatu wanahitaji malighafi ya uhakika sekta ya kilimo na sekta za uzalishaji. Lingine ambalo tunafanya vizuri Tanzania wawekezaji wanahitaji nguvu kazi yenye ujuzi na ndio maana tunawekeza kwenye VETA kila Wilaya, kila Mkoa ili nguvu kazi iweze kupatikana. Kama wawekezaji watawekeza kila mahali, lakini bandari yetu bado inafanya kazi kwa kusuasua kama ambavyo ilivyo sasa hivi tutakuwa uwekezaji kwenye sekta nyingine huu tunafanya kama bure. (Makofi)

Kwa hiyo, ili tupate faida nzuri kabisa kwenye hizi sekta nyingine zote ni muhimu sana tuboreshe bandari kama ambavyo Serikali inajitahidi sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kadri jambo zuri, kila mtu ukimsikiliza anakwambia ni jambo zuri. Upinzani unatoka wapi? Ni maeneo manne; kuna watu wanafaidika na hali iliyopo sasa hivi, changamoto za bandarini pale kuna watu wanafaidika, hao lazima wapige vita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna watu wengine wanapinga ni washindani wa bandari yetu wa pande zetu, wengine majirani zetu, kwa hiyo lazima wapinge. Kuna watu wengine ni wapinzani wa hii kampuni ya DP World na wapinzani wa Dubai, lazima wapinge. Lakini hivi mimi najiuliza ingekuwa Serikali imeleta mwekezaji anatoka Canada au anatoka Ulaya au Marekani hivi angepingwa kiasi hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nadhani kwa sababu sasa tumegeukia kupata fursa mpya za uwekezaji ndio maana upinzania umekuwa umezidi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, la mwisho kuna wivu wa kisiasa kwamba sasa kumbe chama hiki kiko madarakani kinaanza kufanya vizuri zaidi wanaanza kukosa fursa, nashukuru sana naunga mkono hoja, tuwe makini, naunga mkono hoja. (Makofi)