Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Spika, mchango wangu mimi kwanza naunga mkono bajeti, kwa sababu kuna miradi mikubwa ya Musoma Vijijini ambayo inaanza mwezi wa nane, barabara na kilimo cha umwagiliaji na miradi mingi, kwa hiyo, Musoma Vijijini tuunge bajeti hii mkono, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu mimi utakuwa una takwimu, mjitayarishe kwa takwimu. Ni kwamba ninachangia namna ambavyo uchumi wetu unaweza kukua kwa haraka. Sasa hivi tuko kwenye kati ya 4% na 5%; tulikuwa tuko kwenye 7% tukashuka kwa sababu nyingi zilizoelezwa na kuondoa umaskini hii ni wachumi wa dunia magwiji wote wanasema uchumi ni lazima ukue zaidi ya 8%. Kwa hiyo, kati ya 8% mpaka 10%, ndio mchango wangu mimi; mipango na ukuaji wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipanga kwenye maendeleo ya miaka mitano ikifika mwaka 2025 tuwe na GDP per capita ya dola 3,000 na kufika huko kwa mahesabu yote wanaojua uchumi, wanaojua mambo ya umeme unahitaji umeme wa megawati 10,000; kwa hiyo, umeme haujatosha.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hali ilivyo ni kwamba GDP per capita yetu mwaka jana ilikuwa dola 1,253; jirani yetu alikuwa GDP per capita dola 2,278; nimechukua Algeria ambayo ina gesi ina GDP per capita dola 4,315; Seychelles naichukua kwa sababu ina elimu bora sana Afrika halafu ndio yenye uchumi bora, ina GDP per capita zaidi ya dola 19,000. Nini tufanye uchumi wetu ukue kwa 8% mpaka 10%?

Mheshimiwa Spika, cha kwanza kabisa ni umeme, alipoishia Dkt. Kalemani, lakini tunahitaji umeme wa uhakika, tunahitaji umeme mwingi na umeme wa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa vipimo vya umeme duniani na hivi ndio vipimo vya kiuchumi, sio kusema unaweza ukafikisha umeme kwenye kijiji, kwenye kitongoji hata ukafikisha vitongoji vyote suala linakuja ni wangapi kwenye hicho kitongoji wanatumia huo umeme. Hicho ndio kipimo cha kiuchumi (electricity consumption power per capita). Vilevile ukifikisha hapo unaweza ukasema wangapi wamepata fursa kwenye hicho kijiji kupata umeme (access to electricity). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba ripoti zetu zinavyotoka Serikalini lazima zitaje hizo takwimu, ukisema tu vijiji na vitongoji hujajibu hoja ya kiuchumi. Sasa angalia mambo ya umaskini na utumiaji wa uchumi. Nimewatajia Seychelles GDP per capita yao zaidi ya dola 19,000; power per capita ni units 4,514 tunaiita sisi unit, lakini ni kilowatt hour. Unakuja Algeria yenye gesi, umeme wanaotumia power per capita ni units 1,600; unachukua Kenya ambayo inatuzidi GDP per capita, power per capita yao ni unit 170 na Tanzania ni 103, hizi ni kidogo ni chache kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Tanzania tufanyeje? Cha kwanza tuongeze umeme na vyanzo vya umeme viwe vingi, siyo kimoja. Tatizo letu ukisema vyanzo vingi wengine wanasema unachukia bwawa, ni watu wasiokuwa na uelewa. Tunataka vyanzo vingi na umeme wetu utokane na natural gas, utokane na maji, utokane na makaa ya mawe. Halafu unaenda kwenye renewables yaani geothermal, solar, wind, biomass, biogas, tides and waves. Hapo lengo letu ni kufikisha umeme wa megawati 10,000. Hapo ndio tutaanza kusema sasa uchumi unaanza kukwamuka.

Mheshimiwa Spika, bei ya umeme nayo napendekeza ipunguzwe, sasa hivi umeme majumbani ni US cents 9.7 kwa unit, viwandani ni unit 10 ndio zinatumika US cents 10 kwa unit. Kenya wako juu, lakini hii siyo sababu ya kufanya sisi tusipunguze umeme kwa sababu eti nchi za Afrika Mashariki umeme bei iko juu. Kwa hiyo, bei ikiwa chini watumiaji watakuwa wengi. Sasa ili uchumi ukue kwa kasi tunahitaji umeme mwingi na tufikishe zaidi ya megawati 10,000.

Mheshimiwa Spika, kingine cha pili ambacho kitafanya uchumi ukue kwa kasi na umaskini uzidi kutokomea, tuna mambo ya kilimo sawa, mambo ya madini sawa, mambo ya utalii sawa. Kuna kimoja ambacho lazima bajeti inayokuja iwekee mkazo ni uchumi wa gesi. Uchumi wa gesi ni hivi, natoa Algeria ndio ina-export LNG ya kwanza Afrika nzima, ina-export tani 29.3 kwa mwaka. GDP yake niliyowatajia zaidi ya dola 3,000. Qatar ndio ina-export LNG ya kwanza duniani ni tani 80,000,000. GDP per capita ya Qatar ni zaidi ya dola 84,000.

Mheshimiwa Spika, sasa Tanzania tufanyeje? Lazima tuongeze mambo ya gesi. Sasa hivi tunazo hizo trilioni 57.5 ni nyingi, lakini hatujafanya kazi zaidi. Algeria wanazo 159 TCF, Mozambique majirani zetu wanazo 100 mpaka 200 TCF. Kwa hiyo, Tanzania tufanye nini? Lazima tutafute mafuta na gesi kwa bidii zaidi na ndiyo maana mimi mpaka leo hii naamini kabisa kwamba TPDC haifai kufanya kazi ya kuuza mafuta ambayo inaweza kufanywa na kila mtu. Lakini kila mtu hawezi kutafuta mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, Mozambique wanaanza ku–export LNG kwa gesi inayotoka Ruvuma Basin. Sasa sisi tuko na wao kwenye Ruvuma Basin. Tunapaswa kuiuliza TPDC huko tuna gesi kiasi gani? Tuna mafuta kiasi gani? Maana yake wenzetu kwenye hiyo basin wameshapata over hundred trillion cubic feet of natural of gas. Sisi huku chini hatujafanya explorations. TPDC iende huko, iache kuuza mafuta. Hatujatafuta mafuta kwenye Ziwa Tanganyika, kwenye Ziwa Nyasa, kwenye Ziwa Rukwa na muhimu zaidi tena wewe Spika ni mwanasheria, huko tunakoenda kuna hizi resources zitakuwa kwenye mipaka ya nchi mbili, kwa hiyo, TPDC ina kazi mafuta na gesi yakipataikana Ziwa Tanganyika, sisi na Congo na Zambia mambo yatakuwaje? Tukienda Ruvuma Basin tukapata gesi na Mozambique wana gesi hiyo shared resource itakuwaje?

Kwa hiyo, tuweke mkazo kwenye utafutaji wa gesi na mafuta na wataalamu wapo tumewasomesha ambao mimi nawafahamu tumewasomesha Norway tulipeleka Masters 40, hatujui wanafanya kazi gani? China tulipeleka Masters Ph.D 100, vijana wengi wamesoma kwenye oil and gas hawana kazi.

Sasa natural gas; uchumi wa gesi kwa Tanzania matumizi ya kufanya uchumi ukue cha kwanza kabisa tuzalishe umeme yaani kilowatt hour moja hiyo unit moja inahitaji cubic feet 7.36 kuzalisha unit moja ya umeme na sisi tuna materials na uzuri wa umeme na gesi hauna ukame, hauko capital intensive. Kwa hiyo, umeme mwingi tungeutoa siyo kwamba tunasimamisha maji, lakini tungewekeza sana kwenye gesi tupate umeme mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha pili, uchumi wetu kukua kutokana na natural gas.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja malizia Profesa.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Spika, ni mambo ya mbolea na mambo ya viwandani.

Sasa nimalizie hiyo dakika moja kwa biashara ya LNG. Biashara ya LNG itatusaidia kwa sababu duniani sasa hivi kufika mwaka 2030 biashara hiyo itakuwa na ukubwa wa dola bilioni 210; Tanzania lazima ipate pale. Msumbiji wana LNG plants mbili, ya kwanza inaitwa Floating LNG ambayo gesi wameenda kuichukua huko huko baharini na wameanza kusafirisha tani 13,000,000 kwa mwaka za LNG na nyingine wanayoitengeneza wataanza na tani 12,800,000 lakini wataenda mpaka milioni 43,200,000. Kwa hiyo Tanzania kama tunataka uchumi wetu ukue kwa haraka ni lazima tuwekeze kwenye umeme, tuzalishe uwe mwingi, halafu lazima twende kwenye uchumi wa gesi na huu uchumi una vitu vingi sana na ushauri mwingine ni kwamba kwa sababu kuna viwanda vingi kama hivi nimewaambia umeme, mbolea na viwandani kabla haujampatia mshindani wako gesi yako, nadhani ni busara umpatie bidhaa zinazotokana na gesi kuliko kumpatia gesi yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)