Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia katika jambo hili tukufu kabisa lenye mustakabali mpana wa maendeleo ya Taifa letu. I(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kupata fursa ya kuchangia katika makubaliano ya kukubaliana na nchi ya Dubai katika kuendesha baadhi ya maeneo katika bandari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba naomba ni–declare interest, niliyesimama mbele yenu niliwahi kuwa Manager wa Usimamizi wa Mradi katika Bandari ya Dar es Salaam upanuzi kutoka gati…

SPIKA: Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, ngoja tuliweke vizuri hili.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Ndiyo.

SPIKA: Tunapojadili mkataba wa namna hii, ukasema unataka kuweka maslahi yako wazi na ni mkataba unaohusu uwekezaji, maana yake una maslahi ya kifedha kwenye hawa wawekezaji moja wapo.

Sasa kama ni hoja ya kusema umeshawahi kufanya kazi mahali, ama unamfahamu fulani nenda moja kwa moja, ondoa hayo maneno yako unataka kuonesha maslahi yako kuwa wazi kwenye jambo hili. (Makofi)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Dhamira yangu ni kutaka kusema kwamba ni nina uzoefu na bandari na yale upanuzi uliofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam na katika kitu ambacho ninakikumbuka mpaka leo ni kwamba Bandari ya Dar es Salaam imepanuliwa kutoka gati zero mpaka gati namba 7 na bado tunakwenda kupanua gati namba 8 mpaka gati namba 11. Haya yanayokwenda kufanyika sasa hivi ya kutafuta mbia kuendesha Bandari ya Dar es Salaam katika baadhi ya maeneo ninasema Mama Samia anaendelea kuwa mtekelezaji wa yale aliyokwishatangulia akiwa kama Makamu wa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Mama Samia amefanya mengi katika SGR na katika mengine yote ambayo ameshirikiana na mtangulizi wake yeye akiwa Makamu wa Rais, naomba niwaambie Watanzania popote mlipo na hili la uwekezaji wa kumpata mbia katika Bandari ya Dar es Salaam ni sehemu ya muendelezo ule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu gani? Makubaliano na liyetupa fedha ambaye ilikuwa ni Benki ya Dunia mwaka 2017 alipotupa mkopo wa dola za milioni 305 katika Bandari ya Dar es Salaam kutengeneza ile jumla ya milioni 421 ambayo ndiyo trilioni moja ya Tanzania ambayo imetumika kuwekeza katika Bandari ya Dar es Salaam miongoni mwa loan agreement iliyoingiwa na ile Benki ya Dunia ni kuhakikisha kwamba tunaweza kurudisha fedha ile tuliyowekeza pale kwa haraka na Benki ya Dunia katika makubaliano yale imezungumza na sisi tukayakubali kwamba bandari ile itaendeshwa kwa ubia, imesema wazi kwenye loan agreement mwaka 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niseme kwamba Serikali haikukurupuka wala Mama Samia hakukurupuka kama ambavyo wengi walidhani wamefikiri. Mama Samia anafanyakazi kwa mujibu wa maandiko ambayo ameyakuta muda mrefu katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba uwekezaji wote mkubwa unaofanyika katika Taifa letu na katika nchi zozote duniani hauwezi kufanyika kwa kukurupuka tu, ni lazima tafiti, ni lazima stadi zifanyike, ni lazima tutafute traffic forecasting, haiwezekani tufikirie mwekezaji leo kama hatujaangalia Bandari ya Dar es Salaam mwaka 2045 itakuwa na mzigo gani? Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Watanzania, Port Master Plan ya mwaka 2008 ambayo imefanyiwa mapitio mwaka 2018 na Mhandisi mshauri anayeitwa Anova Consult ambaye wala si Mtanzania, katika taarifa yake ya mwisho yote yanayofanyika sasa hivi katika Taifa letu kuanzia upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga, Bandari ya Mtwara, SGR yote yako katika maandiko yaliyofanyiwa tafiti. Serikali haikurupuki, Serikali inafanya mambo kwa maandiko, Watanzania tujifunze kusoma, Watanzania tujifunze kutafuta taarifa, Watanzania tusiishi kwa hofu, tujifunze zaidi hii ni summary report hii ni taarifa fupi ya Port Master Plan ya mwaka 2008 inazungumza yote hayo na page ya 31 mpaka 34 inazungumza suala zima la mzigo utakaokuja Bandari ya Dar es Salaam mpaka mwaka 2045. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile limezungumzwa kwenye page ya 32 suala zima la upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na vilevile katika page ya 34 imezungumza suala zima la Bandari ya Dar es Salaam kuendeshwa under PPP. (Makofi)

Sasa niwaambie ndugu zangu, Serikali yetu haiongozwi na watu wasiokuwa na akili timamu, Serikali yetu inaongozwa na watu wenye akili madhubuti. Watanzania sisi tusiyumbishwe na kupelekwa pelekwa haya mambo yako kwenye maandishi, tujifunzeni kusoma Watanzania. Inavyoonekana ni kama vile Mheshimiwa Rais amekwenda Dubai, akatekwa tu, akasaini tu yaliyosaniwa, siyo kweli. Ni kumkosea heshima Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mama yule ni mama makini, mama yule ni mama mwenye kuipenda Tanznaia kwa mapenzi makubwa sana. Ni fedheha huku kuendelea kusema kama sisi tunaweza kununuliwa bahasha hii ninunuliwe mimi Mwanaisha Ulenge? Bahasha hii nyepesi namna hii ininunue mimi? I see, Watanzania naomba muwe na imani kubwa na Serikali yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali hii ina masikio na Serikali hii ina macho, Serikali hii ina wataalam, Serikali hii inafanya tafiti. Kwa hiyo, naomba niwaambie Mama Samia ndiyo kidedea wa kutekeleza hata yaliyokuwa yamefichamana. Haya anayoyatekeleza mama Samia yalikuwa kwenye maandishi tangu mwaka 2008, Mama Samia leo anakuja kutekeleza. Mama huyu ni kichwa mwanamama wa Kizimkazi, Mungu anedelee kumsimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na tabia Watanzania ya kujilinganisha na Singapore kwamba mwaka 1960 Singapore ilikuwa masikini kama sisi. Tumekuwa na tabia ya kujilinganisha na South Korea kwamba mwaka 1960 ilikuwa kama sisi, lakini tumekuwa na tabia ya kujilinganisha na Malaysia kwamba walikuwa kama sisi.

Sasa katika kitabu hiki nilichokishika mkononi hapa ambacho kimeandikwa na Mtanzania mwenzetu aliyefanya tafiti za Afrika nzima...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia kwa sekunde 30.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: ...ambacho kinaitwa Poverty within, not in the skin kinaeleza kwamba Malaysia, Singapore and South Korea walitoka katika umaskini ule kufikia walipofikia sasa kwa sababu waliamua kuingia katika advancement in technology.

SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)