Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipatia fursa ya kujadili au kuchangia bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/2024; lakini na Mpango wa mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa mwaka 2023/2024 dhima yake ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha sekta za kiuzalishaji ili kuboresha maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini na mpishi mwenyewe Waziri wa Fedha. Hii kauli ya kuboresha maisha nimeipenda sana. Kama unaita majina, Mheshimiwa Mwigulu kama uliita jina wewe hili unajua kuita majina, tunataka kuboresha maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, taarifa kama tulivyoisikia na katika maandishi, utekelezaji wake ni mzuri na ni wa kiwango cha juu, ni kutokana na taarifa lakini ni kutokana na kule tunakoishi nchi nzima, uraiani kwetu, mikoani kwetu, utendaji unaonekana.
Mheshimiwa Spika, ziko dalili wazi; miradi ya umeme vijijini inaendelea, ujenzi wa mashule ikiwemo vyuo vya VETA, ninapozungumza VETA Kijiji cha Bushagara, VETA inajengwa inaendelea, lakini jitihada za Serikali za kuweka pesa katika mabenki TIB ili kuwaongezea watu ukwasi na kuweza kukopa. Lakini jitihada za Serikali katika miradi ya maji, tulikuwa na miradi ya maji 586, kipindi tulichomaliza, nimeiona kwa macho yangu katika Jimbo langu, nimeiona popote napopita Tanzania katika kamati ulizotutuma, lakini mpango wa Serikali wa kutengeneza miradi 1,293 mimi inanituma bila wasiwasi kuunga mkono bajeti hii ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bila kuisahau TARURA niipongeze Serikali kwa mpango wake wa kutenga pesa zaidi kwa idara hii ya TARURA, ili tuweze kutengeneza barabara ziweze kuwafikia wananchi.
Mheshimiwa Spika, linazungumzwa suala la uchumi wa dunia, wanazungumza uchumi wa dunia na kiashiria rahisi cha uchumi wa dunia ni takwimu. Mimi ningependa niwaeleze Watanzania na Wabunge wenzangu viashiria rahisi vya kujua uchumi wa dunia ni mzuri, lakini sisi kiongozi wetu na wasaidizi wake akiwemo Waziri wa Fedha, tumeweza kuudhibiti uchumi. Wakati kuna nchi sio za kutafuta, ndege zilishindwa kuruka, magari yalishindwa kutembea kwa kukosa mafuta, tatizo hili hapa kwetu halikutokea. Wakati kuna nchi watu walilala njaa, Serikali kabisa viongozi wakuu walihangaika wakitafuta chakula sisi hapa hatukukosa chakula. Yupo rafiki yangu aliwahi kuniuliza unamfahamu Waziri wa Kilimo, nikasema yule ni mtumishi mwenzangu akasema kamshukuru. Nilikuwa na shida na njaa kwetu nikamwambia akaandika karatasi NRFA wakapeleka chakula, sisi hatukulalamika na chakula. Kwa hiyo, Serikali imeudhibiti uchumi huu wa dunia kwa tafsiri ya kirahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mtanzania yeyote ajipime kwa hilo ulikuwa kwenye kituo cha mafuta ukakosa mafuta, haikutokea, lakini kuna nchi zimekosa mafuta, zimekosa chakula. Watu wamekuwa na black out, umeme umeshindwa kuwaka wakataka black out, lakini Tanzania hatukuweza kuingia katika hilo. Baya zaidi kuna nchi katika bajeti zao walisimamisha bajeti za maendeleo, yaani Serikali imetengeneza bajeti mwaka jana kwamba maendeleo yasitekelezwe, lakini Tanzania hakuna mradi uliosimama. Kama anavyosema Mheshimiwa Rais hakuna kilichosimama na kweli hakuna kilichosimama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipongeze Serikali na Mheshimiwa Waziri umeweka msingi wa bajeti ambao ni kazi kubwa na kazi lazima ifanyike. Msingi mmoja wa bajeti unasema kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara.
Mheshimiwa Spika, ili bajeti yetu iweze kufanikiwa ni lazima kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi. Mimi nina ushauri wa mambo mawili. Tunapoizungumzia sekta binafsi tusiangalie wakubwa tu, hata hawa wadogo wanaolima kilo mbili za maharage, wanaolima mahindi na wao twende nao. Sekta binafsi ni mzalishaji yoyote, tusikimbilie wale wakubwa. Suala la pili ninaloomba unapozungumza sekta binafsi kuna sekta binafsi ya Tanzania na sekta binafsi ya Kitanzania.
Mheshimiwa Spika, nimshauri Mheshimiwa Waziri lazima sekta binafsi ya Kitanzania tuifikirie. Tungependa watoto wetu tuwaweke katika shughuli kusudi wasije kuwa watazamaji kwenye mchezo ambao waliuanzisha wao. Niipongeze Serikali hasa Mheshimiwa Waziri, umezungumzia juu ya mamlaka za udhibiti, ukazungumzia na TRA, lazima kama tunaitegemea sekta bonafsi basi mamlaka za udhibiti zifanye mazingira ya kufanya shughuli yawe mazuri, wasiwe kikwazo. Siwezi kuongezea zaidi namna ya kutekeleza hii, ni kutembea na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, lakini ni kutembea na maneno yako ambayo uliyatoa kwa maneno yanayoeleweka.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie Tume ya Mipango, tuliomba Tume ya Mipango, Wabunge tumezungumza Tume ya Mipango, hatimaye Tume ya Mipango iko kazini.
Ombi la kwanza Serikali, mamlaka Tume ya Mipango muwape majukumu lakini muwape mamlaka na wawajibike kwayo (authority, responsibility and accountability). Tungependa Tume ya Mipango ituongoze, tunatengeneza dira lakini dira bila Tume ya Mipango haiwezi kufika mahali popote. Unaweza ukawa na mali nyingi, ukakusanya rasilimali nyingi ukazitumia, lakini ukazitumia bila mpango. Sipendi kuzungumza mengi zaidi tuna imani na Tume ya Mipango, lakini Tume ya Mipango iwe wazi ili kusudi watu waweze kutoa mawazo yao.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie dhima ya mwaka wa fedha ujao inayosisitiza kuimarisha sekta za uzalishaji ili kuboresha maisha. Hili neno kuboresha maisha kuna ndugu yangu mmoja anaishi Songwe huko analipenda na mimi nimelipenda zaidi naona Mheshimiwa Waziri ameiga kwako, tuboreshe maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo kuhusu urari wa biashara ya bidhaa na huduma, katika urali wa biashara wa bidhaa na huduma mwaka huu tunaomaliza tumepata hasi bilioni 3.87, bidhaa na huduma, lakini urari wa biashara na bidhaa tumepata nakisi ya bilioni 6.066, urari wa biashara ya huduma tumepata chanya bilioni 2.199 maana yake nini, tumeokolewa na utalii na sekta za huduma.
Kwa hiyo, kwa kuanzia lazima tuwekeze nguvu nyingi kwenye utalii, lakini hizi sekta za kiuzalishaji tulizozungumza lazima tuwekeze katika sekta za uzalishaji kusudi tuuze zaidi. Maana yake nini? Tuingie kwenye import substitution come export promotion, tuingize pesa zaidi kwa kutoka nje ndio tuweze kuhimili kutekeleza bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, naona umeniwashia taa, naunga mkono hoja. (Makofi)