Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie azimio hili ambalo liko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kusema hakuna mtu anapinga uwekezaji kwenye Taifa letu. Hakuna mtu ambaye haoni umuhimu wa kuwekeza leo kwenye Taifa letu hasa kwenye bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa niwakumbushe Wabunge wenzangu, kipindi tuna Kambi Rasmi ya Upinzani hapa Bungeni ushauri wetu miaka yote tulisema bandari yetu inaendeshwa kwa hasara na tukashauri kwamba ni vizuri tukaona utaratibu mwingine wa kuruhusu sekta binafsi. Leo tunapotaka kushauri hatusemi shida ni uwekezaji, tunachotaka kujua masharti ya kwenye huo uwekezaji yana faida gani kwa Taifa letu, yana faida gani kwa Watanzania, na yana athari zipi kwa Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sio mwanasheria kama wewe na vifungu vilivyopo inawezekana ni suala la kutoelewa hivyo hivyo huko nje. Ilikuwa ni suala la elimu lifanyike kwanza kabla ya kuleta hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitazama malalamiko ya Watanzania ndio waliotufanya sisi tuko hapa leo. Bandari tunayoizungumzia ni bandari yao. Tunaofanya maamuzi leo...

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani, samahani kidogo. Waheshimiwa Wabunge naongeza nusu saa ili tuweze kukamilisha kazi hii. (Makofi)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, jambo lolote lenye nia njema linakwenda na dhamira njema. Inawezekana wengi walioko huko ambao wanalalamika ni kwa sababu aidha kama tunavyosema hapa mtu akikiona Ibara ya 23(4) kwa hali ya kawaida Ibara hii ya 23 ya Mkataba wetu na hapa ndani tumeona Wabunge wanavyochangia wapo wanaosema si mkataba bado wanazungumzia makubaliano. Huko nje unaweza ukaona pia na wao wanaelewa nini kuhusu jambo hili linalozungumzwa leo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nia ni njema ya hili jambo, yale maeneo ambayo tunasema yanahitaji kutolewa ufafanuzi, yatolewe ufafanuzi kwa nia hiyo hiyo njema.

Mheshimiwa Spika, ...

SPIKA: Mheshimiwa Aida, kwa nia hiyo hiyo njema hicho kifungu ulichokitaja kifungu kidogo cha (4) ulichokitaja, huko nje wanakisema kana kwamba ni Tanzania pakee ndio inayobanwa na ndio haiwezi kutoka, lakini kifungu hiki hapa kinasema; “The State Parties is shall...” maana yake Dubai pamoja na Tanzania kila mmojawapo haruhusiwi, ukikisoma chenyewe tu peke yake, lakini wao wanakiweka kana kwamba ni Tanzania peke yake ndiyo haiwezekani. Kwa hiyo, nadhani na wewe unacho hapo, kinazungumzia pande zote mbili.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, eneo linalowekezwa ni Tanzania na wanaoumia ni Watanzania kwa sababu wanajua athari zitakzotokea sio kwao, yaani endapo kama itatokea wao labda wamechukua muda mrefu, kwa sababu ni suala la uelewa kama ninavyozungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, unaposema hawatoruhusiwa kujitoa iwe Dubai au Tanzania, wakati huo jambo la kwanza ambalo Watanzania walitamani kuliona ni kwamba wanakuja kuwekeza wapi na kwa muda gani? Hayo mambo kama yangetolewa ufafanuzi mapema yasingetufikisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nia hiyo hiyo njema ninaishauri Serikali, wananchi wanapotoa mawazo yao wachukuliwe kwa nafasi yao kama Watanzania wajibiwe kikamilifu ili waweze kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hiyo hiyo kwamba kwa muda ambao mimi nimekuwepo kwenye Kamati hii iliyoundwa…

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: Naisubiri

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nilitaka tu kumpa taarifa dada yangu Mheshimiwa Khenani ambaye ninamheshimu sana. Bunge hili halipingani na Watanzania wanachokisema, Bunge hili linasema tunamuonya muhuni mmoja ambaye yeye mwenyewe anamjua ambaye wanawake wa hapa, akina mama wametengenezwa kwa miaka 30 kwa sababu ya maslahi yake binafsi leo kila siku wako mahakamani. (Makofi)

Kwa hiyo, Bunge hili linamzungumzia huyo, lakini mawazo ya Watanzania Bunge hili limeyapokea na wakati wote umewasikia Wabunge hawa, lakini huyu muhuni mmoja ni lazima tushughulike naye. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, kulingana na uzito wa jambo lililopo mbele yetu naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kuwapongeza Watanzania waliotoa maoni yao na wakasema hofu zao na ndio hofu ambayo mimi Mbunge ninayezungumza hapa ni kubwa sana kwangu.

Mheshimiwa Spika, unapozungumzia hii Ibara ya 23 kama kweli kuna loophole ambayo sisi tunaweza tukafanya negotiation kulikuwa na haja gani ya msisitizo huu kwenye hii Ibara ya 23(4)? Hiyo ndiyo hofu ya Watanzania wengi, msisitizo ule ulikuwa ni wa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tuna haki ya kutoa maoni yetu kwa mujibu wa Katiba yetu ambayo ndio msingi, leo tunasema kutakuwa mikataba mingine, sawa tunakubali hiyo mikataba mingine ambayo itaendelea labda mkataba wa pili au wa tatu, lakini msingi wake ndio huu tunaoujadili leo.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nilichokuwa nataka kufahamu, kama ndio kuna eneo ambalo tunaweza tukaruhusu mazungumzo yaani tumeona kwenye mkataba hawa DP World kwamba kuna shida fulani ambayo sisi tunaona labda upande wa makusanyo au eneo ambalo tumewapa. kama tunaweza kukutana nao tena kuzungumza, Watanzania wanataka kujua ni vizuri sasa Serikali iseme eneo hili pamoja na kuandikwa hii ibara, ibara hii inatupa nafasi nyingine. Ni Watanzania wangapi wanajua kuhusu hilo jambo?

SPIKA: Sawa na ahsante sana, eneo la makusanyo ni mikataba ijayo. Kwa hiyo, sisi hatujui.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ndilo hilo ninalizungumzia.

SPIKA: Kulikuwa kuna taarifa nyingine kutoka kule nyuma, Mheshimiwa Mnzava.

TAARIFA

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba nimpe tu taarifa mzungumzaji rafiki yangu Mheshimiwa Aida kwamba kifungu hiki cha 23 ukikisoma vizuri usiposoma cha (4) tu ukaanza kusoma kile cha (1) mpaka cha (4) hakina shida yoyote, na kifungu hiki kinachosomeka hapa ndivyo kinavyosomeka hivyo hivyo kwenye makubaliano ya aina hii ya Mkataba wa Bomba la Mafuta na ni kifungu cha 24(4) hivyo hivyo, nakushukuru. (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana, Mheshimiwa Aida Khenani unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa yake, tunawezaje kusaini kitu ambacho hatukijui? Ndio hofu yangu mimi hiyo, na Watanzania wengine waondolewe hii hofu.

Mheshimiwa Spika, wakati tuna...

SPIKA: Kwa sababu wewe upo hapa ndani, mimi nataka kuindoa hiyo hofu yako, wewe una hofu gani?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, na muda wangu bado upo?

SPIKA: Unalindwa, ukizungumza na mimi unalindwa ambao haulindwi ni ule kule. Hofu yako mimi nataka niiondoe wewe una hofu gani Mheshimiwa Aida?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, hofu kubwa iliyopo kwanza kuna mikataba ya hovyo mingi kama Taifa ambayo tumewahi kuingia huko nyuma, mingi sana. Kwa hiyo unapokuja mkataba mwingine mkubwa kama huu, lazima hofu iwepo, lakini Watanzania leo tunapotaka kupitisha hili azimio wanayo historia na kauli ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliyoizungumza, leo tulikuwa na haki ya kuwaambia Watanzania alichokizungumza Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kina utofauti gani na hiki ambacho leo tunakwenda kukiingia? Lazima watu wajue, wana kitu gani leo tunapokwenda kupitisha kitu kama hiki.

SPIKA: Mheshimiwa Aida, mimi nakusiliza ili hofu ile ya Watanzania natamani kwa sababu mwishoni ile Kanuni zetu ya 111 inatupa nafasi kama Bunge kupitisha mkataba huu, kupitisha baadhi ya vifungu au kuukataa kabisa. Sisi kama Bunge tunaruhusiwa vyote vitatu. Ninavyotaka mimi nielewe hofu yako ili na Watanzania tukitoka hapa tuwe tumeelewana. Ukiiweka kwa ujumla mimi nina nafasi ya kufafanua hofu yako, ya kwao naweza nisipate, nafasi lakini na wewe ukiweka jumla basi nitakuacha na wewe utatoka hapa ndani ukiwa na hofu wakati kura utapiga wewe hapa ndani. Karibu Mheshimiwa.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kwamba kura yangu ni ya hapana. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, haya mazingira tunapoyaweka hapa hawa ambao wanatamani kuelewa ni Watanzania, maamuzi yanayokwenda kufanyika yanafanyika kwa niaba ya Watanzania na ndio maana nasema hili jambo lilihitaji mjadala mpana sana kwa maslahi ya Taifa, mpana sana ili watu ambao wanaweza kutoa ushauri wao, watu ambao wanatakiwa kuondolewa hofu zao waondolewe.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia hata kwenye wadau tukiwa tu kwenye Kamati, namna ambavyo hili tangazo lilitolewa la hawa wadau, wadau tuliowapata ni wachache sana kiasi kwamba tulipaswa tupate mawazo ya watu wengi ili kama Bunge tujue tunasimama wapi. Ni kweli sisi hatuhusiki na kusaini mkataba, lakini kama Bunge ni wajibu wetu kuisimamia Serikali na kuikosoa Serikali ndio maana yale maeneo ambayo tunaona kwetu bado yana hofu, ambayo bado yana changamoto lazima tuyaseme.

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi)

TAARIFA

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, si utaratibu wa mimi kusimama, lakini nilitaka nimsaidie tu Mheshimiwa Aida.

Mheshimiwa Spika, hiyo hofu aliyokuwa kwenye article 23(4) alitakiwa akisome mpaka mwisho. Anakisoma maeneo yale ambayo anayaona ni magumu, lakini akija mpaka mwisho kinaeleza vizuri tu; Notwithstanding the foregoing, any dispute between State Parties in respect of such circumstances shall be dealt with accordance with the requirements of Article 20 of this agreement.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo kifungu hiki kinasomwa pamoja na article 20 ambacho ni dispute ya settlement, kwa hiyo hofu hiyo dada yangu itoe. Tatizo lolote litamalizwa na article 20.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani unaipokea hiyo taarifa?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na taarifa zinazoendelea na kwa sababu kiongozi wangu pia namheshimu sana nimepokea taarifa yako, lakini nataka kusema kama umesema sheria zitakazotumika kusuluhisha migogoro ni za Tanzania kwa nini tunakwenda kusuluhisha South Africa? Hayo ndio maeneo ambayo Watanzania wa kawaida wanataka kujua mambo kama hayo. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, jamani too much.

MBUNGE FULANI: Mnaogopa nini?

SPIKA: Taarifa zimeshaisha tatu, kwa hiyo, sasa hivi mimi ndio naruhusiwa kuongea naye.

Mheshimiwa Aida wacha nikufafanulie kwenye hilo eneo ni hivi, huu mkataba kwa sababu ni kati ya nchi mbili; nchi mbili huwezi kuchagua sheria za nchi mojawapo, unachagua wewe nchi ipi duniani huko ama sheria zipi huko duniani mtazitumia, kwa hiyo hofu hiyo nikuondoe kwa namna hiyo kwa sababu mkataba huu ndio unaozungumzia mtakwenda Afrika ya Kusini, ile mikataba mingine ile humu nako kumeshatajwa kwamba tutatumia sheria zetu, wala hatutoki popote. Hata kama tutaenda huko tutatumia zetu.

Nimeona nikufafanulie hapo si umesema una hofu kwa hiyo na mimi nataka nikutoe kabisa hofu yako hata kama utapiga kura ya hapana ni haki yako, lakini hofu iwe imekuondoka.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na niendelee kusema kwamba kwa sababu ni haki yetu kusema, kushauri, maamuzi najua tutafanya kwa wingi mtaamua, lakini lazima tutaelekeza kwenye yale maeneo ambayo tunaona kwetu yana changamoto. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mwenyekiti wangu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kutoa maoni kama Mtanzania, kwa kuonesha kwamba mambo haya lazima mbele tuangalie kuna mambo yanaweza kutokea, ni haki yake kama Mtanzania, kama kiongozi wa chama na sisi tunasema tusipotoshwe kama inavyosema hukio nje wanapotosha. Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe hakuzungumza juu ya mgawanyo wa Tanganyika na Zanzibar, tusipotoshe mambo haya.

SPIKA: Sekunde 30 malizia.

MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Spika, watu wana clip walisikia, wasipotoshe kwa makusudi yule ni kiongozi wa chama anastahili heshima yake kama mnavyoheshimu viongozi wengine na siyo lugha zinazotumika humu ndani.

SPIKA: Ngoja jamani mimi namlinda mchangiaji, Mheshimiwa Aida hawa wamepotosha, wewe unaujua ukweli hebu sema alichosema ili na wewe iingie kwenye record kwamba ndicho alichosema.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana alichozungumzia kwamba kwenye maamuzi haya, kwenye mkataba huu ni vizuri kuchukua tahadhari, ni vizuri kuchukua tahadhari na tahadhari ni jambo la kawaida kabla hujafanya maamuzi, lazima uchukue tahadhari.

SPIKA: Mheshimiwa Aida ngoja, Waheshimiwa Wabunge mimi namlinda.

Mheshimiwa Aida mchango uliokuwa unasema watu wamepotosha Wabunge wengine ni kuhusu hoja ya Mheshimiwa Rais kutoka Zanzibar na Mheshimiwa Waziri kutoka Zanzibar, pale wewe umemsikia nini akisema Mheshimiwa Mbowe? Rekebisha hiyo kwa sababu umesema wapepotosha, sasa mimi nataka kuelewa kutoka kwako wewe ulivyomsikia kasemaje hoja hiyo ili Taarifa zetu za Bunge zikae sawa.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, alisema inaweza kuleta hisia na clip hapa ninayo.

SPIKA: Basi wako sahihi, amesema yeye...

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, hapana.

SPIKA: Inaweza kuleta hisia, ni kama wewe ulivyosema hofu zao kwani tumebishia za wananchi.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika,...

SPIKA: Aah! Mheshimiwa Aida umesema amesema zinaweza kuleta hisia maana yake amesema inaweza kuleta hisia, hisia zinaweza kuwa zake au za watu wengine. Kwa hiyo, yeye ndio kazisema, kwa hiyo wako sahihi hawajapotosha alichokisema.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, jambo hili likienda hivyo, siyo sawa.

SPIKA: Mheshimiwa Aida ujue unaposisitiza nitakwambia ufungue kwenye simu tumsikie alichosema.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, niko tayari kufungua.

SPIKA: Fungua. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, wakati anaendelea kutafuta... kaa tu Mheshimiwa tafuta taratibu wala hatuna haraka.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, sasa hivi tu ipo tu hapa.

Mheshimiwa Spika, ipo tayari.

SPIKA: Haya tuwekee.

Shusha hiyo microphone halafu weka. Weka sehemu hapo ya microphone kama mimi ninavyozungumza tutaisikia, siyo hapo unapoweka microphone unakozungumzia wewe huko.

(Hapa sauti iliyorekodiwa ya Mhe. Freeman Aikael Mbowe ilisikilizwa Bungeni)

“Tunawaletea uchambuzi wa awali wa mkataba wa ushirikiano kwa ajili ya uendeshaji na uboreshaji wa bandari Tanzania kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dubai”

SPIKA: Sasa tupeleke kwenye hoja yake kuhusu Rais kutoka Zanzibar, usituwekee yote hatuwezi kuwa na huo muda wewe tutafutie kwenye hoja yako uliyosema Wabunge wamepotosha kwenye hoja yake ya kuhusu Rais kutoka Zanzibar na Waziri kutoka Zanzibar, itafute tu taratibu mimi nimekupa muda. Itafute tu taratibu.