Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi.

Mheshimiwa Spika, leo Waheshimiwa Wabunge wanafanya kazi ya Kikatiba, lakini vilevile nimepata meseji nyingi kutoka kwa watu wa Tarime na Mkoa wa Mara naomba sasa wasikilize maelezo ya chifu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, la kwanza ni kwamba haya ni makubaliano kati ya Tanzania na Dubai kwenye mambo ya kiuchumi na mambo ya kijamii, jambo la pili kutakuwa na nafasi ya Serikali kutengeneza mikataba midogo midogo kulingana na eneo mahsusi na masharti yake, hili ni vizuri likaeleweka sana, lakini waswahili wanasema wasiwasi ndio akili. Kitendo cha Watanzania kuwa na wasiwasi na hofu ni jambo la kawaida. Mheshimiwa Rais amesikia, Serikali imesikia, Wabunge wamesikia, chama kimesikia, wataalam wamesikiana, watazingatia yote ili katika utekelezaji wa mikataba hiyo hofu ya Watanzania ikapate matibabu ya kudumu na mwisho wa siku nchi iweze kupata manufaa ambayo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile yako mambo ya msingi tu, mtu mmoja akaniambia mnauza bandari, hata ardhi watachukua. Kwenye Ibara ya 8 imezungumza namna ambavyo ardhi itatumika, imejibiwa hiyo hoja, lakini pia amezungumza habari ya ajira, imezungumzwa kwenye Ibara ya 13, local content, wazawa watapata ajira, maboresho, mafundisho na huyu mwekezaji akitoka lazima aache utaalam katika nchi yetu, lakini pia wamezungumza hoja ya kwamba mikataba haivunjwi, Ibara ya 23(4) unarudi Ibara ya 20 inaeleza utaratibu utakaotumika namna ya kuondoa migogoro hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini mimi hii ni awamu ya pili Bungeni hapa sijawahi kujadili azimio lolote hapa likiwa na mkataba wa wazi kama hivi. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Leo kila Mbunge anasimama hapa anachangia akiwa na mkataba kifungu kwa kifungu tunajiridhisha haikuwahi kutokea, sasa nauliza ambao wanalalamika hapa, hivi nani amewahi kuona mkataba wa ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam - Morogoro mmeona? Kutoka Morogoro - Dodoma, mmeona? Kwa nini hamjaona? Nani ameona mkataba ule wa Daraja la Tanzanite, Dar es Salaam, mmeona? Mmeona mkataba wa Kigongo – Busisi mmeona? Mmeona mkataba wa Bwawa la Mwalimu Nyerere? Maana yake Mheshimiwa Rais anataka uwazi katika jambo hili, ameruhusu Watanzania wajadili, watoe maoni na yupo tayari kufanya maboresho hata hapa tulipo anaangalia mijadala ya Wabunge wake, anasoma kwenye mitandao ataifanyia kazi vizuri ili Watanzania waweze kunufaika kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa mara ya kwanza kupata nafasi nzuri sana ya kujadiliana, lakini mimi nimekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi hakuna Mtanzania mwenye akili timamu ambaye atapinga uwekezaji katika bandari zetu zote hakuna atakayepinga, cha muhimu ni kwamba kama tunawekeza tunawekeza wapi, kitu gani, tunapata nini, maslahi mapana ya nchi yetu? Hiyo ni muhimu sana na ni ukweli kwamba tumezidiwa sana na wenzetu kwenye taaluma na teknolojia. Tunataka wenye uwezo waje kuwekeza ili sisi Watanzania na wataalam wenye nafasi wahakikishe kwamba maslahi ya nchi yanazingatiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye kitabu chetu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania ukurasa wa tatu, tarehe 26 Aprili, 1964 Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Watu wa Tanganyika waliungana na kuwa nchi moja na kwa hiyo, ni Taifa moja, lakini pia kwenye kitabu cha historia, sisi ni wajukuu wa Mwalimu Nyerere hebu tuwakumbushe watu mambo haya.

Mheshimiwa Spika, ukisoma kitabu cha Mwalimu Nyerere historia yake, wakati anazungumza anataja misingi ya Chama cha Mapinduzi, CCM ni chama cha wanyonge chenye kupigania vita ya ubepari na unyonyaji, lakini binadamu ni sawa, hakuna ubaguzi wa kidini, kikabila na kijinsia, lakini pia kudumisha na kutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Mwalimu alisema kwamba yeyote atakayetaka kuvunja Muungano hatakomea hapo, ataendaelea kuwagawanya watu kwa misingi ya Ubara na Uzanzibari; Uzanzibari na Upemba na kuendelea unaweza ukasema Ukurya na Uchaga; Umakonde na Umatengo na kuendelea.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Mheshimiwa Rais Mama Samia, ni Rais wa kwanza mwanamke katika nchi hii. Tulimpa heshima Baba wa Taifa akaitwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ninapendekeza huyu aitwe Mama wa Taifa kama ambavyo tulimpa Mwalimu Nyerere hiyo heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili ni mama ambaye alipoingia madarakani aliahidi kwamba kazi itaendelea na kazi inaendelea; lakini Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba hakuna kitakachosimama na hakuna kilichosimama, lakini Mheshimiwa Rais huyu kwa huruma yake alimkuta mtu yuko gerezani akamtoa, akaenda akala pale Ikulu akakaa naye, lakini huyu ameruhusu mikutano ya vyama vya siasa, mama huyu pia ametoa hata ruzuku wanafanya siasa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ningekubaliana na ndugu yangu yule kama angekosoa vifungu kwenye muswada huo au kwenye makubaliano hayo. Kitendo cha kusema kwamba Mheshimiwa Rais kwa sababu ni Mzanzibari anauza Bandari ya Dar es Salaam na Ndugu Profesa Makame Mnyaa Mbarawa kwa sababu ni Mpemba, ni Mzanzibari anauza Bandari ya Watanganyika, Mheshimiwa Mbowe amemkosea sana Mheshimiwa Rais, amewakosea sana Watanzania na Mheshimiwa Mbowe anapaswa kumwomba radhi Mheshimiwa Rais kwa kumdhalilisha, lakini kuleta dalili mbaya za kuligawa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kujadili hoja za msingi za Watanzania kwa misingi ya tulipotokea. Profesa Kitila amesema amekuwa Mbunge wa Ubungo, mimi nimekuwa Mwenyekiti wa Mtaa pale Kivule, Dar es Salaam, nimekuwa Mbunge wa Dar es Salaam hata Mlimani nilikuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina Watanzania wote na watu kutoka nje wangeniuliza mimi ni Mkurya kutoka Kanganiani nisingepata fursa hiyo.

Mheshimiwa Spika, nataka nikwambie kitendo hiki viongozi wa nchi hii lazima tukichukulie hatua. Kwenye Vyama vya Siasa, kwenye sheria yetu Political Parties, inataja mahsusi kwamba Chama cha Siasa lazima kioneshe Ibara mahsusi ambayo italinda Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tutaruhusu mijadala ya design hii ya kuanza kubagua ukimsema Rais wa nchi umemsema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, nataka niwambie Watanzania, wanachama, viongozi, wafuasi wa Chama cha Mapinduzi hatuwezi kukaa kimya kwa mambo kama haya. Tunataka watu walete hoja za msingi, watujengee hoja, watukosoe na Rais mwenyewe amekwishasema akosolewe kwa hoja. Tena amesema wakifanya vikao vyao wakisema ya kwao, Rais ametuzuia amesemea tutoe hoja tusitukane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaombe Wabunge wa Chama cha Mapinduzi hii ni dalili nzuri kwamba watu hawa hawawezi kupewa nchi, wametuonesha wenyewe. Mheshimiwa Rais ajiandae 2025/2030 njia iko wazi, abebe msalaba huu, sisi tumemuamini na wanawake wanaweza na chenji inabaki. Tunataka tumpe heshima Mheshimiwa Rais ili atoe nafasi kwa wakina mama wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni mwanamama Watanzania tunakuamini, Wabunge tunakuamini, hauwezi kuleta hapa mkataba ambao ni wa hovyo. Wewe ni Wakili Msomi, Daktari wa Falsafam PhD ya Sheria, haiwezekani. Kwa hiyo, wasituone kwamba sisi Wabunge wa CCM hatuna akili sio kweli, tunajua sana. Hiyo kazi ambayo wanafanya kwenye mitandao, hayo mambo ambayo wanapotosha tuna uwezo mkubwa kuliko wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais katika jambo hili atuache tushughulike na watu kidogo, tulikuwa tumepoa. Tunaweza kufanya ambayo wanafanya zaidi yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Waitara, sekunde 30 malizia.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nataka niwambie watu wa Tarime, huyu mama Mheshimiwa Rais ndiye aliyesema mgogoro wa hifadhi kule utakwisha; fidia ya Nyamongo; mama huyu ndiye amesema; kulikuwa na viongozi wa ajabu ajabu ametuondolea; mama huyu ameahidi miradi mikubwa ya nchi; mama huyu ndiye amepeleka VETA Nyamongo; na mama huyu ndio ameahidi zile ambulance. Tunapoongeza mapato ya bandati maana yake madarasa yatajengwa, vijana watapata ajira na mradi wa maji kutoka Rorya – Tarime – Nyamwaga – Nyamongo utakamilika, hizi ndizo fedha ambazo zimekuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo watu wa Tarime, watu wa Mara na Watanzania waelewe Wabunge wa CCM wanaunga mkono mambo ya msingi na hapa tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nataka niwambie Watanzania...

SPIKA: Mheshimiwa Waitara, ahsante sana.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, haiwezekani Mbunge wa Chama cha Mapinduzi uje ukae humu ndani uje upinge hoja ya Mama Samia utakuwa hujitaki. Ukitaka kutupinga toka nje, tafuta chama kingine, hii ni hoja ya Chama cha Mapinduzi, ni hoja ya Mama Samia lazima tumuunge mkono iwe jua, iwe mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono azimio kwa nguvu zote na Watanzania watuelewe, watuunge mkono, tukachape kazi. (Makofi)