Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa fursa hii na mimi nianze kwa kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu. Kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na viongozi wake kwenye Wizara hii tusimsahau Gavana wa Benki Kuu kwa kazi nzuri ambayo wamefanya na kutuonesha kwamba inawezekana mahali popote kufikia au kuendeleza uchumi wa jumla ambao ni tulivu ukiwa na inflation iliyo ndogo.

Mheshimiwa Spika, kabla sijasema machache kuhusu hii bajeti ambayo nasema ni bajeti nzuri kulinganisha na bajeti nyingine ambazo nimesoma, niseme kidogo kuhusu mambo ya jimboni kwa sababu wananchi wa Vunjo wamesema hawajanisikia.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza niseme kwamba nashukuru kwamba Serikali imeweza kuendelea kuipa TARURA fedha ya kutosha kiasi na kwa hivyo TARURA inakuwa imeendeleza kujenga na kukarabati barabara kule vijijini kwetu.

Mheshimiwa Spika, pia nawashukuru kipekee kwamba TARURA wamesikia agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwamba waweze kujenga barabara ya Himo sokoni kwenda Makuyuni na Rotima kwa kiwango cha lami, na wameanza kuijenga lakini nawakumbusha kwamba Mheshimiwa aliagiza ipate kilometa 7.4 wasije wakaishia mita 800 ambazo naona wanakazana nazo sasa hivi, naamini watafikisha kama ilivyokuwa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine tumeweza kuwasilisha kupitia Bodi ya Barabara ya Kilimanjaro, Mwenyekiti wetu amewasilisha maombi kwa Wizara ya Ujenzi waweze kupandisha hadhi barabara tatu; barabara ya kwanza ni ile ya Pofo - Kilema - Mandaka ambayo tayari wanaanza kuiweka lami, lakini kuna Uchira – Kisomachi – Kolarie; na Chekereni - Kahe hadi TPC hizo ni barabara ambazo tumeziombea sasa zipandishwe hadhi ziwe ni barabara za kimkoa, kwa hiyo, ziweze kuhudumiwa na TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kwamba sasa kwa sababu kwenye ile bajeti ya Wizara hii zaidi ya shilingi trilioni 3.7 wanaweza pia na sisi tukapata kidogo wakapokea barabara mojawapo na sisi tukapata kidogo. Hatukupata fedha yoyote au mradi wowote kwenye Wizara hii katika bajeti inayokuja.

Kwa upande wa vituo vya afya, tulishukuru pia kwamba Serikali imeweza kutupa Kituo cha Marangu Head Quarter ambacho tulipewa shilingi milioni 500 na kama kinakamilika isipokuwa kuna jengo la maternity na theater ambalo halitaweza kukamilika kwa fedha hizi. Tunaomba TAMISEMI waweze kuona namna gani wataongeza fedha hiyo, siyo nyingi sana itahitajika shilingi milioni 50 tu kuweza kukamilisha hilo.

Mheshimiwa Spika, tunaomba pia kwamba Serikali iweze kutuletea vifaa tiba ili waweze kuanza kazi kwenye kituo hiki ambacho kiko karibu sana na wananchi wengi. Pia tunaomba kituo kile cha Koresa ambacho tumeahidiwa na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aliyekuwepo basi nacho kianze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa maji nilizungumza hapa kwamba Mheshimiwa Waziri atakuja, Naibu Waziri atakuja kule ili tuweze kuhakikisha kwamba ile miradi ambayo ipo kwenye Kata zile za Mwika Kusini na Kaskazini, Mamba Kusini na Kaskazini, Marangu Mashariki na Magharibi na Kilema kwamba kazi yenyewe ziwe zinakamilisha kwa sababu ilikuwa iwe mwaka mmoja, lakini sasa imechukua miaka mitatu bado hatujamaliza.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa elimu; tuna shule tatu tu ambazo zimepewa kidato cha tano na sita. Sasa hiyo ni changamoto kwa sababu tuna shule za sekondari ya kawaida ni 32 na ushee, kwa hiyo, tunaomba kwamba sasa na hasa tukizingatia hii mitaala mpya inayoingia na mfumo mpya wa elimu tunaokuja ku–adopt basi waanze kupandisha hadhi baadhi ya shule hizi za kawaida hususani shule kwa mfano ile shule ya Mboni, kuna shule ya Kokirie, kuna shule kule Marangu na kadhalika. Tunaomba kwamba sasa tuanze mchakato wa kuainisha ili zianze kupandishwa hadhi kupata kidato cha tano na cha sita.

Mheshimiwa Spika, mwisho niseme kwamba nije sasa kwenye upande wa bajeti hii ambayo nimesema ni bajeti ambayo kwa ujumla inavutia kwa sababu gani? Kuna wakati nilisimama hapa mwaka 2022 ile bajeti tulivyokuwa tunapitisha, kwa hivyo, ile bajeti ilikuwa contractionary kwamba isiwe bajeti ya kuchochea uchumi, kwa sababu wakati ule kusema ukweli kuwa na nakisi ya bajeti ambayo ina asilimia tatu ya pato la Taifa, ilikuwa hairuhusu ina maana Serikali haikuona kwamba kuna uwezekano wa kukopa zaidi na kwenye soko la ndani wakati ule ambapo hata sekta binafsi ilikuwa haikopi, haihitaji kukopa kwa sababu mazingira yalikuwa hayaruhusu sana kufanya biashara yenye tija.

Kwa hiyo, wakati ule ilikuwa ni wakati ambao ilikuwa inatarajia kwamba Serikali itakuwa na nakisi kubwa zaidi iweze kukopa zaidi na iweze kuchochea uchumi wakati ule private sector ikiwa inaogopa risks zilizokuwepo.

Mheshimiwa Spika, lakini na pia kwa wakati ule naona huko kulikuwa hali hata riba zilikuwa ziko juu, lakini siyo Serikali hazikuweza kufanya chochote kwa upande ule. Lakini nilisema kwamba ni contraction lakini mwaka huu tunaona pia kwamba ni contraction kwa sababu nakisi kwa uwezo wa pato la Taifa iko 2.7 lakini wakati ule ni wakati wake kabisa na mimi napongeza hayo maamuzi kwamba tujaribu kupunguza matumizi na ukopaji kwa sababu hatuna uwezo sasa hivi kuna cons trait mbili, cons trait ya kwanza sasa hivi ndiyo kubwa zaidi ni hii nakisi kwenye malipo ya nje pamoja na upungufu wa dola. Sasa hiyo ndiyo inatubana kwa sababu unaweza ukawa na miradi mikubwa, lakini mwisho wa ukomo wako utaishia kwenye kuomba fedha za kigeni unazo, na kama huna utalazimika kuishia hapo.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba hapa wamesema pia wanakopa, wamepunguza maoteo ya kukopa nje kwa masharti ya biashara. Lakini utaona kwamba mimi naamini kwamba tunapoendelea kutekeleza hii bajeti utakuta kwamba tutalazimika kukopa zaidi kwa sababu tukiongeza miradi hii ambayo tunayo hatutaweza kutokulazimika kukopa zaidi nje ili tuweze kupata dola ambazo zitatusaidia kuendeleza hii miradi ambayo yenye uwezo ambayo tunaenda nayo.

Mheshimiwa Spika, mimi napongeza pia kwamba Serikali pamoja na Benki Kuu wameweza kushikilia kweli sera zao za kifedha na kibajeti na kuhakikisha kwamba uchumi wetu umebakia tulivu, inflations ni 4.3 katika mazingira ambayo ni magumu sana. Japokuwa bado naamini kwamba bado riba haziendani na hii inflation ndogo ya kiasi hiki ambayo imekaa kwa muda mrefu. Mimi naamini bado riba tuna kazi ya kufanya pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napongeza pia hii ukamilishaji wa tathimini na ukopeshakaji wa nchi yetu; fitch ratings wakatupa B2 plus na ile watakupa B+ ambayo ni nzuri (rate nzuri sana) kwa nchi ambayo inaendelea kama ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napongeza pia kwamba hiyo nisiseme, lakini nisemi hivi kuna jambo moja ambalo ninataka nishauri ili kuongeza mapato yetu na kupunguza ruzuku tunazotoa kutokana na mapato madogo, mimi nafikiri kwamba kwamba kwa upande kwa mfano wa mafuta, mafuta yanashuka bei petrol na diesel zinashuka bei, mimi nafikiri kwamba tungekuwa na threshold tukisema ikizidi 3,000 tutatoa ruzuku, tunaingiza kwenye mfuko wa ku–standardize bei za mafuta siyo Serikali iingie tena kwenye bajeti yake kutoa ruzuku tutengeneze huo mfuko kutokana na hii fluctuation’s ikishuka, ikizidi 3,000 tuwape ruzuku, ikishuka tuendelee kuchukua kwa muda kiasi halafu tuone inaendelea kushuka basi tunaji–adjust na sisi chini hivyo hivyo, hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kuwa na ruzuku ya mafuta ambayo itasaidia uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia kwamba kuna tatizo la takwimu hizi za ukuaji wa uchumi ni ukuaji wetu wa uchumi. Ukiangalia figure tulizonazo kwenye bajeti, kitabu cha bajeti uchumi wetu GDP ilikuwa kutoka trilioni 169.8 mwaka 2021/2022 ikafika trilioni 188.6 mwaka 2022/2023. Kwa hiyo, ina maana kuna ukweli wa asilimia 11 kwa bei ya miaka husika. Sasa kama ni bei ya miaka husika kama inflation ni four percent ina maana tofauti ya bei za soko ya mwaka husika na constant price inakuwa sana sana ni hiyo ya inflation ile unatoa.

Kwa hiyo, inatakiwa iwe kwamba kama ni 11.1 percent ukitoa hapo 4.3 percent unabakiwa na almost 7 percent ya real growth hasa inawezekana kwamba kuna mahali ambapo tuna-miss kidogo huo ukuaji na ukiangalia kwa dola, dola ni fedha ambayo haina inflation, inflation yake ndogo sana ile sasa hivi ni kubwa, lakini imekuwa pia kuchukua kwa dola tulizonazo, dola zilikuwa ni bilioni 77.6 iliyo pato letu hasa ikapanda mpaka bilioni 85.3 ambayo ni ukuaji wa eleven; ten percent kwa maana ya miaka hiyo miwili.

Mheshimiwa Spika, kwa nini iwe kwamba tunapokuja kwenye shilingi ni 4.3 percent au and around five percent? Sasa five percent utakuta ni chini sana kutokana na kwamba nchi nyingine average ya East Africa ni 6.3 percent.

Kwa hiyo, mimi nataka kusema kwamba tuangalie hizi takwimu zetu na kuna mahali kumejificha kitu hakijulikani na kwa nini nakubali kwamba inawezekana hivyo? Hakuna ambacho tulikuwa tunafanya miaka ile ya nyuma kabla ya mwaka 2019 na ambacho hatufanyi sasa hivi tunafanya tena zaidi, kwa nini sasa uchumi utasema bado unakuwa kwa asilimia tano? Mimi nafikiri tuangalie kuna kitu ambacho hakiendi sawa sawa na ningemuomba hapa Waziri wa Fedha kupitia Ofisi ya Takwimu aweze kuangalia na kuona atafanya namna gani.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hiyo nilijaribu kwenye swali moja nilitaka kuuliza asubuhi wakati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa sekunde 30, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)