Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu. Kwa sababu za wazi kabisa nitajikita katika sekta ya ujenzi na mawasiliano na ile sekta nyingine nitai-skip kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kupongeza Baraza zima la Mawaziri, mmeanza vizuri sana na kwa kweli fikisheni salamu zetu kwa Mheshimiwa Rais kwamba anaendelea kufanya vizuri na ninyi mnaomsaidia tunawaombea kila lililo la kheri. Kwa kutambua kwamba hii ndiyo bajeti yenu ya kwanza basi sisi wenzenu tuna matumaini makubwa sana na ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekipitia kitabu cha Mheshimiwa Waziri na kwa kweli kwa kiwango kikubwa kimekaa vizuri sana, kime-capture maeneo mengi muhimu na ya msingi. Wasiwasi wangu tu ni kama yote yaliyoandikwa yatatekelezwa kama yalivyoandikwa. Kwa sababu limekuwepo tatizo la muda mrefu tu kwamba mpango huu tunaupitisha ukiwa mzuri sana lakini utekelezaji ukianza mambo mengi yale yaliyoandikwa yanaachwa yanatekelezwa mengine pia ambayo hata hayakuwa yameandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati natafiti kwa nini hili linatokea, nimejifunza tu kwamba katika ile Appropriation Act tunayoipitisha hapa, kipengele kile cha sita (6) kinatoa mwanya kwa Waziri mwenye mamlaka kufanya mabadiliko au kuhamisha pesa, wataalam wa haya mambo wanaita budget leakage. Napenda sana niseme haya Mheshimiwa Dkt. Mpango akiwa hapa kwa sababu yeye hasa ndiye mwenye kuweza kuruhusu hizi leakages kutokea. Nina hakika leakages zisingekuwepo katika bajeti hakuna Mbunge angekuwa analalamika sana hapa kwa sababu mambo tunapitisha wote na kwa hiyo tungekuwa tunatumaini yatatekelezwa kama tulivyoyapitsha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda ifike wakati tukiangalie hicho kipengele cha sita (6), tukipe masharti ili mabadiliko hayo ya fedha kutolewa fungu moja kwenda lingine yafanyike, basi ziwepo sababu za msingi na kama inawezekana angalau Kamati ya Bunge ya Bajeti iwe imeridhia mabadiliko hayo. Kwa namna hii, tutakuwa tumezuia sana au tume-ring fence mpango mzima kama tunavyokuwa tumeupitisha hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kuzungumzia ni Road Fund, lakini naomba nianze na barabara yangu. Mheshimiwa Mbarawa, hii barabara siyo ya kwangu tu, inaanzia mkoa wa Geita inaishia Mwanza. Kwa vigezo vya kiuchumi na kadhalika vyote inakidhi na kwa umuhimu huo ndiyo maana ipo katika Ilani. Mimi nisiseme mengi, nikuombe tu Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha anipe commitment, mwaka huu potelea mbali, lakini naomba commitment ya mwaka kesho na anipe kwa maandishi mzee siyo kwa mdomo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili eneo la Road Fund, katika kuchangia bajeti ya Waziri Mkuu nilitoa maoni kwamba umefika wakati Sheria ile ya Road Fund iangaliwe upya. Yakatolewa majibu hapa kwamba Serikali inaangalia utaratibu wa kuanzisha kitu kinachoitwa Tanzania Rural Roads Agency lakini kwenye kitabu humu hakuna. Kama kwenye mpango wa mwaka huu hauzungumzii chochote kuhusu hiyo agency kuanzishwa basi tuangalie kwanza tulichonacho tukifanyie marekebisho ili malalamishi ya Wabunge kuhusu barabara za vijiji na za wilaya kutokuwa na appropriate funding liishe. Leo tukiendelea hivi kwa matumaini ya Tanzania Rural Roads Agency kuanzishwa, sisi tunaokaa katika vijiji huko tutaendeea kuathirika kwa matumaini. Tubadilishe hii sheria, mgawanyo uwe mwingine, itakapanzishwa hiyo agency basi ita-fit in katika hili ambalo tutakuwa tumelianzisha na kulifanyia mabadiliko sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge katika majimbo ya vijijini, ninyi mnajua suala la fedha ya barabara zetu kwenye Halmashauri ilivyo kidogo. Tunaendelea kuomba barabara zipandishwe hadhi, zitapandishwa hadhi ngapi? Suala ni kupeleka hela huko huko barabara zinakotengenezwa na siyo kuomba zipandishwe hadhi. Mmoja alikuwa anasema sijui kuna barabara elfu kumi na tatu na mia ngapi zinasubiri kupandishwa hadhi, halafu mwaka kesho tena elfu ishirini na ngapi, mwisho wake nini? Kwa hiyo, niombe sana suala hili la ama kubadilisha Sheria ya Mfuko wa Barabara au kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini basi tuambiwe haya yote yapo katika hatua gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia hicho kitabu, barabara inayoanzia Sengerema – Nyehunge - Nkome imepewa fedha za matengenezo katika sections mbalimbali. Nimestaajabu sana kipande cha Sengerema - Nyamazugo hakimo! Tutatengeneza barabara hii kwa style gani kwamba kipande hicho kisipopata matengenezo barabara hii haipitiki na kipande hicho ni kibaya kweli, Mheshimiwa Ngeleja anajua, hakina fedha. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, niende kwenye vivuko. Ukurasa wa 211, Mheshimiwa Waziri fungua uone pale, zimetengwa fedha za kununua vivuko viwili, kimoja Kigamboni na kingine Busisi. Hata hivyo, juzi tu mmezindua daraja la Kigamboni, ndani ya kitabu hiki mmetenga fedha shilingi milioni 800 na zaidi za kuanzisha usanifu kwa ajili ya daraja la Busisi, sasa unafanya lipi? Mara unaendelea kununua vivuko pale Kigamboni huku daraja limeanza kufanya kazi. Wale watu wanatoza pale, tusiwa-sabotage kwa kuendelea kununua vivuko huku. Busisi tunataka daraja pale, habari ya kununua ferry mpaka ije ikamilike na daraja umeanza kujenga, why? Maana ferry hii siyo kibiriti kwamba utakwenda dukani utanunua kesho, utaanza tena na yenyewe michoro kuja kufikia kuipata na daraja umeanza kujenga.
Mheshimwa Mwenyekiti, nataka mliangalie upya suala hilo ili zile fedha za Busisi mpeleke Kome. Pale Kome kivuko kile sasa hivi ni kidogo na hakifai, wanapandisha huku na huku, SUMATRA hawataki kufanya kazi yao vizuri tu, wangeshakizuia kile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni gharama za ujenzi wa barabara. Naomba tu nitoe ushauri katika hili, Mheshimiwa Waziri, hebu zitazame upya. Pamoja na Sheria ya Manunuzi isiyofaa lakini nadhani zimekuwa exaggerated sana. Haiwezekani hapa Tanzania ndiyo tunajenga barabara zenye gharama kubwa kuliko dunia nzima, why? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, DSTV, Star times, Azam na kadhalika, hawa watu wawekeeni sheria ya kuwabana. Jamani ukinunua airtime ni mpaka uongee ndiyo fedha yako itumike, lakini kwa hawa watu wa ving‟amuzi ukilipa hata usifungue mwisho wa mwezi fedha imekwisha. Imekwenda wapi na mimi sijafungulia king‟amuzi? Software za ku-bill zipo, kwa nini hawa watu wa ving‟amuzi hawawekewi hizo taratibu? Tuombe tu, kwa sababu watu wanalalamikia mengine lakini na hili eneo, TCRA mko hapa mnasikiliza, kitu gani kigumu kuwaambia hawa mtu akiwasha decoder ndiyo ianze kusoma matumizi ya fedha yake? Mna mgao huko, sidhani kama mna mgao huko, basi tusaidieni tu wafunge na wao software hiyo ambayo mtu akianza kutumia king‟amuzi chao ndiyo kweli aanze kuwa billed lakini vinginevyo jamani inatuumiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unalipia DSTV Dodoma hapa mnakaa wiki mbili ukiondoka ukija kurudi hiyo ilishakwisha uanze tena kulipa upya, utakuwa na hela kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.