Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, lakini nikushukuru wewe pia kwa nafasi uliyonipa ya kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza mchango wangu ningependa pia kutoa shukrani kwa Wizara ya TAMISEMI kwa kunielewa baada ya kuwa nimelia muda mrefu humu ndani kutokana na changamoto za Halmashauri yangu. Namshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa kuniletea mtu makini sana pale wilayani kwangu. Ni makini sana huyu mtu, huyu ni Mkuu wa Wilaya anaitwa Mr. Kanuni, hapa ni kanuni kweli kweli, na nafikiri vilio vyangu vilivyokuwa vikifululiza hapa kuhusiana na changamoto zinazojitokeza katika halmashauri yangu zitapungua kwa muda mfupi tu aliokaa Mheshimiwa huyu nimeona matunda yake makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo nianze moja kwa moja na mchango wangu, na mchango wangu utajielekeza katika maeneo mawili; eneo la kwanza litahusiana na masuala ya Wizara ya kilimo, na hapa moja kwa moja nitajielekeza kwenye zao la korosho.

Mheshimiwa Spika, kwa nini ni zao la korosho? Ni kwa sababu zao la korosho limekuwa likituongezea sana pesa za kigeni ambazo ni muhimu sana katika muhimili wa uchumi wa nchi hii. Kwa mfano, mwaka 2017/2018 korosho ililiingizia pato la Taifa dola takribani milioni 500, pesa hizi ni pesa nyingi sana katika uchumi, na imekuwa ikifanya hivyo kwa wastani kiasi hicho hicho kama miaka mitatu minne mfululizo hivi, lakini ninazungumzia suala hili sasa hivi kwamba uzalishaji wa korosho umeshuka kwa kiasi kikubwa sana, jambo ambalo nafikiri tunahitaji kila sababu ya kujiuliza kwa nini kushuka kwa namna hii.

Mheshimiwa Spika, mwaka takribani 2017/2018 kulikuwa na uzalishaji wa korosho wa tani 313,000 hivi, lakini kutoka hapo mpaka kufikia mwaka 2022 kumekuwa uzalishaji ukishuka kwa kiwango kikubwa sana kufikia kutishia amani ya lengo letu tulilojiwekea la kuzalisha tani 700,000 kwa mwaka. Kutoka tani 313,000 mwaka 2022/2023 korosho zilizalishwa kwa tani 186,000 hivyo kufanya mchango wa zao hili kwenye pato la Taifa kushuka kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada kubwa anazozifanya Mheshimiwa Rais kutaka kuboresha zao hili, lakini kumekuwa na mambo ya makusudi kabisa yanayoonekana kuwa ni uzembe unaosababisha kushuka kwa zao hili. Kwa mfano, hivi ninavyokwambia tayari pembejeo zimeshafika ambazo Mheshimiwa Rais kwa jitihada yake kubwa sana aliifanya kuzileta hapa nchini. Nashukuru pia Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Bashe na wasaidizi wake wa karibu walifanya jitihada za kuhakikisha kwamba, pembejeo hizi zinaingia nchini, lakini cha kushanganza mpaka sasahivi hizi pembejeo bado hazijagawiwa. Jambo ambalo linatia shaka kwamba, ni kwa sababu gani hizi pembejeo hazigawiwi licha ya kuwa zimekuja hapa ni mwezi mzima sasa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo yanatakiwa kutoa pembejeo hii ni maeneo ambayo kwa sasa hivi wanatakiwa wajiandae na masuala ya kupulizia, kwa mfano katika Wilaya ya Masasi, Jimbo la Lulindi, takribani kata zote sasa hivi zinahitaji pembejeo, lakini so far ni kata chache sana wamepewa pembejeo na kuna maeneo mengine tunashangaa unapeleka mfumo uliotumika sasa hivi ambao ni mfumo bora wa kupata idadi halisi ya wazalishaji, lakini coupon zinakwenda, zile coupon hazina idadi ya pembejeo inayotakiwa apewe mzalishaji. Unakuta umeambiwa fulani utapewa pembejeo, unapewa coupon, ukienda pale hakuna chochote. Kwa hiyo, sasa tunashangaa tatizo ni nini?

Mheshimiwa Spika, ni uzembe kama nilivyosema kwa kweli, na hali hii inafanya kuwakatisha tamaa viongozi wetu wakubwa kwa sababu wao wana ndoto ya kuona kwamba zao hili linakwenda vizuri, liendelee kuzalisha, lakini pia liendelee kutoa mchango mkubwa kama ilivyokuwa ikifanya hapo mwanzo kwenye uchumi wa nchi hii. Ni muhimu kwa sababu inapunguza urari, I mean ile deficit ya urari wa biashara. Sasa kama hali itaendelea kuwa hivi kwamba, inashuka kila siku bila shaka hata hiyo faida hatutaiona.

Mheshimiwa Spika, lakini nilitaka niongelee pia kwamba zao hili limekuwa tegemezi sana kwa baadhi ya taasisi katika hii nchi. Ni kwamba pesa nyingi zimekuwa zikitoka kwa mfano, kila kilo moja ya korosho imekuwa ikikatwa pesa kadhaa kwa maana ya tozo kwa ajili ya kuhudumia hizo taasisi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Korosho wanapata shilingi 30 katika kila kilo; Halmashauri wanapata shilingi 65 kwenye kila kilo; Chuo cha Naliendele wanapata shilingi 15 kwenye kila kilo; Chama Kikuu cha Ushirika wanapata shilingi 30 kwenye kila kilo; Chama cha Msingi wanapata shilingi 25 katika kila kilo; Halmashauri inachangiwa pia elimu shilingi 30 katika kila kilo; lakini cha kushangaza hata mfanyabiashara yule anayenunua korosho anachangiwa kwa kusafirishiwab korosho zake mpaka kwenye eneo anakotaka kuzipeleka.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia hapa utakuta kwamba ni zao pekee lenye pesa nyingi sana za tozo, lakini licha ya umuhimu huu zao hili hawa wanaochangiwa wanalidharau kwa maana ya kwamba hawafanyi kazi inayostahili kuhakikisha kwamba zao hili linakuwa bora.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kuna shida hapo na uzalishaji imeshuka, lakini halikadhalika kuna shida ya bei. Mwaka jana ni mwaka ulikuwa very worse, bei ilishuka kwa kiwango cha ajabu kabisa na kama unakumbuka nilishauliza hapa kwamba taratibu gani zinafanyika na Serikali kuhakikisha ile bei inaimarika, lakini mpaka sasa hivi bado hakujawa na majibu yaliyokuwa yanaleta matumaini kwa wakulima kwamba, hizi bei zitapanda au huu uzalishaji utapanda. Kwa kweli ni jambo ambalo tunatakiwa tujitathmini sana kwa umakini kama kweli tunataka kuendeleza zao hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine nililotaka kulizungumzia kwa siku ya leo ni kuhusiana na udhibiti wa mifumo; kumekuwa na mifumo mbalimbali ambayo imetengenezwa so far, ni jambo jema sana kwa Serikali kwa sababu ya nia nzuri ya kutaka kudhibiti mapato ya Serikali kwa namna moja au nyingine katika level mbalimbali, level ya Halmashauri, lakini hadi kwenye Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, mifumo iliyowekwa ni mizuri japo kwa kiasi kikubwa kuna changamoto kwamba tulikuwa tunategemea sana katika suala la uboreshaji paboreshwe katika mfumo wa I mean internal control system, mfumo wa control system. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, muda wako umekwisha.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, baada ya kusema hayo niunge mkono hoja, ahsante. (Makofi)