Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru sana, lakini nikiri kwamba una Wabunge wazuri sana, tangu asubuhi saa 3:00 mpaka saa hizi nafikiri asilimia kubwa ya Watanzania wameelewa azimio lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niseme ukweli, nitazungumza kidogo wala sitachukua muda wangu mrefu. Ni kweli nimemsikiliza mtoa hoja Mheshimiwa Waziri, nimemsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu wamezungumza jambo kubwa, lakini mimi nafikiri nitaliongeza kidogo kwamba huu sio mkataba, huu sio mkataba wa kiutendaji.

Mheshimiwa Spika, haya ni makubaliano kati ya nchi na nchi. Tumepata Uhuru mwaka 1961 Waheshimiwa Wabunge, nina uhakika Serikali zote zote zimeingia makubaliano kama haya, ni kwa sababu tu tulikuwa hatuletewi hapa kuridhia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano, Serikali ilishawahi kuingia makubaliano na nchi ya Marekani kama haya haya upande wa afya; Serikali ilishawahi kuingia makubaliano kama haya na Canada upande wa elimu, hakuna kitu kipya Waheshimiwa Watanzania; na Serikali ilishawahi kuingia makubaliano kama haya na China upande wa biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Watanzania wanachanganywa, lakini hili jambo la makubaliano ni jambo la kawaida kabisa na ninaomba Watanzania muone kwamba kipindi hiki linaleta hekaheka kwa sababu imepitishwa hapa turidhie. Hii ni mara ya pili tunaridhia.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Issa Mtemvu.

TAARIFA

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, mchangiaji anachangia vizuri sana, eneo la historia kwa makubaliano kama hayo unayoyasema, hata juzi tu tunayo makubaliano kama haya ya bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Ohima, Tanga. Kwa hiyo, ni makubaliano yanayofanana kabisa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, naipokea Taarifa hiyo na tena ninakumbuka vizuri tuliridhia.

Kwa hiyo, Waheshimiwa Watanzania wetu, wapiga kura wetu msichanganywe, hakuna kitu kipya hapa. Hapa kitu kinachosumbua watu Awamu ya Sita inakwenda kushika nchi tena, hakuna kitu kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge Serikali ya Chama cha Mapinduzi sio wajinga, wanaingia uchaguzi mwaka ujao, wana uchaguzi mwaka 2025, walete bomu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawawezi kuleta bomu, hiki kitu ni kitu kinakwenda kutuimarisha, na Waheshimiwa Wabunge mkakitumie vizuri mtakapoomba kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongee jambo la pili; mimi nimewafurahia Watanzania sana, nimewapenda Watanzania sana kwa sababu Watanzania wameonesha hofu yao, wameonesha hofu yao kubwa, wakamfanya na Rais amefurahi sana, wameifanya na Serikali imejua Watanzania wanataka nini. Kama mmegundua, mimi nimewasikiliza kwa siku zote nikitika nikirudi nyumbani nawasikiliza kwenye njia nyingi, Watanzania wanaipenda nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanafahamu kama bandari ndio lango kubwa la mapato ya nchi yao. Kwa hiyo, wameona aah, bora tuseme, mimi ambao nawaweka kando ni wale wapotoshaji wale siwasifu, lakini Watanzania nimewapenda mno, mlitumia haki yenu ya Kikatiba, mmezungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Watanzania kilichowasumbua ni hofu; ahh hii bandari yetu, hiyo mikataba itakayoingiwa itakuwa mikataba mibovu, itamaliza nchi yetu, ndio kimewasumbua Watanzania, lakini naomba niwatoe hofu Watanzania kwa kitu kimoja kikubwa.
Mheshimiwa Spika, mimi nimetulia kwenye mitandao nikasema hivi Rais hajasema kitu chochote kuhusu mikataba?

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nimnukuu Mheshimiwa Rais. Naomba nimnukuu Mheshimiwa Rais na kwa sababu yeye anazungumza kwa sauti ndogo na mimi nizungumze kwa sauti ndogo kidogo.

Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Mheshimiwa Rais jana ITV wamemleta kwenye kipindi cha mubashara, Rais anasema hivi; “Jamani mikataba hii ina aina zake, unajua kabisa mkataba wa aina hii hauwezi kuwa na vifungu hivi vikawa ndani ya huo mkataba, lakini unaukuta mkataba wa aina hiyo na kuna kifungu cha ajabu ajabu kimo ndani ya huo mkataba ambacho hakipaswi kuwa ndani ya huo mkataba, lakini umepita kote, njia zote na mkataba ukaenda ukafanya kazi na sasa waliofanya wanadai ni kimkataba, ni kimkataba, kwenye mkataba ipo. Sasa unawapa watu wengine, hebu someni huu mkataba, wanasema huo mkataba mama haukupaswa kuwa na vifungu hivi. Sasa unawauliza ilikuwaje vikaingia? Wanaangaliana machoni. Dhambi zetu sisi wenyewe, sisi wenyewe tunauwa nchi yetu, sisi wenyewe. Unaruhusu vifungu vya ajabu vinaingia kwenye mikataba isiyopaswa, kwa hiyo, huku kwenye mikataba kuangalieni vizuri,” mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais ameshawaonesha Watanzania kwamba hataki mikataba mibovu, alilizungumza hili kabla hatujafikia kujadili hili azimio hapa. Naomba Watanzania wawe na uhakika kwamba huyu siye, hatakubali mikataba mibovu. Wawe na uhakika kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inakwenda kuleta ufanisi ndani ya bandari zetu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja na n awaomba na Waheshimiwa Wabunge tusimameni imara tuipe nafasi Serikali ifanye kazi. Ahsante sana. (Makofi)