Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Spika, kwanza niweze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaendela kuifanya kwa ajili ya Watanzania, lakini pia nimpongeze Waziri wa Fedha, Naibu wake, Katibu Mkuu na taasisi ya TRA ambayo inakusanya mapato kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bajeti hii kwa kweli imetoa mwelekeo kwa wananchi maskini, hasa kwenye vyuo ambavyo ni vyuo vya ufundi kuwa na ada bure. Hili tunakwenda kuongeza wataalam ambao walikuwa wanabaki, wanapochaguliwa na Serikali kwenda kwenye vyuo hivyo wanakosa ada. Kwa hiyo, hapo tumekwenda kumgausa mwananchi moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye vyuo vya kati vya sayansi afya na mambo mengine, kutoa mkopo ambao W abunge hawa mmeridhia miaka yote ili hawa wanafunzi waweze kupata mikopo na wao waweze kusoma kwa sababu wengi walikuwa wanabaki. Napongeza sana na ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Rais kwa kukubaliana na jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi nilimsikiliza vizuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, alisema tozo siyo za Rais, tozo siyo za Waziri Mwigulu na mimi nakubaliana na yeye, tozo ni za Watanzania kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Kama kuna tozo vikwazo ni nafasi yetu sisi Bunge kuziondoa tozo hizo vikwazo, kuliko kumuachia mzigo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba kushauri hapa ili angalau tuone ni namna gani hawa wafanyabiashara wanaweza kukwepa kodi kwa sababu ya tozo vikwazo na naomba nianzie na service levy. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, msingi wa service levy uliwekwa kwa ajili ya viwanda wanapozalisha wanatozwa service levy kwa ajili ya Halmashauri zetu. Lakini msingi wake ulitokana na kwamba ili hii service levy itozwe ni kwamba Halmashauri zetu baada ya kuangalia mauzo ambayo yanauzwa kwenye Wilaya zetu, yanapeleka moja kwa moja viwandani, viwanda vinalipa. Naomba nitoe mfano, pale Ilemela Kiwanda cha Bia service levy Halmashauri ya Ilemela inatoza moja kwa moja pale, lakini hata yule agent ambaye kiwanda kinamuuzia kwenda pale pale mita 100, na yeye akiuza Halmashauri inamtoza kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini bidhaa hizi zote ukiangalia kwa mfano tu nataka nitoe mfano, bundle moja ya bati mfanyabiashara ananunua shilingi 370,000 ukimtioza 0.3% sawa sawa na shilingi 1,100 lakini huyu anapata shilingi 1,400. Je, atakuwa tayari kutoa risiti? Ndio maana sasa unakuta wafanyabiashara hawatoi risiti kwa sababu wakitoa risiti, service levy inakwenda kuwa nyingi kuliko faida ambayo anapata mfanyabiashara. Kwa hiyo, hapa tunakwenda moja kwa moja kupunguza mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, service levy mwanzo msingi wake ilikuwa ni income, lakini leo wanatoza kwa revenue. Income maana yake ni kwamba umeshatoa matumizi yote na gharama zote, kinachobaki ndicho kinachopaswa kutozwa, lakini wao sivyo, kwa hiyo, ndiyo maana sasa tunakwenda wafanyabiashara wanakwepa kutoa risiti kwa sababu ya vikwazo hivyo na hilo wanajifanya sasa wafanyabiashara kuandamana kwenye mambo haya. Sasa lawama zinamrudia Mheshimiwa Rais, zinamrudia Waziri wa Fedha lawama, kumbe vikwazo hivi inapaswa tukae chini tuangalie je, tutoze kwa revenue? Je, tutoze kwa income au tupunguze badala ya 0.3% tuwe na 0.03% hapo ndipo sasa risiti zote zitatolewa, nilitaka kushauri hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shilingi 100 ambayo imeongezwa kwenye mafuta kwanza niwatoe hofu Watanzania na niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, nataka tu kutoa mfano, lori likipakia lita 1,000 kule Dar es Salaam kubeba mzigo kwenda Mwanza inayoongezeka ni shilingi 100,000 tu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hiyo unaweza ukasema kwamba inaweza kupunguza gharama za uendeshaji au kuongeza gharama za uendeshaji. Kwa hiyo, mimi nataka kusema kwamba kwa sababu soko la dunia la mafuta hatuna uwezo nalo, kuna kushuka na kuna kupanda kodi hii inakwenda kutusaidia kwenye miradi ya kimkakati hasa kwenye kilimo ambapo kwa kweli Watanzania wengi wapo kwa sababu tunaweza kutengeneza hofu, lakini tukashindwa kutengeneza huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi naendelea kusema kule Magu mahindi yanakauka kwa sababu ya kukosa maji. Kwa hiyo, hii shilingi 100 pamoja na kwenda kwenye miradi ya kimkakati hasa reli ya Standard Gauge lakini pia lazima iende kwenye kilimo kwa ajili ya umwagiliaji ili wananchi wetu waweze kupata mapato ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nasikitika kidogo na ninashangaa sana sijui wataalam hawa Waziri wa Fedha wanakushauri vizuri? Leo Serikali imetoa ruzuku ya mbolea, Serikali imetoa ruzuku ya mbegu, watu wamelima vya kutosha, alizeti Mwanza, Simiyu, Tabora, Singida, Mbeya na Iringa na maeneo mengine Babati imelimwa ya kutosha; pamba ipo ya kutosha, mikoa 17 inayolima pamba. Kwa hiyo, tuna uhakika wa kuwa na mafuta mengi ya kutosha kwenye nchi hii, kwa hiyo, unapokwenda kutoa kodi kwa mafuta yanayotoka nje unaweka 25% badala ya 35% unakwenda kuwafanya wakulima wa nchi hii kwa masikini, siyo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili siyo sawa, halafu unakwenda kuongeza 18% VAT kwenye mafuta yanayozalishwa nchini unatoa ya nje, kwa kweli hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha hawakukushauri vizuri. (Makofi)
Naomba nishauri Serikali, hatuwezi kuongeza ajira ya wakulima wetu, hatuwezi kuongeza ajira kujenga viwanda kama kodi za mafuta yanayotoka nje tunazipunguza. Napendekeza 35% ya mafuta yanayotoka nje iwekwe ili kuhakikisha kwamba wakulima wetu wa alizeti wanapata bei nzuri, wakulima wetu wa pamba wanapata bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haiwezekani tukatajirisha nje, tukawaweka wananchi wetu kuwa maskini, hili haliwezekani. Nishauri sana, naunga mkono lakini kwenye hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha nitashika shilingi. Kama 35% haitawekwa, kama VAT haitaondolewa kwenye mafuta ya ndani, hili nitashika shilingi kwa sababu tunakwenda kuwatia umaskini wananchi na hivi viwanda vinamilikiwa 80% na Watanzania. Leo ukiruhusu hiyo 25% maana yake viwanda vyetu vinakwenda kufa. Hili siyo sawa, niombe sana kwa kweli Waziri wa Fedha unafanya kazi vizuri, lakini katika hili niombe kwa kweli lazima tulinde wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakuja kwenye ngano; ngano tunalima, kule Njombe wanalima, kule Katavi wanalima, kule Arusha, Babati wanalima, lakini mapendekezo ya wataalam wako Mheshimiwa Waziri yanasema unaondoa 35% unaweka 10%. Sasa hawa Watanzania wanalima ngano ya nini? Kwa sababu ukipunguza tu kodi ya ngano nje maana yake kwamba unamfanya mkulima wa Tanzania asiendelee kulima. Sasa hapa tunakuza uchumi? Hapa tunakuza uchumi au tunakuza mapato? Haiwezekani, lazima tuwe tayari, tumetoa mbegu za ngano, tumetoa ruzuku kila mahali, kwa hiyo lazima tulinde wakulima wetu na tulinde biashara ya Tanzania na niombe sana hapa, kama tuna mazao ambayo ni ya kimkakati ambayo yanaweza kwenda kuinua uchumi na kupunguza fedha za kigeni kwenda nje lazima tuyalinde kwa wivu, tusiyaachie hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili Bunge ndilo ambalo linaweza kutengeneza mwelekeo wa uchumi kwa nchi hii. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri mimi nataka uwe na uwezo wa kukusanya fedha ili heshima ya nchi iwepo ni mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapokwenda kupunguza kodi, tunapunguza mapato. Ili heshima ya familia iwepo ni mapato kwenye familia. Familia ukikosa baba wa familia hela hauna heshima. Kwa hiyo, tunapokwenda kupunguza mapato kwa sababu ya vitu kutoka nje tunakwenda kupunguza heshima ya nchi. Lazima tujitegemee, tutaendelea kukulaumu, tutaendelea kumlaumu Mheshimiwa Rais, lakini lazima tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Sekunde 30.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, naomba ni-declare interest mimi ni Mwenyekiti wa Wachambuaji wa Pamba Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2019 Serikali ilisema wanunuzi wa pamba wanunue pamba kwa bei yoyote itafidia. Bunge lako limeshatoa azimio na hawa wafanyabiashara 100% ni Watanzania. Leo benki interest zinaendelea kuwa cruel. Niombe kwa sababu ni Azimio la Bunge na fedha tunaamini zipo, Mheshimiwa Waziri aone namna ya kuweza kulipa ili kuwawezesha hawa wafanyabiashara na kuwezesha viwanda viweze kuendelea. Hatuwezi kulipa madeni ya nje tushindwe kulipa madeni ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)