Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, namimi nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia bajeti yetu ya Wizara ya Fedha na kama walivyosema wenzangu na mimi nianze kwa kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe shukrani zangu za dhati kwa Katibu Mkuu wetu wa Chama cha Mapinduzi, chama tawala na wazi kabisa ziara zake zinaonesha utofauti mkubwa sana wa chama tawala kilicho madarakani na vyama vya upinzani kwamba anakofika maeneo kuna kero ya maji basi anawaita Mawaziri na viongozi wanatatua kero hizo hilo ni jambo jema na jambo zuri la kuungwa mkono, tunaomba sana viongozo wote na watumishi wote wa Serikali kuhakikisha wanaenda sambamba na maelekezo ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo namshukuru Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba amenisaidia na anaendelea kunisaidia kuhusu barabara yetu ya lami ya Ifakara – Kidatu. Barabara ile iko chini ya Wizara Fedha, amendelea kusaidia kutatua changamoto na mambo yanaenda vizuri na Mheshimiwa Waziri uliniahidi kwamba utatembelea barabara ile ya lami ili ukaone ule mkeka unavyopendeza pendeza sasa hivi maana yake wanachora ile mistari ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niseme kabisa Mheshimiwa Mwigulu wewe katika kuwasilisha bajeti hatuna mashaka na wewe na ni wazi tu kwamba watozwa ushuru duniani hawajawahi kupendwa, kwa hiyo, kuna watu wengi wanaweza wasipende lakini kazi yako yenyewe hiyo ya kukusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu ni kazi ambayo kwa vyovyote vile huweza kupendwa na watu wote. Mtu akitaka kukupima tu kwa kigezo rahisi ni kwamba tulikuwa na malengo ya kukusanya shilingi trilioni 41.4; ukikusanya shilingi trilioni 41.4 ni sawa sawa na 100% na mpaka unawasilisha bajeti yako ya Wizara yako hii kwa taarifa za Aprili, 2023 umekusanya shilingi trilioni 32.4 ukifanya multiplication equation hapo tu utapata ni karibu 78% mmeweza kukusanya mapato yetu, ina maana na bajeti utekelezaji wake ni kama 78%, nawapongeza sana, tunawashukuru sana lakini lazima tuongeze nguvu ya kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano TRA walipanga kukusanya shilingi trilioni 23 lakini mpaka wanawasilisha walikusanya shilingi trilioni 18.8. Kwa hiyo ni imani yangu kwamba uwekezaji mkubwa unaendelea kufanyika utaongeza mapato katika Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti yako nimejaribu kuipitia pitia ina mambo mengi mazuri na kwa haraka haraka labda niseme kwamba suala la kufanya inflation libaki katika single digit ni jambo zuri, suala la VAT kuanza kufikiria kadirio la VAT litaanza kuanzia milioni 200 mpaka milioni 500 ni jambo zuri sana, kuweka kodi na kuongeza kodi katika mashine za kamari ni jambo zuri, lakini haitoshi, ongezeni kodi katika mashine za kamari ili ku-discourage vijana wetu kushinda katika mambo haya ya kamari na Serikali itaendelea kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umezungumza katika bajeti yako kuna suala la kuboresha adhabu za TRA zisiende moja kwa moja katika mazingira ya kutengeneza rushwa, ni jambo zuri. Tunaomba kuwe na mifumo imara ambayo itawezeshesha kupunguza mianya ya rushwa.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono taarifa ya Mheshimiwa Waziri aliyoandika kwenye bajeti yake kuhusu kuwezesha Ofisi ya CAG iende zaidi kwenye kuzuia taratibu kuvunjwa, kuliko kwenye kuona makosa na kuyaandika makosa ya Serikali. Tunapongeza kuhusu kupunguza riba kutoka 16.5% to 15%. Tunaendelea kupongeza kama alivyosema Mbunge aliyetangulia kuhusu hiyo bilioni moja ya vifaa vya walemavu ni jambo zuri sana na Mwalimu Nyerere alishawahi kusema katika Taifa hili makundi ya watu yanayopaswa kutegemea watu wengine ni wazee sana, watoto na walemavu. Kwa hiyo, jambo hili ni zuri sana kwa walemavu wetu na nchi yetu itapata baraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amezungumza mchakato wa mikopo ya 10% ya Halmashauri. Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo ya kusimamisha mchakato ulivyokuwa awali, swali letu la msingi ukija kujumuisha hapa Mheshimiwa Waziri tusaidie, vijana, akinamama huko majimboni na kwenye halmashauri wanasubiri mchakato mpya wa Mheshimiwa Rais alioelekeza kuhusu mikopo ya 10% ya halmashauri utakuja kwa utaratibu gani, na utakuja lini? Kwa sababu sasa hivi wamekaa dilemma na wanasubiri na nimeona kwenye hotuba yako umesema kwanza jambo hilo litatolewa majibu, ni vizuri mkaanzisha mapema kwa mfano Ifakara tulishaanzisha kukopesha watu pikipiki, tumesimamisha zoezi hilo linaleta manung’uniko sana.

Mheshimiwa Spika, kilimo; mwaka jana tuliongeza bajeti ya kilimo kwa shilingi bilioni 954; mwaka huu naona Waziri Bashe umempa shilingi bilioni 970; ni mapato makubwa, lakini ushauri katika suala la kilimo na tunashauri safari hii Waziri Bashe watuwahishie mbolea sisi wakulima, mwaka jana nia ilikuwa njema, lakini kwa kweli mbolea ilichelewa kidogo kuna baadhi ya maeneo ikaleta manung’uniko. Tunaomba Wizara ya kilimo itazame Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Morogoro ni ghala la Taifa, Mkoa wa Morogoro hata ukipeleka mradi wa umwagiliaji hauna haja ya kuchimba kisima, vyanzo vya maji vipo.

Kwa hiyo, tunamuomba Waziri wa Kilimo atusaidie kuangalia Mkoa wa Morogoro ni ghala la Taifa na sisi tunaongoza nchi nzima katilka kilimo cha mpunga na miwa ya sukari. Tunamshukuru Waziri Bashe ametutengenezea kitalu pale Illovo cha mbegu za miwa, nafikiri mbegu hizo zitaenda kwa wananchi na wakulima wa muwa watapata mbegu nzuri kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamuomba Waziri wa Kilimo, Waziri Bashe mpunga safari hii hautakauka kwa sababu hakuna jua la kutosha. Teknolojia ya kulima kwa mpunga kuanika kwenye majamvi ilishapitwa na wakati, Waziri wa Fedha tusaidie kuingiza mashine hizi kwa rahisi zikakaushe mpunga. Mpunga safari hii hautakauka, Ifakara kuna shida ya jua, tunaomba mashine hizi ziende kwa wakati.

Namshukuru sana Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe alinipelekea timu ya watu kuanza mchakatio wa uaratibu wa kununua mpunga kwa Ifakara pale utakaosababisha wakulima kuuza mpunga kwa Serikali kwa bei nzuri kabla ya walanguzi hawajafika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo kubwa kwenye kilimo na ushuru hapa nataka kusema vizuri. Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi na hapa nasisitiza vizuri sana naomba Mheshimiwa Spika na Mawaziri wawili wa Kilimo na wa Fedha wanisaidie.

Mheshimiwa Spika, kuna kero kubwa sana sasa katika Wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero kwa maana ya Jimbo la Mlimba, Ifakara, Malinyi na Ulanga kuhusu tozo ya chini ya tani moja. Serikali ya Awamu ya Tano na Mheshimiwa Rais Samia akiwa Makamu wa Rais alizunguka kwenye kampeni akasisitiza tumeondoa tozo ya chini ya tani moja kwa wananchi. Katibu Mkuu wa CCM Comrade Chongolo amepita juzi ameulizwa na wananchi Ifakara akasema katazo hilo halijaondolewa, lakini wananchi wanatozwa geti la Idete, wanatozwa geti la Ulanga na mpaka mkaa wanapimiwa kilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri semeni jambo hili, mwakani tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hili jmbo linatia hasira wananchi message zao wanazotuma huku ni hatari kabisa, naomba sana mlisemee jambo hili je, limefutwa na kama limefutwa toeni tamko tumefuta, chini ya tani moja watu wanatozwa. Zamani wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano hakukuwa kuna mambo ya barua na urasimu, kwa nini sasa hivi unarudishwa urasimu mwananchi aje na barua, sijui aje na nini, mbona huko nyuma haikuwepo? Hili jambo linamchafua Mheshimiwa Rais na hapa nimelisema kwa kifupi linachafua kweli kweli, wachukue hatua waseme wamerudisha au wamefuta? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nataka kusema kuhusu TASAF. TASAF mmekuja na mradi mzuri sana wa wazee wetu kujishughulisha kwenye barabara za mitaro. Kila siku Mbunge ukiamka unakutana na suala la TASAF, TASAF fedha zao pelekeni. Mtu akichimba mtaro anapata shilingi 3,000 kwa siku mtu, amefanya mitaro miezi mitatu fedha hazijaenda, watu wanalaumu, watu wanalalamika naomba sana Mheshimiwa Waziri tusaidie kupata majibu haya ili nia yako njema ya kuendelea kupunguza kero na tozo kero kwa wananchi iendelee kuwa nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ni kusisitiza kuhusu madeni, mimi nipo kwenye Kamati ya Miundombinu, Mheshimiwa Waziri tunakuomba bajeti yako tutaipitisha hapa vizuri kabisa, tunaomba wakandarasi katika Kamati ya Miundombinu tunaona kuna wakandarasi wa ndani na wa nje wanadai na madeni yenye riba, tunaomba sana myalipe. Kuna kampuni tumekutana nayo Dar es Salaam ya Mtanzania ESTEN inajenga barabara pale akina Mzee Giri, ni Tanzania hajalipwa, kuna kampuni tulikutana nayo ya CHICO lipeni makampuni haya ili yaweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nataka kusema kuhusu ukurasa wa 42 alichosema Waziri. Jambo la msingi sana Mheshimiwa Waziri amesema anaomba viongoizi wote katika nchi hii kuchukua hatua za haraka kuhusu uzembe wa miradi inayoiua fedha, watu wasisubiri taarifa ya CAG, wasisubiri mwenge, wala wasisubiri viongozi wakuu. Hili jambo tunataka tuliunge mkono. Kama tutakuwa tunapeleka fedha na Mheshimiwa Rais anatafuta fedha zinaenda kwenye halmashauri hakuna usimamizi wa kutosha, tunacheka na watu itakuwa hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la kwanza Serikali iendelee kuboresha maslahi ya watumishi, wakuu wa idara na wote wanaodai madeni, iboreshe maslahi ya Madiwani iwape vyanzo vya kutembelea Madiwani wakakague miradi, tuwasikilize Madiwani wetu wanasemaje. Nasema katika Halmashauri ya Ifakara mmeleta pesa kibao pale lakini miradi hohe hahe, anasema RC, anasema DC, hatuna hata engineer wa ujenzi, mama kaleta shilingi bilioni moja hospitali ya Halmashauri, kuna shilingi milioni 500 za Kituo cha Afya Mbasa, kuna shilingi milioni 500 za Kituo cha Afya Msolla Station, madarasa 120. Sisi na wenzetu waliopewa pesa hapaeleweki. Kwa hiyo, tutaendelea kusisitiza, atakayekasirika akasirike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)