Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI: Mheshimiwa Spika, naomba nitoe shukrani nyingi sana kwako kwa kunipa heshima kubwa ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika Bajeti Kuu ya Serikali, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema sisi Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako tukufu, lakini kubwa nikupongeze na kukushukuru wewe kwa umahiri wako, uhodari wako, uzoefu wako, kwa kweli unaliongoza Bunge vizuri, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze Waheshimiwa Wabunge na tujipongeze Waheshimiwa Wabunge wote tulivyo mpata Mheshimiwa Spika huyu, ahsanteni tujipongeze Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Spika kaka yetu Azzan Zungu kwa kazi nzuri anayofanya ya kukusaidia wewe. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuchangia kwa namna hii toka nizaliwe naomba nianze mchango wangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nikipongeze sana chama chetu Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri kinachofanya kutengeneza Ilani inayotekelezeka kwa mpango wa bajeti tunayokwenda kupitisha leo na kipekee nimpongeze sana Mwenyekiti wa chama chetu Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukiongoza vizuri Chama cha Mapinduzi. Lakini kipekee nimpongeze kaka yetu Comrade Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi anavyomsaidia Mheshimiwa Mwenyekiti wa chama chetu na nimpongeze Comrade Daniel Chongolo, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo anasimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitachangia kwa bajeti kuu ya Serikali kama ambavyo nimeomba, lakini kubwa naomba nianze kwa kweli kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuandaa bajeti kubwa na nono ambayo haijawahi kutokea kwa takribani miaka yote toka nchi yetu imeumbwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakwenda kujadili na kupitisha bajeti hii kubwa ya shilingi trilioni 44.14; ni bajeti kubwa sana inayokwenda kujibu na kutatua kero za Watanzania wanyonge. Hongera sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa kutuleta bajeti hiyo kubwa. Lakini Waheshimiwa Wabunge mnakwenda kuvunja rekodi kuwa Wabunge wa kwanza kupitisha bajeti kubwa ya namna hii, hongereni sana kwa kupitisha bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na bajeti; kwa takribani miaka minne iliyopita bajeti ambayo tumeipitisha katika Bunge hili ukiangalia na ukilinganisha na bajeti ya leo ni kubwa, hii bajeti inakwenda kuisha maradufu kuliko za miaka iliyopita. Mwaka 2019/2020 tulipitisha katika Bunge hili hili takribani shilingi trilioni 29.5 na tukapeleka fedha za maendeleo shilingi trilioni 9.3, mwaka uliofuata mwaka 2020/2021 tukapitisha bajeti katika Bunge hili hili shilingi trilioni 34.8 na tukapeleka kwenye fedha za maendeleo shilingi trilioni 13.3, mwaka 2021/2022 tukapeleka bajeti shilingi trilioni 36.84 na tukapeleka kwenye miradi ya maendeleo shilingi trilioni 13.87. mwaka jana kwa maana mpango unaomalizika tulipitisha trilioni kama mnavyofahamu shilingi trilioni 41.48 na zilizokwenda kwenye miradi ya maendeleo ni shilingi trilioni 15.00.

Mheshimiwa Spika, mwaka huu bajeti hii ikipita ni shilingi trilioni kubwa zaidi ya shilingi trilioni 2.8 zaidi ya bajeti iliyopita ambayo ni takribani asilimia 7.0 ya bajeti zilizopita. Tujipongeze sana Wabunge, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumze sasa kwenye miradi ya kimkakati, tumeona kwenye bajeti nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mwigulu Madelu Nchemba hongera sana kwa kazi kubwa. Wewe na timu yako Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mwigulu kwa sababu alivyoisoma bajeti ya juzi imetatua na inakwenda kujibu kero za Watanzania wanyonge. Hongera sana kaka yangu Mwigulu Mungu akutangulie, tuna matumaini makubwa bajeti ikitekelezeka maana yake utafanya kazi ya kukumbukwa kwa dunia nzima, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze sasa kwa miradi michache ya kipaumbele. Tumeona Mradi wa SGR, tumeanza kuutekeleza takribani miaka minne iliyopita, lakini kasi tunayokwenda nayo hatuna budi kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha kudhihirisha kwamba utekelezaji wa mradi huo utakamilika kama ulivyotarajiwa na tunaona miradi mikubwa kama ambavyo ameweka dhamira yake wazi kwamba kazi inaendelea tunamhakikishia sisi Waheshimiwa Wabunge na mimi ninasema kwa niaba yangu na wananzengo ambao wanatusikiliza, Mheshimiwa Rais kazi anayoifanya ni ya uzalendo sana. (Makofi)

Ndugu zandu Waheshimiwa Wabunge hii treni ya SGR, ya mwendo kasi ikitekelezwa kama ambavyo tumepanga nimeona kwenye bajeti ilivyosomwa katika nchi za Afrika Mashariki itakuwa ndio treni ya kwanza kutembea kuliko nchi nyingine ambazo zinatuzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni treni ambayo tumeona bajeti yake ni kubwa, lakini utekelezaji wake unakwenda vizuri. Nimesikiliza vizuri sana bajeti ya Mheshimiwa Mwigulu na Waziri wa Ujenzi kwamba tumeshakamilisha kipande cha kilometa 300 kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na tunakwenda kukamilisha umbali wa kilometa 822 kutoka Morogoro kwenda Makutopora na kutoka Makutopora kwenda mpaka Tabora takribani kilometa 371 zinakwenda kutekelezweka na itakamilika si muda mrefu, lakini kutoka Isaka kwenda Mwanza kilometa 341 inakwenda kukamilika na kutoka Isaka kwenda Tabora 342 zinakwenda kukamilika, kutoka Tabora mpaka Kigoma kilometa 506 zinakwenda kukamilika. (Makofi)

Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, mnafahamu wenzetu majirani wetu wanajiandaa pia kujenga SGR, lakini nataka niwape taarifa kwamba Rwanda hawajaanza kutumia, Burundi hawajaanza kutumia, Kenya hawajaanza kuitumia, sisi chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan tunakwenda kuwa watu wa kwenza kutumia treni ya mwendokasi ya SGR ni jambo la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Lakini hiyo haitoshi na nikapenda niwaambie Watanzania treni hii nadhani tumeshapata taarifa kwamba ina uwezo wa kukimbia umbali wa kilometa 160 kwa saa. Sasa hesabu kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza ambapo ni kilometa 1,112 itakwenda masaa mangapi? Kwa hiyo, ni masaa machache sana. (Makofi)

Kwa hiyo, Watanzania tujiandae kuitumia ili iweze kulrta tija kwenye shughuli zetu za uchumi. Lakini nitoe rai tu kwa wasimamizi kwamba isimamie kwa haraka, ikamilike haraka ili Watanzania waanze kuitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, SGR napenda nizungumze eneo hili kwa upana kidogo, itakuwa inatumia umeme na ni mara ya kwanza sisi hapa Bara la Afrika ukiondoa Ethiopia ambao walianza kuitumia kwa umbali wa kilometa 752. Ukiondoa Ethiopia, Morocco, Afrika ya Kusini na Nigeria nchi inayofuata kwa nchi za Afrika ni Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhihirisha kwa nchi za Afrika Mashariki kuwa Rais wa kwanza kuanza kulitembeza na kulikimbiza li-SGR tukiwa sisi Watanzania. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nizungumze mabehewa yatakayoanza kufanya kazi kwa nilivyosoma katika Taarifa za Serikali. Kutakuwa na mabehewa takribani 400 ya abiria lakini mabehewa 59 yataanza kuingia na mabehewa 14 yameshaanza kuingia. Mheshimiwa Waziri wa ujenzi na wewe hongera sana Kaka Mbarawa kwa kusimamia kwa ubora kabisa kazi hiyo. Lakini hiyo ni kazi ya Mheshimiwa Rais ameifanya na sisi watendaji tumuunge mkono kwa kuharakisha utekelezaji huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mabehewa haya yatakuwa na uwezo wa kutunza umeme kwa masaa manne bila kukatika hata kama umeme utakatika sehemu zingine. Kwa hiyo, ni jambo la kheri ni uhakika kwamba yatafanya kazi lakini mabehewa ya mizigo yatakuwa takribani 1,430. Sasa elewa ni mizigo mingapi ya Watanzania itabebwa katika mabehewa yale kwa muda mfupi. Kwa hiyo, ni kazi nzuri naomba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais na Serikali tukamilishe mradi huu na mradi huu ndugu zangu Wakenya wanatengemea kuanza kuujenga mwakani na Burundi na Uganda na sehemu nyingine mwaka 2025. Kwa hiyo, miaka mitatu hii tutakuwa tunaongoza katika ulingo wa kuhudumia hapa Afrika Mashariki, Tanzania tukiongoza kukimbiza na kutembeza li-treni la mwendo kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere; naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais nimeona fedha zilizotolewa kwenda kukamilisha mradi ule kwa mwaka jana takribani shilingi bilioni 869 ambazo tuna matarajio kwa muda uliopangwa mradi huu unakwenda kukamilika. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira hiyo ya kutoa fedha na wewe Mheshimiwa Mwigulu Nchemba usingekuwa unatoa fedha mradi usingefika kiwango hicho, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nishati Kaka yangu January Makamba kwa kusimamia vizuri pamoja na timu yake pamoja na TANESCO wanafanya kazi nzuri ni matumaini yetu kwamba mradi ule unakwenda kufufua uchumi kwa kiwango cha juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania mnaonisikiliza, Mradi huu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mradi mkubwa sana. Kama tulivyo kwenye SGR kwa nchi za Afrika Mashariki ndio bwawa kubwa peke yake hakuna bawawa lingine linalozalisha umeme wa namna hii na kwa nchi za SADC ni bwawa la tatu kwa ukubwa ikiongozwa na Bwawa la Mambilla lililoko Nigeria na Caculo Cabaça la Angola na linafuata la Tanzania. Kwa Afrika nzima ni bwawa la nne ukiondoa la Ethiopia ambalo ni Renaissance, la megawati 6,450 na duniani kote ni bwawa la 60. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tuelewane, sasa elewa dunia kuna nchi ngapi? Kwa hiyo, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa Afrika anaongoza kwa kuwa na bwawa kubwa kwa nchi za Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Rais hongera sana kwa kazi hiyo tunakwenda kufufua uchumi tunakwenda kumaliza changamoto za kinishati tukikamilisha bwawa hili pamoja na miradi mingine itakapo kamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee niwapongeze Serikali na Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge, na ninyi Waheshimiwa Wabunge mnakwenda kuingia kwenye rekodi ya Bunge Hansard zitaandika kwamba militekeleza miradi hii mikubwa kwa niaba ya Watanzania. Mjipongeze sana kwa kazi nzuri tunayoifanya. Bwawa la Mwalimu Nyerere likikamilika litatuongezea umeme, kwa sasa nimeona kwenye taarifa kwamba tuna takribani megawati 1,872 kwa uwezo wa juu, ingawaje mahitaji yetu nilivyoona kwenye taarifa ni megawati 1,432.05 lakini tukikamilisha tutakuwa na takribani megawati 4,193 ukijumlisha na miradi mingine. Maana yake nini? Mwaka 2025/2026 miaka inayokuja michache mahitaji yetu ya umeme yaweza kufikia megawati 2070 kwa sasa mahitaji yetu ni megawati 1,432.05. Kwa hiyo, tutaweza kujitosheleza kuwa na umeme nchini, lakini na kuwasambazia majirani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Waheshimiwa Wabunge leo hii Kenya ana jumla ya megawati 2,722 anahitaji umeme takribani megawati 500; kwa hiyo, tunaweza kumuuzia. Rwanda ana megawati 230, Burundi ana megawati 86, Zambia ana megawati 1,472; sisi tunakwenda kuwa na megawati 4,198 mnasubiri nini kupiga makofi kwa Mheshimiwa Rais wetu, ni kazi kubwa ameifanya. Lakini ni ninye Waheshimiwa Wabunge na Serikali na wananzengo... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, sekunde 30 malizia sentensi yako.

MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI: Mheshimiwa Spika, naomba niongezee dakika mbili. Mradi huu unakwenda kujibu kero za Watanzania, mahala ambapo kuna changamoto za umeme. Tumeelewa bado kuna vitongoji takribani 36,101 lakini mradi unakwenda kukamilisha vitongoji vya Wabunge takribani vyote, hata kwako pale Igomba, Itonya na Itua ambako kuna kero wanakwenda kupelekewa umeme. (Makofi)

Kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba Watanzania wengi watapata umeme, hata Gezaulole kwa Mheshimiwa kule Kigamboni watapata umeme, mpaka kule Itonya na maeneo mengine ambayo nimesema mpaka Katubuka watapata umeme. Kwa hiyo, ni matumaini hata kule Chato kwenye Majangala watapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu ni mkubwa sana ni mategemeo yetu kwamba utakwenda kujibu kero za Watanzania.

Naomba niombe kidogo kwa sababu hela hizi ni nyingi zinakwenda kwa wananchi takribani kujibu kero za Watanzania wanyonge na wakulima wanyonge. Ninajua mradi huu utakwenda kwa Watanzania milioni 61; utakwenda kwa ng’ombe tulionazo milioni 6.6; kwa mbuzi milioni 21.6; kwa kondoo milioni 92.7; pamoja na nguruwe milioni 3.7; na mifugo mingine, lakini tutatatua kero za wakulima wetu kwa ajili ya kuwapelekea kilimo cha umwagiliaji. Naona Mheshimiwa Bashe umefanya kazi kubwa sana, peleka miradi ya umwagiliaji kule Chato, maeneo ya Makurugusi, Ilyamchele, Nganza, Rubambangwe, Nyambogo, Katende, Mongela pamoja na maeneo mengine ambayo hayajapata mradi wa umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, Mheshimiwa Mbarawa tumepitishia bajeti kubwa sana; kuna barabara ya kero kubwa ya muda mrefu kule Jimbo langu la Chato na wanachato wananisikia, kutoka Nyamirembe - Gatini mpaka Katoke yenye umbali wa kilometa 51.0 inayojengwa kwa kiwango cha lami. Naomba uanze kutekeleza miradi hiyo kwa sababu Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 2.3 na tayari umezipokea. Tangaza tender, peleka ma-bulldozer wananchi wa Ichwankima wanaopitiwa na barabara hiyo, wananchi wa Busarara, wananchi wa Nyambiti, wananchi wa Kalwelezo, wananchi wa Kazunguti, wananchi wa Kasenka mpaka Katoke mradi uweze kukamilika kwa kiwano cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa naomba kipekee, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, tumtakie kila la kheri sisi pamoja na Watanzania wote Kwenda kutekeleza mradi huu muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, nashukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, ahsanteni sana.

MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono, ahsante sana. (Makofi)