Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia machache kuhusu hoja ya bajeti ya Serikali iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kunshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutuwezesha wote kwa pamoja tukawepo hapa mpaka siku ya leo tunajadili mipango yetu na tunaiweka katika tafsiri ya fedha.

Napenda pia nipende kuchukua nafasi hii kuukupongeza wewe kwa kuendesha Bunge hili vizuri. Umekuwa imara na kitu kinachofanya mimi nikuheshimu sana, hauna upendeleo kusema kweli pamoja na ile tree line whip, lakini umejitahidi sana kutuweka wote kwa pamoja ili tuweze kutoa mawazo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi leo mchango wangu nitaulelekeza katika Wizara ya Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Kwanza nipende kumshukuru Rais ambaye aliona umuhimu sasa wa kurejesha Wizara hii ambayo kwa miaka fulani tuliteleza kidogo na sasa hivi ameirudisha upya na anaipa uwezo na tumepata Waziri ambaye anajitahidi kuonesha ni namna gani anaweza kuleta ustawi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ya maendeleo ya wanawake, watoto na jinsia ina idara tano; ina idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jinsia na mambo mengine. Mimi nitaongelea mbili; Maendeleo ya Jamii, ukitatazama Wizara hii tunaangalia vitu viwili, watu wanaangalia maendeleo ya jamii na ndio imetoka Wizara hii. Lakini watu wa maendeleo ya jamii kazi yao wale ni walagabishi. Wale wanahamasisha maendeleo katika ngazi za chini ili watu waweze kujiletea maendeleo, lakini mimi nitaongelea kuhusu ustawi wa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu wa ustawi wa jamii ndio wamepewa mamlaka ya kisheria ya kuweza kusimamia ustawi wa jamii ya watu yaani kwa niaba ya Serikali. Wanapaswa wao kufanya kazi ya kuhakikisha nchi pamoja na mipango tuliyonayo tutajenga shule, tutajenga madarasa, tutajenga hospitali, tutajenga barabara, lakini ni lazima malengo yetu ni kuhakikisha kwmaba jamii inastawi na inakaa katika utulivu wa aina fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa hivi inapitia katika mmomonyoko wa maadili. Tunajipanga ili tuweze kurudisha maadili katika mstari. Ili tuweze kufanikiwa Wizara hii inapaswa kupata nguvu ya kibajeti ili iweze kufanya kazi yake, kwa nini?

Mheshimiwa Spika, Serikali iliandaa vyuo vya ustawi wa jamii, ikasomesha wataalam ambao kazi yao wanatoa ushauri nasaha na siyo kila mtu anaweza kufanya hiyo, wako wataalamu ambao wanaandaliwa na nchi kupitia vyuo vya ustawi wa jamii ili waweze kusaidia watu. Tunaangalia akili sijui zimekuwaje wanasema akili na zenyewe zimepotea potea, watu wanafanya mambo machafu katika nchi, watu wanabaka watoto, watu wanafanya ulawiti, yaani nchi imevurugika, na hata wazazi wanafanya mambo machafu dhidi ya watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nani ambaye anaweza kusaidia ili watu wetu waweze kurudi katika mstari. Ni watu wa ustawi wa jamii, kama kuna vyuo na kama kuna wataalamu ni kwa nini hawaajiriwi? Na kwa kweli hawa watu wanatosha kukaa ngazi ya kaya. Hawa ndio wanaweza kuangalia zile tunaziita home based violences huku chini, kama wanawake wanaonewa, kama watoto wanaonewa, hawa ni wataalam wakiwa ngazi ya kata ngazi ya vijiji, wataweza kujua na kuleta taarifa iliyo sahihi ni kwa nini, watafanya utafiti ni kwa nini nchi inakuwa hivi? Ni kwa nini watu wanamong’onyoka namna hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Serikali inaonekana inapendelea Idara ya Maendeleo ya Jamii peke yake. Ukitizama katika kitabu cha bajeti. Hata zile ajira 800 ambazo wataajiri wanaanjiri watu wa maendeleo ya jamii, ustawi jamii hakuna hata kidogo, yaani ni kama wamepuuzwa, lakini naomba Serikali isipuuzie jambo hili, lazima tuwaajiri watu warudi huku chini. Waende kusaidia watu katika ngazi ya kaya, waende kufanya utafiti, waweze…

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Ngoja amalize sentensi yake, waweze kufanya utafiti?

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Waweze kufanya utafiti na waweze kuja na taarifa sahihi ni kwa nini mambo haya yanatendeka katika jamii? Ni kwa nini watu wanabaka? Ni kwa nini watu wanalawiti watoto? Ni kwa nini kuna ushoga? Why? Lazima kuwe na watu wa kufanya hivi, hatuwezi kufanya hapa kupata taarifa kutoka juu lazima...

SPIKA: Haya kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mgaya.

TAARIFA

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nilikuwa napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge jambo analozungumzia ni la muhimu sana na Serikali itambue kwamba kuna tofauti kubwa kati ya Afisa Maendeleo ya Jamii na Afisa Ustawi wa Jamii. Kwa maana ya Social Worker na huyo Afisa Maendeleo ya Jamii. Kazi ambayo inafanywa na huyo Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye ni Social Worker ni kuangalia maadili na kila kitu mambo ya psychology na vitu vya kijamii kwa ujumla na kwa hali mbaya tuliyokuwanayo sasa hivi ulimwenguni na kwenda na mambo ya ushoga na nini, ni muhimu sana wakaajiriwa Maafisa Ustawi wa Jamii wa kutosha ili kuweza kunusuru watoto wetu na vizazi vyetu, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza unaipokea taarifa hiyo?

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, naipokea.

Mheshimiwa Spika, ni kweli lazima waajiriwe kwa sababu hawa ndio watu pekee ambao wanaweza kusaidia nchi kutoka mahali ilipo. Lakini ukitazama hata bajeti yao ukiangalia kwenye randama mimi nimepitia kwenye randama yao. Kile kifungu 5001 ambacho kinaonesha maendeleo, wamewapa shilingi bilioni mbili tu. Sasa nikawa najiuliza na zile wameziweka katika kutoa service ya social welfare, je, hapo wanapoajiriwa wanaenda kufanyaje? Wanakaa wapi? Hakuna hata hela za ajira.

Mheshimiwa Spika, hakuna hata development, hata hiyo hela iliyopo ya maendeleo ni ya kurekebisha nyumba sijui ni nini, hakuna mahali ambapo wanaonesha hawa watu wanaweza kwenda kuzama vijijini ili waweze kusaidia jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo kama sisi watu wa zamani kidogo, wakati wa Awamu ya Kwanza lilikuwepo, social workers walikuwepo, walikuwa wanakwenda kata hadi kata, kijiji hadi Kijiji, wanakwenda ngazi ya familia kuangalia ni kwa nini hata mtu akigombana na mkewe. Ninachotaka kukwambia ni kwamba vijijini hakuna siri, ukimpiga mwanamke kijiji chote kinajua. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ina maana social welfare huyu atakuja kufuatilia ni kwa nini hapa kuna ugomvi? Ni kwa nini mambo kama haya yapo? Na watu wanasema unauliza, kwa hiyo bila kuwa na watu hawa kusema kweli hatuwezi kuhakikisha kwamba kama tunataka mabadiliko tutayafanya mimi najua kwamba Waziri amekuja na programu mbalimabli, lakini hii bado inampiga chenga kwa sababu hana nguvu ya kibajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemaliza hiyo sasa niongelee magereza kidogo kabla muda haujamalizika.

Kuna majeshi mbalimbali, kuna Jeshi la Polisi, Magereza, Jeshi la Wananchi lakini kuna malalamiko yanayotoka katika Jeshi la Magereza kwamba hawa watu wako chini ya Utumishi, lakini ni Jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba unisikilize, hawa ni Jeshi wako chini ya Mambo ya Ndani lakini ajira zao na mienendo yao iko chini ya Utumishi. Lakini hawa wana-standing orders zao za Magereza ambazo zinaonesha ni namna wanavyoweza kupanda vyeo, namna wanavyoweza kulipwa, lakini hawafanyiwi hivi kwa sababu wao wako chini ya Utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa inakuwaje Jeshi linakuwa chini ya Utumishi na majeshi mengine yale yaliyobaki yako chini ya mfuko unaitwa Consolidated Fund wale wanahudumiwa huko, hawa wanashindwa kama Polisi, TISS na watu wengine wao wanakwenda na mfuko wa Consolidated Fund, lakini hawa wako chini ya Utumishi. (Makofi)

Mimi napenda kujua na nitoe ushauri kwa nini Serikali hailioni hili na ni kwa nini hawatoi watu wa magereza katika Utumishi? Sasa wanakuwaje Jeshi wa Magereza halafu huku wanaongozwa na Sheria za Utumishi, kwa hiyo mahali pengine hawatendewi haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu posho zao za vyakula, posho za malazi, posho za mavazi. Kwa hiyo, tunaomba Serikali isikie au tuishauri kuwapandishia posho kutoka shilingi 10,000 kwenda shilingi 15,000 maisha yamepanda angalau. Wapewe uniform zao, wajinunulie wakati mwingine wanalaliwa wale na hawana mahali pa kulalamika. Kwa hiyo, wapewe pesa zao za mavazi, wapewe pesa zao za chakula, za umeme, za maji; wajilipie kila mtu kwa bajeti yake. Kwa sababu kipato cha Askari Magereza kwa kweli ni kidogo sana. Ili waweze kufanikiwa na wenyewe waweze ku-enjoy kazi yao naomba Serikali, nakuomba Waziri wa Fedha kupitia kwa Spika wewe uende utazame hili, maana sasa hivi tunatoa ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo mimi sina mengi kwa leo, nashukuru sana na ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)