Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye jambo hili zito na kubwa kwa manufaa ya nchi yetu.

Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutuwezesha kukaa na kujadili jambo hili, lakini nitumie nafasi hii kwanza kabisa kusema kwamba wakati tunajadili jambo hili Watanzania wenzetu walio wengi wapo wanatusikiliza na wanatusikiliza ili kupata ukweli wa mambo mengi yaliyopotoshwa kabla ya sisi Wabunge wao hatujakaa hapa kujadili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii kuwaambia wananchi wa Tanzania kwamba walituamini wakatuchagua ili tuje tufanye kazi ya kuisimamia Serikali, kutunga sheria na kupitisha bajeti. Wapo Watanzania wengi kama alivyotoka kusema Dada yangu Halima Mdee huko nje anasema wapo wenye akili nyingi wengine kuliko sisi, hao wenye akili nyingi kuliko sisi, wenye akili za kati na wenye akili za chini hawakuja humu wakatuleta sisi ili tuwawakilishe wote wenye akili nyingi, akili za kati na akili za chini.

Ndugu Watanzania leo tunazungumza kwa niaba yenu, tukiwa na kiapo tulichoapa mbele ya Spika, kulinda Katiba na sheria za nchi. Lakini tukiwa na dua ambayo huwa tunaiomba kila siku ya kuliombea Bunge na kumuombea Rais wetu ili Mungu atupe hekima na busara za kufanya kazi zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini si hilo tu ninyi kila siku mmekuwa mkituombea, mashehe, mapadri, wachungaji na viongozi mbalimbali na wananchi mbalimbali ili tuweze kuifanya kazi yenu vizuri. Kama mlimsikiliza mtu yeyote kuhusu jambo hili, sasa tusikilizeni sisi mliotuamini, naona upotoshaji ni mwingi sana huko nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyotangulia kusema msemaji wa kwanza Profesa Kitila Mkumbo, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na chama kinachotawala Chama cha Mapinduzi haviwezi kuja hapa na mkataba wa kutokomeza nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais kwa wajibu wake ndiyo msimamizi wa shughuli zote za nchi, lakini ni mfariji na mlinzi wa haki za raia na watu wengine wote ambao wako kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anafanya kazi ya kuhakikisha kwamba anapo ongoza nchi yake anaangalia kila fursa ya kuvutia uwekezaji kwa manufaa ya Watanzania na tumekuwa tukimwamini hivyo, amefanya kazi kubwa kwenye Royal Tour kwa ubunifu wake na leo tunapokea watalii kwa wingi na wamekwenda kwenye maonesho Dubai, amefanya mazungumzo na Mfalme na leo sasa tunaiona nyota ya kusaidia kupata ufumbuzi wa matatizo ya bandari zetu. (Makofi)

Kwa hiyo, kwanza mimi natumia nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanya jambo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya ubia huu ambao tunataka kuingia kwa njia ya uwekezaji tulikuwa na ubia huu na Kampuni ya TICTS na hao TICTS pamoja na kwamba mkataba wao tulikuwa tunautazama kila wakati tunauangalia, tunafanya maboresho lakini bado waliweza kufanya kazi nzuri kuliko tulipokuwa tunaendesha wenyewe bandari asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zinaonesha hapa magati yote haya 11 yalipokuwa yanasimamiwa na TPA tulikuwa tunapata gawio la kama bilioni 180; lakini walipoingia TICTS wakachukua magati nane tu; gati namba 8, namba 9, namba 10 na namba 11 tukawa tunapata bilioni 345. Huku tunakokwenda sasa nataka niwaarifu Watanzania kwamba tunakwenda sasa kufanya makubwa zaidi ya yale tuliyokuwa tunayapata kwa TICTS maana ingekuwa tunataka yale tungebaki pale pale, tungeongeza mkataba lakini tumeona hapana huku tunakokwenda tutapata zaidi na tutafanikiwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo tunaliona amelisema mtoa hoja, kwamba tumekuwa na tatizo la meli zinazokuja kupakua kwa wakati, wakati mwingine zinakaa mpaka siku tano na kila meli inapokaa siku moja tunakuwa-charged dola 25,000 kama shilingi milioni 60 za Kitanzania. Ikikaa siku tano ni milioni 300 za Kitanzania, hizi gharama zote mwisho wa yote zitakwenda kuingia kwenye gharama za mlaji wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunataka kupata mwarobaini wa tatizo hili na mwarobaini wa tatizo hili ni mkataba huu ambao Serikali yetu na Serikali ya Dubai inaweka framework ya kutengeneza mikataba ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka kutumia nafasi hii kuipongeza sana Serikali na kusema kwa kweli tupige ndiyo, twende haraka tuweze kufikia hatua hii, na katika yote haya masuala yanayohusu ajira za Watanzania yamezingatiwa, masuala yanayohusu usalama wa Taifa letu yamezingatiwa, masuala yanayohusu kodi yamezingatiwa tunataka nini zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi uliniteua miongoni mwa kundi la Wabunge kushirikiana na Serikali kwenda kuangalia sekta binafsi inavyowekeza kwenye bandari. Mimi nilikwenda India, tukaenda Adani Port, tukaangalia kazi kubwa inayofanywa na wale Adani Port kule Jimbo la Gujarat tulikwenda kule Gujarat tukaangalia ile port yao wanavyoendesha. Kazi kubwa sana inafanywa na mimi nilidhani wale ndiyo watafika mahala watapata, lakini katika uchambuzi Serikali imeweka makampuni mengi ikaona hawa DP World wa Dubai ndiyo ambao kwa kweli kupitia Serikali ya Dubai wanaweza wakafika mahala huko mbele wakatusaidia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasema Serikali imefanya vizuri kuwa na makubaliano na Serikali ya Dubai ili makubaliano haya sasa yakatupe mikataba ya uwekezaji kwenye bandari zetu na maeneo mengine hatua kwa hatua na kila mkataba uwekezaji wake utakuwa na uwekezaji wake, utakuwa na gharama zake, utakuwa na malipo yake, utakuwa na faida zake na utakuwa na muda wake. Haiwezekani leo mtu awekeze katika bandari kama hivyo walivyokuwa yanasemwa hapa tumeishawekeza trilioni moja, inaweza ikawa na kazi yake Serikali ikaona huyu nikuendesha tu kwa sababu sisi tumeishawekeza na kama huyu ni kuendesha utatulipa kiasi hiki kule ambako wanawekeza, wanaleta mitambo, anatengeneza sijui hivi unajua gharama ni hii, kwa hiyo, atapaswa kulipa kiasi hiki haya yote Serikali yetu imesheheni wataalamu wa fani mbalimbali ambao tunawaamini chini ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nasema kwamba tumechelewa, tupige hatua haraka, tuweze kufika mahala tupate mwarubaini. Tukiweza kumaliza tatizo la baadhi ya bandari zetu huku tutaweza kumaliza hata matatizo ya bandari za kwetu kule Kigoma kwenye Lake Tanganyika.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)